Waziri mkuu Sanchez ashinda uchaguzi Hispania

Chama cha Kisoshalisti cha Waziri mkuu, Pedro Sanchez kimeshinda katika uchaguzi mkuu wa kitaifa wa Hispania jana.

Katika uchaguzi huo wa pili katika muda wa chini ya miezi saba, chama hicho cha kinachoegemea siasa za mrengo wa kushoto kimeendelea kupata wingi wa viti katika Bunge la Kitaifa.

Huku asilimia 99.9 za kura zikiwa zimehesabiwa, chama hicho kilijinyakulia viti 120, hii ikiwa ni idadi iliyopungua viti vitatu kutoka uchaguzi uliopita wa mwezi Aprili lakini pia vikiwa pungu ya kiwango cha viti 176 vinavyohitajika ili kiweze kuunda serikali peke yake.

Uchaguzi huo umerudiwa ili kujaribu kumaliza mkwamo wa kisiasa nchini humo baada ya  Sanchez, licha ya kushinda katika uchaguzi wa Aprili, kushindwa kuunda Serikali.

    

Takriban wapiga kura milioni 37 walipiga kura Jumapili kuchagua Nunge jipya wakiwa na matarajio kwamba chama cha Sanchez kingeshinda, lakini pia kwamba asingepata wingi wa kutosha bungeni kumwezesha kuunda serikali.

Kwa miezi kadhaa, Sanchez alijaribu kuunda serikali ya muungano baada ya uchaguzi wa Aprili, lakini hakufaulu. Hali iliyomlazimu Mfalme Felipe VI kuitisha uchaguzi mpya.

Uchaguzi uliitishwa kwa sababu Sanchez alishindwa kuunda serikali ya muungano pamoja na vyama vingine kama Unidas Podemos au Ciudadanos.

Ikiwa mkwamo utaendelea, huenda chama cha People's Party (PP) kikajaribu kuunda serikali ya muungano pamoja na vyama vya Ciudadanos pamoja na Vox.

Hii ni mara ya nne Hispania inapiga kura ndani ya miaka minne, hali ambayo imewachosha wananchi na kusababisha idadi ya wapiga kura wanaojitokeza kupungua.