Abdul Wakil, Maalim Seif walivyopambana vikali urais Zanzibar ndani ya CCM 1985

Oktoba 9, 1985, mwenyekiti wa CCM, Mwalimu Julius Nyerere alihutubia mkutano wa hadhara mjini Chake Chake, Pemba, akianza kumpigia kampeni Ali Hassan Mwinyi aliyepitishwa na chama hicho kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano, ikiwa ni takriban mwaka mmoja baada ya kuongoza visiwa vya Zanzibar.

Mwalimu Nyerere alieleza mengi kuhusu mgombea huyo ili achaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na kuwataka Wazanzibari kusahau yaliyopita na kujenga Zanzibar mpya yenye kushikilia umoja na kujitokeza kupiga kura Oktoba 27, 1985.

Lakini akadokeza jambo lililovuta masikio ya wengi; alisema bado kuna watu waliokuwa na ndoto za kutaka kuigawa Zanzibar.

Alikuwa akidokeza kilichotokea katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa Zanzibar ndani ya CCM kati ya Idris Abdulwakil na Maalim Seif Sharif Hamad ulivyofanyika na matatizo yaliyojitokeza.

“Kati ya watu wa Makunduchi (Kusini mwa Zanzibar), waasisi wa (Afro Shiraz Party) ASP, Hizbu na (Zanzibar People’s Party) ZPP kabla ya Mapinduzi na kabla ya CCM, kuna wanaojaribu kuwagawa watu kwa kuwatenga kati ya Unguja na Pemba, Bara na Visiwani na kuna wanaojaribu kutumia dini ya Kiislamu na Kikristo,” alisema. “Mzanzibari ni Mzanzibari popote anapotoka. Kitu ambacho lazima tukipige vita ni kujaribu kutugawa.”

Aliwaambia mamia ya wananchi waliokuwa wakimsikiliza kuwa amepata habari kuwa baadhi ya Wapemba wangependa mgombea urais wa Zanzibar awe Seif Sharif Hamad (kwa wakati huo Maalim Seif alikuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar ambaye ni mzaliwa wa Pemba), badala ya Abdul Wakil ambaye alipitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM.

Abdulwakil alichaguliwa kuwa mgombea pekee wa Urais wa Zanzibar baada ya kupata kura 85 ikilinganishwa na kura 78 za Maalim Seif.

“Halmashauri Kuu ya Taifa ingemchagua Hamad, nina hakika kungekuwa na mgogoro Unguja,” alisema Mwalimu Nyerere.

Hata hivyo, alisema Abdulwakil alichaguliwa na chama kwa utaratibu halali wa kuchagua viongozi na kwamba, lazima uheshimiwe kwa kuwa wajumbe waliopiga kura hawakuangalia ni mzaliwa wa Pemba au Unguja.

“Abdulwakil ni wetu sote. Hata tukimchagua Seif angekuwa ni wetu sote pia,” Mwalimu alisema.

“Utaratibu mwingine wowote zaidi ya huo wa kupiga kura usingeweza kutumika, ama sivyo, labda ingebidi tuchague viongozi kwa kutumia mapanga.

“Mawazo ya baadhi ya wananchi wa Pemba ya kutaka mzaliwa wa Pemba ndiye awe Rais katika kipindi hiki kwa kuwa marais wote wa Zanzibar walikuwa ni wazaliwa wa Unguja, nilielezwa na sasa nimethibitisha. Nilipotamka katika Halmashauri Kuu ya Taifa iliyoyapigia kura majina mawili, Abdulwakil na Hamad, makofi mengi yalipigwa baada ya kutajwa jina la Hamad.

“Mkiwa na wawili, lazima achaguliwe mmoja. Hatuwezi kuwa na Rais wawili wa Zanzibar. Lazima tuheshimu uamuzi huo. Hata Rais wa Jamhuri ya Muungano anaweza kutoka upande wowote. Haimo katika Katiba kwamba mara hii atoke Zanzibar na mara nyingine atoke Bara.”

Katika mchuano huo mkali ndani ya CCM, Abdulwakil alimshinda Maalim Seif kwa kupata kura 85 dhidi ya 78 za mpinzani wake.

