Rais Uhuru Kenyatta atimua mawaziri

Nairobi. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ametimua mawaziri wawili kwenye mabadiliko ya baraza lake aliyotangaza jana.

Katika mabadiliko hayo, Mwangi Kiunjuri ameondolewa kama Waziri wa Kilimo na nafasi yake itachukuliwa na Peter Munya, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Waziri wa Biashara.

Rais huyo wa nne wa Kenya, alimtoa rasmi Henry Rotich kama Waziri wa Fedha na nafasi yake imechukulia moja kwa moja na Ukur Yattani, ambaye alikuwa anakaimu nafasi hiyo siku za karibuni.

Rotich, aliwekwa pembeni kutokana na kukabiliwa na kesi mahakamani kwa tuhuma za ufisadi wa fedha za ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror.

Pamoja na kuwa Rais Kenyatta, hakutaja majina ya Kiunjuri na Rotich, lakini alipoulizwa kama wamefukuzwa kazi, alijibu: “Wale ambao sijawataja majina yao ina maana hawana nafasi kwenye baraza kwani maisha yetu Kenya lazima yaendelee.”

Katika mabadiliko hayo ya mawaziri aliyotangazia katika Ikulu ya mjini Mombasa, seneta wa zamani wa Nyeri, Mutahi Kagwe na Betty Maina wameula kutokana na kuteuliwa kuongoza wizara za afya na viwanda.

Maina, alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mazingira kabla ya uteuzi huo na sasa amepandishwa kuwa Waziri wa Afya wakati Kagwe ambaye alikuwa nje ya baraza hilo anachukua nafasi ya Sicily Kariuki, ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Maji.

Kariuki anachukua nafasi ya Simon Chelugui, ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Kazi, wizara iliyokuwa chini ya Yattani.

Mawaziri wanawake Rachel Omamo watabadilishana wizara, ambapo Waziri wa Mambo ya nchi za Nje, Monica Juma atakuwa Waziri mpya wa Ulinzi akibadilishana na Omamo, ambaye alikuwa anashikilia nafasi hiyo.

Mawaziri ambao hawakuguswa na mabadiliko hayo ni pamoja na Fred Matiang’i (Mambo ya Ndani), James Macharia (Usafirishaji), Najib Balala (Utalii na Maliasili), Amina Mohamed (Michezo na Utamaduni), Adan Mohamed, (Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Eugene Wamalwa (Tawala za Mikoa) na Charles Keter (Nishati).

Wengine ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Joe Mucheru, Margaret Kobia (Jamii na Jinsia), John Munyes (Madini na Mafuta), Keriako Tobiko (Mazingira na Misitu), Farida Karoney (Ardhi na Mipango Miji) na George Magoha (Elimu).