Aliyefariki kwa corona Tanzania alivyopigania maisha yake

Dar es Salaam. Iddi Mbita, mfanyabiashara aliyekuwa akiuza vitakasa mikono vinavyotumika kukabiliana na virusi vya corona, amekuwa Mtanzania wa kwanza kufariki kwa ugonjwa unaosababishwa na virusi hivyo.

Iddi, ambaye jina lake halikuwekwa bayana katika taarifa iliyotolewa na Serikali kuhusu kifo chake jana asubuhi, alifariki akiwa Hospitali ya Mloganzila ambako alipelekwa baada ya kugundulika kuwa na maambukizi ya virusi hivyo.

Familia ya Iddi Mbita imeeleza kuwa mpendwa wao alijitahidi kupambana na ugonjwa huo wa homa kali ya mapafu, Covid-19, lakini mauti yalimkuta jana alfajiri.

“Ni bahati mbaya sana corona imechukua uhai wa Iddi wakati mwenyewe alikuwa anafanya biashara ya vitakasa mikono,” alieleza mmoja wa rafiki zake wa karibu, Simba Magani.

Magani, ambaye alisoma na Iddi Arusha alisema walikuwa na uhusiano tangu utotoni kwa kuwa mama yake alikuwa katibu muhtasi wa Brigedia Hashim Mbita.

Brigedia Mbita, ambaye alikuwa katibu mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), ni baba yake Iddi.

“Nilifahamu Iddi tangu utotoni ukizingatia familia zetu zilikuwa karibu sana. Alikuwa mtu wa watu sana na pia alikuwa na bidii ya kujishughulisha,” alisema Magani.

Magani alisema Iddi alijikuta katika masuala ya biashara na hivi karibuni alianza kufanya biashara ya kusambaza vitakasa mikono, ambavyo hivi sasa vimekuwa lulu kutokana na kutumika kujikinga na virusi vya corona.

Iddi anakuwa mgonjwa wa kwanza mwenye maambukizi ya virusi vya corona kufariki dunia tangu Serikali ilipotangaza kuwepo na maambukizi hayo Machi 16.

Hadi jana, Tanzania ilikuwa na watu 19 walioripotiwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitoa taarifa hiyo jana, akisema Mtanzania wa kwanza amefariki kwa ugonjwa huo bila ya kumtaja jina.

“Ninasikitika kutangaza kifo cha kwanza cha mgonjwa wa Covid-19 (ambukizo la virusi vya corona) kilichotokea alfajiri ya leo (jana) tarehe 31 Machi, 2020 katika kituo cha matibabu cha Covid-19 kilichopo Mloganzila, jijini Dar es Salaam,” inasema taarifa ya Waziri Ummy.

“Marehemu alikuwa mwanaume mwenye umri wa miaka 49, ambaye alikuwa akisumbuliwa na maradhi mengine. Tunaomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi na tunatoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu.”

Iddi, ambaye alikuwa mdau mkubwa wa soka na akiishabikia klabu ya Simba, alikuwa miongoni mwa watu 19 waliogundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo. Mgonjwa wa kwanza aliyepatikana mkoani Arusha, ameshapona.

Baada ya habari kuanza kusambaa mitandaoni, kaka wa marehemu, Ibrahim Mbita aliithibitishia Mwananchi jana kuwa aliyefariki kwa ugonjwa huo unaoshambulia mapafu ni kaka yake wa damu ambaye alikuwa anafanya biashara.

Iddi, ambaye alikuwa anaishi maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam, alifariki jana saa 9:00 usiku akiwa kituo cha Mloganzila alikokuwa anatibiwa ugonjwa wa corona.

Alizikwa jana kwenye maziko yaliyosimamiwa na Serikali na kuhudhuriwa na wanafamilia wachache.

Ibrahim alisema kwa muda mrefu kaka yake alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya mafua na shinikizo la damu.

“Wiki moja iliyopita alishikwa na mafua makali, ingawa hii ilikuwa inamtokea mara nyingi. Baada ya kushikwa na mafua yale alikwenda hospitali moja huko Masaki, jijini Dar es Salaam,” alisema Ibrahim.

