VIDEO: CCM kufyeka vimbelembele wanaonyemelea ubunge, udiwani tutawafyeka’

Dodoma. Makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula amesema wanachama walioanza kupita mapema katika majimbo na kata kutaka kuwang’oa wabunge na madiwani wa maeneo hayo watafyekwa.

Wakati akisema hayo, viongozi wa jumuiya za chama hicho wamesema watamuunga mkono mwenyekiti wao, John Magufuli katika kuwania urais kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Mangula alitoa kauli hiyo jana katika kongamano la miaka 43 ya kuzaliwa kwa CCM jijini Dodoma.

Alisema wana taarifa kuwa baadhi ya watu wanapitapita majimboni na kwenye kata mbalimbali kufanya kampeni kabla ya muda, jambo linalosababisha waliopo sasa kukosa nafasi ya kuwatumikia watu wao.

Alisema CCM haitamvumilia mtu yeyote na haitajali ukubwa wala nafasi yake iwapo atafanya kosa hilo kabla ya Bunge au mabaraza ya madiwani kuvunjwa.

“Kuna vimbelembele wanaopita huko kabla ya muda, hao hatutakuwa na huruma nao,” alisema Mangula.

Alisema uchaguzi wa mwaka huu utakuwa tofauti na chaguzi zilizopita kwa kuwa hawawezi kuruhusu kundi kubwa la wagombea kwenda katika kata kuomba kura kwa kuwa kufanya hivyo ni kuingiza rushwa na kujenga makundi.

Kwa mujibu wa Mangula, iko kamati maalumu inayoshughulikia maadili aliyosema ina wajumbe wanne, huku akimtaja Maalim Kombo Juma kuwa ni miongoni mwa wajumbe hao.

“Tuna kamati ya watu wanne tu ambao tunashughulika na watu hao, tena nitoe siri mmoja wapo ni huyu hapa (anamuonyesha Juma), hatuna huruma kama kuna uthibitisho kuwa ulifanya rafu lazima tukuondoe,” alisema.

Maalim Kombo Juma ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ambaye ni mlezi wa jumuiya zote tatu za chama hicho.

Kwa maelezo ya Mangula, kura za maoni ndani ya CCM zitakuwa na wagombea wasiozidi watatu na kutakuwa na mkutano mmoja ama wa kata au wilaya badala ya kuzunguka kwa wanachama.

Kuhusu CCM kushinda, alisema jambo hilo halina mjadala kwa kuwa chama hicho kimejizatiti kwa kuwa kina idadi kubwa ya wanachama ambao alisema wako milioni 17 wakati vyama vingine vina wanachama wasiofika hata milioni moja.

Hata hivyo, katika uchaguzi uliopita wa Rais, mgombea wa CCM alipata kura milioni 8.8 na wa muungano wa upinzani alipata kura milioni 6.07.

Kwa mujibu wa Mangula misingi ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere ndiyo inayowapa jeuri ya kushinda kwa kuwa chama kilipewa nafasi kubwa kuliko Serikali.

Alisema hakuna hofu wala shaka kwamba chama hicho kitaibuka na ushindi mnono katika uchaguzi mkuu wa 2020, lakini akasisitiza suala la amani akisema bila kuwepo kwa amani nchi haitatawalika na kwamba wanaoweza kuivuruga ni wanasiasa.

Makamu mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Zanzibar, Abdallah Haji Haider alisema CCM ilishamaliza uchaguzi hivyo kinachosubiriwa ni kuunda Serikali.

“Nasema sisi tulishamaliza uchaguzi siku nyingi, watake wasitake Zanzibar ni nchi ya mapinduzi lazima serikali zote zitakuwa za CCM,” alisema Haider.

Jumuiya zamuunga mkono

Viongozi wa jumuiya za chama hicho walitoa matamshi kuonyesha kuwa watamuunga mkono Rais Magufuli na ya wazazi ikitangaza kumchukulia fomu.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Dk Edmond Mndolwa alisema wameamua kumchukulia fomu mwenyekiti huyo wa chama hicho.

Hata hivyo, Dk Mndolwa amerudia ombi lake kuwa chama kitenge nafasi sawa za viti maalum vya ubunge ambayo hutolewa katika matokeo ya uchaguzi badala ya kuangalia jumuiya mbili tu.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake (UWT), Gaudensia Kabaka alisema uchaguzi wa mwaka huu kwa Rais Magufuli utakuwa ni mwepesi sana na kuwataka Watanzania kutulia.

Kabaka alitaja siri ya ushindi huo kuwa ni mambo mengi yaliyofanywa na Rais hasa katika kundi la kuwatetea wanyonge.