Waliokufa kwa corona wazidi 900

Muktasari:

Ni baada ya watu wengine 97 kufariki dunia kwa siku moja.

Wuhan, China. Jumla ya watu 97 wamepoteza maisha kwa siku moja kutokana na virusi vya corona.

Watu hao wamefariki dunia Jumapili iliyopita imeweka rekodi kuwa ndio idadi kubwa ilioripotiwa kwa siku nchini China.

Idadi hiyo inayotokana na maambukizi ya virusi hivyo inafikisha watu 908 waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo tangu ulipoanza miezi mitatu iliyopita,

Shirika la habari la AFP ilisema kuwa kwa sasa viwango vya maambukizi mapya vimepungua.

Kwa mujibu wa AFP, zaidi ya watu 40,171 wameambukizwa ugonjwa huo huku wengine 187,518 wakiwekwa katika maeneo maalum ili kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.

Pia wagonjwa 3,281 walioambukizwa virusi hivyo wamefikishwa katika hospitali mbalimbali na baada ya matiababu waliruhusiwa kurudi nyumbani.

Jumatatu iliyopita, mamilioni ya watu walirudi kazini baada ya kusherehekea mwaka mpya wa Kichina ambao uliongezwa muda ili kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo.

Tume ya Afya nchini China ilisema kuwa mamlaka za afya nchini huo zinaendelea kuchukua hatua za tahadhari ikiwamo kupunguza muda wa kufanya kazi mbali na kuchagua maeneo ambayo kampuni zinafaa kuendelea na kazi.

Virusi hivyo pia vimesambaa katika mataifa 27 duniani na kusababisha vifo viwili pekee pekee nje ya China ambako ndiyo chimbuko la ugonjwa huo.