Corona, mkao mpya mjadala mkali bungeni

Wednesday April 1 2020

Mbunge wa jimbo la Musoma Mjini (CCM), Vedastus

Mbunge wa jimbo la Musoma Mjini (CCM), Vedastus Manyinyi akifuatilia Hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya Makadirio ya Mapato na matumizi kwa mwaka wa Fedha 2020/2021 bungeni jijini Dodoma leo katika ya moja ya kumbi zilizotengwa  eneo la bunge kutokana na kupunguza maambukizi ya virus vya corona. Picha na Anthony Siame 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mkutano wa 19 wa Bunge mahususi kwa ajili ya Bajeti jana ulianza kwa mkao mpya wa tahadhari na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, suala ambalo pia ndilo lilitawala katika kikao cha kwanza jana.

Hoja nyingi za wabunge kuhusu ugonjwa wa Covid-19 ziliibuliwa na wabunge baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kueleza utaratibu utakaotumika kuendesha mkutano huo ikiwa ni hatua ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Upimaji wa wabunge

Mapema subuhi nje ya geti kabla ya kuingia katika viwanja vya Bunge, wabunge na watu wengine walipimwa joto la mwili na kusafisha mikono kwa kutumia vitakasa mikono vilivyowekwa.

Wabunge waliiingia katika kumbi walizopangiwa ambapo katika ukumbi rasmi wa Bunge waliingia mawaziri, naibu mawaziri, wanadhimu wa kambi zote, Kamati ya Bunge ya Bajeti, wenyeviti wa kamati, mawaziri kivuli na naibu mawaziri vivuli.

Waandishi wa habari walielezwa kutojazana katika kumbi zilizotengwa kwa ajili yao kama ilivyokuwa katika mikutano mingine huku wasiopiga picha wakishauriwa kufuatilia televisheni katika kumbi mbalimbali ya Bunge.

Advertisement

Katika dawati la Spika kulifungwa ‘skrini’ ambayo ilimwezesha kuwaona wabunge wote walio katika kumbi zote zilizoandaliwa kwa ajili ya uendeshaji wa vikao.

Pia maswali na majibu yalitumwa kupitia ‘tablet’ za wabunge, huku wenye maswali ya msingi pekee wakiruhusiwa kuuliza maswali ya nyongeza, tofauti na utaratibu wa zamani uliokuwa unaruhusu mbunge yeyote kuuliza swali la nyongeza.

Wabunge wataka taarifa za serikali

Katika mchango wake, Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema ni vyema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na ikatoa taarifa bungeni ya kina ya hali ya corona nchini na hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Alisema ukaaji wa umbali baina ya mtu na mtu upo kwa watu wenye uwezo wa juu na watu wenye uwezo wa kati lakini sio huko mitaani, kwenye daladala wala kwenye mabasi ya mwendokasi.

Pia aliitaka wizara hiyo iseme ina mpango gani wa kibajeti kwasababu katika nchi nyingine dunia wakiamua watu kujitenga kwa kujifungia majumbani, Serikali inawafidia wafanyabiashara na vibarua.

“Sasa kama leo Serikali inaweza kutekeleza kwa asilimia 15 tu ya bajeti kwenye wizara muhimu kama ya afya, hivi corona tutaiweza kweli? Kwa hiyo tukija kuzungumza tunaweza kuishauri vizuri Serikali,” alisema.

Alishauri wabunge wapimwe ili kama kuna watakaoigundulika na virusi hivyo watengwe na kupatiwa matibabu wakati wengine wanaendelea na majukumu yao.

“Labda tungepimwa ili ijulikane kama Halima ana corona nipelekwe kwenye karantini ili wabaki watu wafanye kazi lakini wabunge leo wapo kwenye vyumba, kwanini tusianze na sisi tupimwe wote,” alisema.

Ombi kama hilo pia lilitolewa na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) Mchungaji Peter Msigwa akiitaka Serikali ipeleke bungeni mpango wa kukabiliana na athari za kiuchumi zinazosababishwa na virusi vya corona.

Alisema wasipokuwa waangalifu na ugonjwa huo kwa kuchukua hatua za kujikinga, unaweza kumdondosha mtu mmoja mmoja kati yao.

Msigwa alisema nchi haikuathirika kwa ugonjwa tu bali pia kwenye suala la uchumi na kwamba ni lazima Serikali ipeleke taarifa bungeni itakayoonyesha ina mipango gani ya kukabiliana na athari za kiuchumi.

“Mfano sekta ya utalii kuporomoka. Watalii hawapo, mapato hayapo Serikali ije na mpango kwa pamoja tujadiliane ni njia gani tutapita ili tujikwamue katika tatizo hili. Lakini tukienda kidogo kidogo hivi haiwezi kutusaidia,” alisema.

Akijibu hoja hizo, Spika Ndugai alisema leo Bunge litaanza na Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ndio mratibu wa suala hilo kwa hiyo itakuwa ni mahali sahihi kwa hoja zinazohusu wizara mtambuka.

“Pia kupitia kamati yetu ya huduma na maendeleo ya jamii na kamati nyingine, mnaweza kulipeleka moja kwa moja, mnaweza kulileta kwa Spika, mnaweza kulifikisha kwa waziri mkuu. Ningependa kutoa wito tufanye hivyo kadri inavyowezekana,” alisema.

Kuhusu, kuwapima wabunge alisema ni wazo zuri wanalichukua na kwamba watashauriana na Serikali wanaone inakuwaje na kwamba hata huko kwenye maabara kuu ya Taifa, sampuli zitakuwa nyingi kuliko wakati wowote ambao zinaongezeka.

Maoni kinzani

Akitoa maoni yake nje Bunge, Mbunge wa Konde (CUF) Khatibu Said Haji alisema ni bora vikao hivyo vingeahirishwa hadi hali itakapokuwa nzuri ili kuwapa nafasi wabunge kutoa michango yao katika bajeti hiyo.

Alikosoa utaratibu wa kuwagawa kimafungu kuwa utawafanya washindwe kuwasilisha hoja zao kutokana na baadhi kushindwa kutumia vizuri tablet walizopewa.

Suzan Kiwanga, mbunge wa Mlimba (Chadema) alisema utaratibu huo utawafanya wabunge washindwe kuuliza maswali ya nyongeza kutoka kwa wananchi.

Lakini, Martha Mlata (Viti Maalumu -CCM) alisema utaratibu huo ni mzuri kwa sababu ni lazima mkutano huo ufanyike ili kupanga bajeti, licha ya uwepo wa ugonjwa wa corona.

“Ushauri wa kupima ni mzuri lakini pia na madereva wetu wao wapimwe maana kama mbunge anao na dereva ataambukizwa,” alisema.

Mbunge wa Busega (CCM) Dk Raphael Chegeni alisema corona inaathiri uchumi wa nchi hivyo ni lazima Serikali ije na mkakati wa kukabiliana na jambo hilo.

Advertisement