VIDEO: Viongozi G20 waapa kupambana na corona

Muktasari:

Viongozi wa nchi zenye nguvu kiuchumi duniani (G20) wamekutana kwa dharura katika kikao kilichofanyika kwa njia ya video kujadili jinsi ya kukabiliana na maambukuzi ya virusi vya corona (CODIV-19).

Washington D.C. Viongozi wa nchi zenye nguvu kiuchumi duniani (G20) wamefanya mkutano wa dharura kwa njia ya video wakiahidi kushirikiana katika kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 pamoja na kutoa msaada wa kifedha.

Katika taarifa yao ya pamoja, viongozi hao wamesema “virusi hivyo havijali mipaka,” hivyo, wameahidi kutoa zaidi ya Dola za Marekani trilioni 5 katika uchumi wa dunia ili kupambana na athari za kijamii, kiuchumi na kifedha zilizosababishwa na ugonjwa huo.

Baadhi ya viongozi walioshiriki mkutano huo ni Boris Johnson wa Uingereza, Justin Trudeau wa Canada, Narendra Modi wa India, Vladmir Putin wa Urusi, Shinzo Abe wa Japan na Donald Trump wa Marekani.

Mkutano huo pia uliwahusisha Rais wa China, Xi Jinping na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ambaye alishiriki akiwa nyumbani kwake mjini Berlin ambako yuko katika karantini baada ya daktari aliyempa chanjo ya nimonia kukutwa na virusi vya corona.

Pia, mkutano huo wa kilele uliwashirikisha viongozi wa Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

Wakati hofu ikiendelea kuongezeka kuhusu mdororo wa kiuchumi ulimwenguni, viongozi wa G20 waliahidi kushirikiana katika kupambana na mlipuko wa ugonjwa huo pamoja na kutoa msaada wa kifedha.

Kwa mujibu wa shirika la habari la DW, viongozi hao waliahidi msaada mkubwa kwa mataifa yanayoendelea ambako virusi vya corona huenda vikasambaa zaidi baada ya kuathiri nchi ya China na kisha mataifa ya Ulaya.

Katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres aliwaeleza viongozi wa G20 kuwa “tupo katika vita na kirusi na hatuonekani kushinda vita hivyo” licha ya hatua kubwa zinazochukuliwa na nchi mbalimbali kuifunga mipaka yake, kufunga biashara na kuamuru zaidi ya robo ya watu duniani kubakia majumbani mwao.

“Lazima tuwasaidie walio katika hatari kubwa, mamilioni kwa mamilioni ya watu ambao hawana uwezo wa kujilinda. Hili ni suala la mshikamano wa kibinaadamu,” alisema Guterres katika mkutano huo.

Saudi Arabia ambayo inashikilia urais wa G20 mwaka huu, iliufungua mkutano kwa ombi la dharula kutoka kwa Mfalme Salman kwa mataifa yenye nguvu zaidi duniani kufadhili utafiti na utengenezaji wa chanjo dhidi ya virusi hivyo.

Zaidi ya watu 500,000 duniani kote sasa wameambukizwa virusi vya corona na kuilemea mifumo ya huduma ya afya hata katika mataifa tajiri na kusababisha serikali kuchukua hatua za kuwafungia raia majumbani mwao na kuvuruga maisha ya mabilioni ya watu.

Huko Marekani, zaidi ya watu 85,500 wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya ugonjwa wa corona na kuipiku Italia ambayo imeripoti vifo vingi zaidi na China ambako virusi hivyo vilianzia Disemba 2019.