Siku mbili kabla, CCM ilikuwa imetoa taarifa ya kushukuru wananchi kwa kujiandikisha kupiga kura na kuwahamasisha wajitokeze kukamilisha mchakato.

Taarifa aliyoitoa katibu mkuu wa chama hicho kwa vyombo vya habari kutoka Dodoma ilisema, idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ilikuwa watu milioni 6.9.

Pia, alizungumzia uchaguzi wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Baraza la Wawakilishi ambao ulifanyika Oktoba 13. Kawawa alisema idadi ya waliojiandikisha kupiga kura visiwani ilikuwa watu 230,738 na kati ya hao, 133,662 walijiandikisha Unguja.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 84.1 ya watu wote waliotazamiwa kujiandikisha.

Alisema waliojiandikisha kutokea Pemba walikuwa 97,076 ambao ni sawa na asilimia 88.8 ya waliotazamiwa kujiandikisha.

“Chama kinawataka wale wote waliojiandikisha kwa uchaguzi wa rais wa Zanzibar na Baraza la Wawakilishi waende kupiga kura Oktoba 13, 1985 (siku sita baada ya kutoa taarifa hiyo) kwa kumpigia kura zote za ndiyo Idris Abdulwakil na pia wachague wajumbe wao wa Baraza la Wawakilishi,” alisema. “Aidha, tunataka kuona kwamba wale waliojiandikisha kwa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Bunge la Muungano wakienda kumpigia kura zote za ndiyo Ndugu Ali Hassan Mwinyi na pia wachague wabunge wao Oktoba 27, 1985.”

Alisema wagombea pekee wa urais wa Muungano na wa Zanzibar wameteuliwa na CCM na hivyo ni juu ya chama hicho kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanikiwa.

“Tunataka matawi yote ya sehemu za kazini, mitaani na vijijini yaanze kujiandaa kufanikisha kazi hii ... Chama kinataka utaratibu mzuri wenye demokrasia utengenezwe ili kuhakikisha kwamba wote waliojiandikisha kupiga kura wanakwenda kupiga kura siku ya uchaguzi,” alisema.

Kampeni za wagombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi zilianza rasmi Oktoba 7 na kukamilika Oktoba 12, siku moja kabla ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar na wajumbe wa Baraza.

Baada ya kumalizika kwa kampeni hizo, uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika Oktoba 13 kumchagua rais mpya na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, Iddi Pandu Hassan alisema uchaguzi ulikuwa “shwari”.

Katika uchaguzi huo mawaziri watano walishinda wakati waziri mmoja na naibu mmoja walibwagwa.

Abdulwakil alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi baada ya kupata kura 131,471 za ndiyo kati ya kura 214,309 zilizopigwa.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 58.61 ya ushindi.

Kura 75,220 zilimkataa ambazo ni sawa na asilimia 41.39 na kura 7,038 ziliharibika.

Kati ya watu 230,738 waliojiandikisha kupiga kura, 16,678 hawakupiga kura.

Matokeo hayo yalitangazwa na kaimu mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Abdallah Maisara Suleiman katika sherehe iliyofanyika makao makuu ya muda ya Abdulwakil, eneo la Kibweni, nje kidogo ya Zanzibar.

Abdallah Maisara Suleiman alitamka: “Kulingana na kifungu cha 34(2)(c)(i) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1984, kwa niaba ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, natamka rasmi kuwa ndugu Idris Abdulwakil amechaguliwa kwa kura halali kuwa Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.”

Chini ya kifungu hicho, ikiwa zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi zinakuwa zimemkubali mgombea urais, anatangazwa kuwa mshindi. Kabla ya uchaguzi huo, Abdulwakil alikuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Oktoba 17, 1985 aliapishwa kuwa Rais katika sherehe iliyofanyika kwenye viwanja vya Baraza la Wawakilishi mjini Zanzibar.

Aliapishwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Agustino Ramadhani, katika sherehe zilizohudhuriwa na Rais Nyerere, Katibu Mkuu wa CCM, Rashidi Kawawa, Jaji Mkuu wa Tanzania, Francis Nyalali na viongozi kadhaa wa CCM na Serikali.