VIDEO: Daraja la Kiyegea lawaacha watoto bila baba, mama

Wednesday March 25 2020

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Wazazi wa majeruhi Grace Baraka (2) na Yonusi Baraka (6) ni kati watu watano waliokufa katika ajali iliyotokea katika mchepuko wa Daraja la Kiyegea wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro.

Chanzo cha ajali hiyo iliyotokea Machi 22 ni lori lililokuwa limepakia shehena ya saruji kufeli breki wakati likiteremka kuelekea katika daraja hilo na kuyagonga magari mengine matatu, likiwemo gari aina ya Toyota Noah lililokuwa limepakia abiria zaidi ya 10.

Ajali hiyo ilitokea katika njia ya mchepuko ya daraja hilo kutokana na daraja kuu kusombwa na maji hivi karibuni.

Waliofariki dunia walikuwa katika Noah hiyo pamoja na wengine watano waliojeruhiwa na kulazwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea usiku wa Jumapili katika daraja hilo lililopo barabara ya Morogoro-Dodoma na kwamba Said Kifaila ambaye ni dereva wa lori hilo mali ya kampuni ya Road Steel Haulage lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, alikimbia.

Hata hivyo, Kamanda Mufafungwa katika mkutano huo hakutaja majina ya watu watatu waliofariki kwa kuwa walikuwa hawajatambulika na alipotafutwa jioni alisema apewe muda ili asome vyema taarifa yake.

Advertisement

Mganga mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Dk Ritha Lyamuya ndiye aliyethibitisha vifo vya wazazi hao na kuzungumzia hali za watoto hao.

Akizungumzia ajali hiyo ilivyotokea, Kamanda Mutafungwa alisema wakati lori likiteremka katika daraja hilo breki zilifeli.

“Gari zilizogongwa ni Brevis, Toyota Harrier na Noah iliyokuwa ikiendeshwa na Ramadhan Mohamed mkazi wa Dumila. Noah hiyo ilikuwa ikipandisha mwinuko wa daraja hilo,” alisema kamanda huyo.

Aliwataja waliofariki kuwa ni Mahungo Martine (25), Sijaona Chamene (29) na wengine watatu ambao majina yao hayajatambulika.

Alisema majeruhi ni Neema Braiton (27), Elimelek Msigula (28), Mkoa Michael (25), Eliwahad Mshana (28) na Mohamed.

Mbali na kumzungumzia dereva aliyekimbia, Kamanda Mutafungwa pia alitoa wito kwa madereva kuheshimu sheria za usalama barabarani hasa kwa madereva wa magari ya mizigo kuwa makini wakiwa wamebeba mizigo na wanapofika maeneo ya miteremko mikali na madaraja.

Kwa upande wake Dk Lyamuya alisema kati ya majeruhi watano waliowapokea, watatu wameruhusiwa. Aliwataja wanaoendelea kupatiwa matibabu kuwa ni watoto Grace Baraka (2) na Yonusi Baraka (6) aliyelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).

“Leo (jana) tunaangalia uwezekeno wa kumtoa Yonusi kwenye chumba cha wagonjwa wenye uangalizi maalum na kumhamishia katika wodi ya wagonjwa wa kawaida,” alisema Dk Lyamuya.

Alisema kwamba watoto hao ni ndugu na walikuwa wakisafiri na wazazi wao ambao walipoteza maisha katika ajali hiyo na majina yao hayajaweza kupatikana.

Advertisement