Bashiru awataja tena Makonda, Chalamila kuhusu uongozi

Dar es Salaam. Kama kuna majina ambayo katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally anayarudiarudia, basi ya Paul Makonda na Albert Chalamila hayawezi kukosa kwenye orodha hiyo.

Na takriban mara tatu alipoyataja hadharani, aliyahusisha na mafunzo maalum ya uongozi kwa ajili ya kuwafanya wawe bora.

Juzi, mwanazuoni huyo wa zamani alimtaja tena Makonda, ambaye ni mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, na Chalamila (mkuu wa Mkoa wa Mbeya) kuwa watakuwa wanafunzi wa kwanza watakaonufaika na darasa la mafunzo ya uongozi chini ya mpango mpya wa CCM.

Bashiru alisema hilo katika siku yake ya pili ya ziara wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam akisema wana vipaji vya uongozi na kwamba ameshawaorodhesha kuwa wanufaika wa kwanza wa mpango huo unaotokana na maelekezo ya mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli.

Dk Bashiru alisema malengo ya mpango huo ni kuhakikisha vijana wa kizazi cha sasa wanabeba deni la ukombozi wa Afrika dhidi ya wakoloni waliorejea kwa majina mengine.

“Mwenyekiti ameshaelekeza mpango wa kuwaandaa viongozi utekelezwe haraka na walengwa wakubwa ni vijana. Kati ya watakaoanza mafunzo hayo na nimeshawaorodhesha ni Makonda na Chalamila,” alisema Dk Bashiru.

“Tena wa Mbeya ni mwanafunzi wangu wa darasani kabisa. Tunataka kuandaa akina Baba wa Taifa, Julius) Nyerere wa leo na kesho, akina (muasisi wa Zanzibar, Abeid) Karume akina (Waziri Mkuu wa zamani, Rashid) Kawawa, rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson) Mandela na (rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert) Mugabe.

“Tusipofanya hivyo wakoloni watarudi. Na hawajaondoka, bado wako hapa wanajigeuza majina kwa hiyo vijana katika uongozi wangu mnivumilie.

“Nitakuwa mkali kwenu lakini kwa nia njema. Mna wajibu wa kuishi mapambano ya ukombozi wetu.”

Dk Bashiru alisema hayo alipokuwa akiwapongeza vijana wa chama hicho kwa ukakamavu na utayari wao huku akiwataka kutolegeza kamba kwa kuwa wana deni baada ya kuondoka kizazi cha waasisi waliopigania uhuru wa kisiasa Tanzania na barani Afrika.

Dk Bashiru aliwataka vijana wa chama hicho wasikasirike wanapokosolewa na kumpongeza Makonda kwa kile alichosema ni uvumilivu na uwezo wake wa kushughulikia changamoto za wananchi.

Hii si mara ya kwanza kuwazungumzia wawili hao. Akiwa katika ibada ya mazishi ya mwenyekiti wa IPP, Mei 9 mkoani Kilimanjaro, Dk Bashiru alimuombea msamaha Makonda kwa kutoa maneno ambayo yalionekana kukera kabila la Wachaga wakati wa kuaga mwili wa mfanyabiashara huyo jijini Dar es Salaam.

Dk Bashiru alisema kitendo hicho ni matokeo ya chama kutokuwa na mpango wa kuandaa viongozi.

Kwa habari zaidi pata nakala ya Gazeti la Mwananchi Agosti 30,2019