Wanaume wanne wanyongwa India kwa kumbaka msichana

Muktasari:

Wanaume wanne raia wa India, Akshay Thakur, Vinay Sharma, Pawan Gupta na Mukesh Singh wamenyongwa hadi kufa baada ya kumbaka na kumuua mwanafunzi mjini Delhi mwaka 2012.

New Delhi. Wanaume wanne raia wa India waliotekeleza shambulizi, kumbaka na kumuua mwanafunzi mjini Delhi mwaka 2012 wamenyongwa.

Wanaume hao, Akshay Thakur, Vinay Sharma, Pawan Gupta na Mukesh Singh walihukumiwa kifo na Mahakama mwaka 2013 lakini adhabu hiyo imetekelezwa leo Machi 20.

Wanne hao wamenyongwa katika gereza kuu la Tihar ikiwa ni mara ya kwanza hukumu ya kifo kutekelezwa India tangu mwaka 2015.

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, msichana aliyebakwa alifariki kutokana na majeraha aliyopata siku kadhaa baada ya kubakwa na wanaume sita ndani ya basi.

Kisa hicho kilizua ghadhabu ya umma ambayo ilichangia kubuniwa kwa sheria mpya dhidi ya ubakaji nchini India.

Mwanafunzi huyo aliyekuwa na umri wa miaka 23, aliyepewa jina la Nirbhaya na vyombo vya habari kuashiria “mjasiri”, hakuweza kutajwa jina lake halisi kutokana na sheria za India kutoruhusu.

Baada ya tukio hilo la ubakaji, watu sita walikamatwa kwa kumshambulia msichana huyo. Mmoja wao, Ram Singh alikutwa amekufa ndani ya gereza Machi 2013 kwa kile kinachoaminika kuwa alijiua mwenyewe.

Mtuhumiwa mwingine ambaye alikuwa na miaka 17 wakati wa shambulio hilo, aliachiliwa huru mwaka 2015 baada ya kufungwa kwa miaka mitatu katika kituo cha kurekebisha tabia. Kifungo hicho ni cha juu kwa watoto chini ya miaka 18.

Miezi ya hivi karibuni, wafungwa wote wanne waliwasilisha ombi katika Mahakama ya Juu zaidi nchini humo kutaka hukumu yao ibadilishwe kutoka kifo hadi kifungo cha maisha gerezani.

Hata hivyo, ombi lao lilikataliwa na kuwaacha bila njia nyingine ya kisheria ya kujinasua. Rufaa ya mwisho ya kutaka hukumu ya kifo isitekelezwe dhidi yao pia ilikataliwa saa kadhaa kabla ya wote wanne kunyongwa.

Dakika kadhaa baada ya wafungwa hao kunyongwa leo asubuhi, mama wa msichana aliyeuawa alisema, “nilitundika picha ya binti yangu ukutani na kumwambia hatimaye tumepata haki.” Naye baba wa msichana huyo, alisema “mahakama imerejesha hadhi yake.”

Usalama uliimarishwa nje ya gereza walikonyongewa wabakaji hao huku maofisa wa polisi wakipelewa kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo.

Kundi la watu waliokuwa wamekusanyika nje ya lango la gereza hilo wakiwa wamebeba mabango walianza kusherehekea baada ya tangazo la kunyongwa kwa wafungwa hao wanne kutolewa.