Diwani wa nne afariki kabla ya kuapishwa

Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM kwa upande wa Zanzibar, Catherine Peter.

Muktasari:

Diwani mteule wa kata ya Kinuni iliyopo Zanzibar, Suleiman Mohamed Hassan amefariki dunia juzi na kufanya idadi ya madiwani waliofariki dunia baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 kufikia wanne.

Dar es Salaam. Diwani mteule wa kata ya Kinuni iliyopo Zanzibar, Suleiman Mohamed Hassan amefariki dunia juzi na kufanya idadi ya madiwani waliofariki dunia baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 kufikia wanne.

Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM kwa upande wa Zanzibar, Catherine Peter Nao amesema diwani huyo alifariki ghafla baada ya kuanguka nyumbani kwake na kupelekwa katika Hospitali ya Altabib.

Hata hivyo, Hassan alifariki dunia muda mfupi baadaye akiwa katika hospitali hiyo.

“Sisi kama CCM tumepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba wa diwani Hassan na tunaiomba familia yake kuwa na moyo wa subira,” alisema Nao.

Wananchi wa kata hiyo wanaungana na wenzao katika tatu nyingine wanaosubiri Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi mdogo ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi na madiwani waliofariki baada ya uchaguzi.

Mbalia na hizo, zipo kata nyingine nane ambazo hazina madiwani kwa kuwa hazikufanya uchaguzi wa madiwani kwa sababu mbalimbali ikiwamo vifo vya wagombea watatu wa nafasi hiyo na kata moja ambayo uchaguzi uliahirishwa.

Madiwani waliofariki baada kushinda uchaguzi walikuwa wakisubiri kuapishwa kwenye mabaraza yao ya madiwani ambayo mengi hayajaanza vikao vyao rasmi.

Katika Mkoa wa Geita, CCM imepata pigo baada ya madiwani wake wawili wateule kupoteza maisha kwa nyakati tofauti.

Madiwani hao wanatoka katika jimbo la Geita na Chato na walipoteza maisha wakipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza.

Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Geita, David Azaria aliwataja madiwani kuwa ni Masalu Luponya ambaye alikuwa diwani mteule wa kata ya Bugalama, Geita na Magomamoto Zanzibar wa kata ya Buziku, Chato.

Azaria alisema Luponya aliugua wakati wa kampeni na hata siku ya uchaguzi alipigiwa kura akiwa Bugando.

Kuhusu Magomamoto, alisema aliugua ghafla baada ya uchaguzi na alipelekwa Bugando ambako alipoteza maisha.

Katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Geita, Jonathan Masele alisema kifo cha Luponya ni pigo kwa chama na kwa jamii inayokuzunguka.

Alisema Luponya alikuwa anasomesha wanafunzi 50 wa sekondari na 20 wa vyuo vya ualimu.

Katika mkoa wa Pwani, wiki hii kilitokea kifo cha diwani mteule wa kata ya Kikongo, Fatuma Ngozi pamoja na wajukuu zake wawili baada ya nyumba waliyokuwamo kuteketea kwa moto.

Mbali na vifo vya madiwani hao, taarifa ya Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage kabla ya uchaguzi, ilibainisha kwamba kata nne hazikupiga kura ya udiwani kwa sababu ya vifo vya wagombea katika kata tatu na kukosewa kwa karatasi za kura katika kata moja.

Alizitaja kata tatu ambazo wagombea wake walifariki kuwa ni Igambilo iliyopo manispaa ya Iringa, Kisingia (halmashauri ya Kilolo) na Nyahanga (halmashauri ya Kahama). Pia, aliitaja kata moja ya Kibosho Kati (halmashauri ya Moshi) ambayo karatasi za kura zilikosewa.

“Kwa mujibu wa Kifungu cha 51(1) cha Sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa, kikisomwa pamoja na kanuni ya uchaguzi wa serikali za mitaa (uchaguzi wa madiwani) za mwaka 2020, Tume itapanga tarehe nyingine ya uteuzi wa wagombea wa vyama ambavyo wagombea wake wamefariki,” alisema.