Ibrahim alisema, hata hivyo, siku tano zilizopita ndugu yake alizidiwa na ikabidi aende Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.

“Akiwa hospitalini Aga Khan, alifanyiwa vipimo kikiwamo kile cha ugonjwa wa Covid-19,” alisema Ibrahim.

Ibrahim alisema kuwa majibu ya ndugu yake yalitolewa juzi na yalionyesha alikuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Alisema baada ya majibu kutolewa, alichukuliwa na watu wa Wizara ya Afya na kupelekwa Mloganzila ambako alifariki dunia jana alfajiri.

Ulipoulizwa kuhusu suala la matibabu ya ugonjwa huyo, uongozi wa Hospitali ya Aga Khan ulikataa kuzungumzia jambo hilo.

Badala yake, Olayce Lotha, ambaye ni meneja masoko na mawasiliano wa hospitali hiyo, aliiambia Mwananchi kuwa masuala yote kuhusu ugonjwa huo yanazungumzwa na Serikali.

Marehemu ameacha mke na watoto wawili, ambao nao pia walikuwa wanatarajiwa kuwekwa chini ya karantini.

Iddi na Ibrahim wanatoka familia ya watoto sita ya Brigedia Mbita.

Iddi alikuwa mtoto wa mwisho akifuatana na Ibrahim katika familia hiyo.

Brigedia Mbita alikuwa katibu wa tatu wa kamati hiyo ya ukombozi ya OAU baada ya Watanzania wengine wawili; George Magombe na Sebastian Chale.

Aliongoza kamati hiyo kwa miaka 22 kuanzia mwaka 1972 hadi 1994 na pia aliwahi kuwa katibu mtendaji wa Tanu, mwandishi wa Rais na balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.

Idadi ya wagonjwa

Kifo cha Iddi kimetokea siku moja baada ya Waziri Ummy kutangaza ongezeko la wagonjwa wa corona nchini.

Waziri Ummy alitoa taarifa ya ongezeko la wagonjwa watano, watatu wakiwa wa Tanzania Bara na huku wawili wakiwa wamepatikana Zanzibar.

Ongezeko hilo la wagonjwa watano lilifanya idadi ya Watanzania waliopata ugonjwa huo kufikia 19.

Aliwaelezea wagonjwa wapya wa Tanzania Bara kuwa ni mwanaume mwenye umri wa miaka 29, ambaye alikutana na raia wa kigeni kutoka miongoni mwa nchi zilizoathirika na ugonjwa huo.

Mtu wa pili alikuwa mwanamke mwenye umri wa miaka 21, ambaye ni miongoni mwa watu waliokuwa wanafuatiliwa.

Mgonjwa wa tatu aliyeelezewa na Waziri wa Ummy ni mwanaume mwenye umri wa miaka 49, ambaye pia inadaiwa ni miongoni mwa watu waliokuwa wanafuatiliwa.

Iddi, ambaye alifariki jana, haikubainishwa wazi kama naye alikuwa anafuatiliwa.

Kuhusu maisha yake Magani, ambaye pia ni mpenzi wa soka akiishabikia Yanga, alimwelezea Iddi kama mpenzi mkubwa wa soka, ambapo alikuwa akiipenda Simba na alikuwa mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo.

Naye Abdul Gugu, ambao familia zao zilikuwa majirani maeneo ya Chang’ombe jijini Dar es Salaam, alieleza kuwa Iddi alikuwa mtu mpole na sio muongeaji.

“Ukimwona mara ya kwanza unaweza kufikiri pengine Iddi ana maringo, lakini kama anakufahamu ilikuwa si jambo rahisi kukupita bila ya kukusalimia,” alisema Gugu.

Gugu alisema Iddi alikuwa anapenda sana soka, akiishabikia Simba nyumbani na kwa Ligi Kuu England alikuwa anaipenda Manchester United.

“Kwa kuongezea Iddi alikuwa anaifuatilia sana Taifa Stars na mara kadhaa alisafiri kwenda nje ya nchi pale ilipokuwa inakabiliwa na mechi za kimataifa,” alisema.

“Mfano alikwenda Ivory Coast fainali za CHAN (michuano ya mataifa ya Afrika inayoshirikisha wanasoka wa ligi za ndani).”