Rais Xi asema virusi vya corona changamoto kubwa

Beijing. Rais wa China, Xi Jinping amesema nchi yake inakabiliwa na hali mbaya kutokana na virusi vya corona kuenea kwa kasi huku watu 1,975 wakiliripotiwa kuwa wameambukizwa.

Leo Jumapili China imezidisha vizuizi vya usafiri ili iweze kupambana na virusi vya corona ambavyo Rais Xi Jinping amesema ni tishio kubwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la China, Xinhua, serikali ya China imesimamisha shughuli za kuwatembeza watalii kutoka mataifa ya nje, pia hakutakuwapo safari za mabasi yanayotoka na kwenda mikoani kuanzia Jumapili katika juhudi za kupunguza kuenea kwa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona.

Mlipuko huo unaaminika kuwa ulianzia katika eneo la mashariki mwa China katika mji wa Wuhan na umesambaa hadi katika nchi zingine kadhaa kama Marekani, Ufaransa, Japan na Australia.

Watu wapatao 1,975 wanaaminika kuwa wameambukizwa, na vifo 56 vimeripotiwa. Taarifa ya serikali  imesema watu 324 wamo katika hali mbaya. Wakati huohuo serikali ya China imeweka karantini yaani imezuia kuingia au kutoka kwenye mkoa wa Hubei ulio katikati mwa nchi hiyo, ambao pia umeathiriwa vibaya, ili kudhibiti maambukizi zaidi.

Katika hatua nyingine, kiongozi wa Hong Kong, Carrie Lam ametangaza hali ya dharura kuhusu virusi vya corona katika jiji hilo na serikali yake imetangaza kufungwa shughuli za usafiri, shule na vyuo vikuu.

Visa vitano vya maambukizi ya virusi vya corona vimeripotiwa katika jiji la  Hong Kong na watu zaidi ya 122 wanadhaniwa kuwa na virusi hivyo.

Shughuli mbalimbali zimefungwa wakati ambapo raia wengi wa Hong Kong wanasherehekea mwaka mpya.

Ndege na safari za reli ya mwendo wa kasi kati ya Hong Kong na Wuhan zimesimamishwa, huku shule na vyuo vikuu vikiendelea kufungwa hadi Februari 17.

Katika mji wa Wuhan, ambako karibu visa 2000 vya mambukizi na vifo vingi vimeripotiwa, matumizi ya magari ya umma yamepigwa marufuku na usafiri wa kuingia na kutoka nje.

Serikali ya China Ijumaa ilitangaza kwamba mji wa Wuhan utajengewa hospitali yenye takriban vitanda 1,000 ili kukabiliana na janga hilo, ambayo ujenzi wake utakamilika Februari 3.