Dk Bashiru: Puuzeni kauli mbiu ya ‘kazi na bata’

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally

Kagera. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewaomba wananchi kupuuza kauli mbiu ya ‘kazi na bata’ inayosambazwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini kutokana na athari zinazoweza kujitokeza, akiwataka kuwekeza muda wao katika kufanya kazi.

Kauli mbiu hiyo ni wazo la kisiasa lililoibuliwa na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe Septemba 2, mwaka jana, akiwaeleza wafuasi na wanamabadiliko kwamba endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania kupitia uchaguzi mkuu ujao 2020, atahakikisha wananchi wanapata muda wa kufanya kazi na kustarehe.

Kauli hiyo iliyopokelewa kwa hisia hususani kundi la vijana mitandaoni, iliibua mjadala huku baadhi ya wachambuzi wa siasa na masuala ya uongozi wakitofautiana mitazamo kuhusu nadharia hiyo.

Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini kwa sasa alikuwa akitafuta ushawishi unaokinzana na sera ya Rais John Magufuli ambaye amekuwa akihubiri kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi tu tangu alipoingia Ikulu 2015.

Hata hivyo, akizungumza juzi na wananchi waliojitokeza kumsikiliza katika ukaguzi wa ujenzi wa ofisi ya CCM Kata ya Bwanjai wilayani Misenyi, Dk Bashiru alisema kauli hiyo inashawishi kuzalisha Taifa legelege kupitia kizazi cha wapenda starehe badala ya kazi, akitaka ikemewe.

Dk Bashiru alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotakiwa kujikomboa kiuchumi hivyo Watanzania wanatakiwa kupinga kauli mbiu inayoendeshwa na mtu mmoja anayetaka kubakia kwenye hali ya umaskini.

Alisema kauli hiyo ni usaliti kwa Watanzania katika vita ya kujikomboa kiuchumi.

“CCM kuna kauli mbalimbali za kuhimiza kazi zikiwemo, Hapa kazi tu, kazi na maendeleo, Uhuru na kazi, kazi ni utu, ila kuna baadhi ya vyama wao wanahubiri kazi kwa starehe, na huo ndio utofauti wa Chama kiongozi na vyama vya uchaguzi,” alisema Dk Bashiru.

Katika ufafanuzi wake, Dk Bashiru alitaja athari za kauli mbiu hiyo, akidai inadhalilisha wanawake na ambao wakati wote wamekuwa wakifanya kazi ya kusomesha watoto, kulisha familia zao, akisema kila mmoja ni matokeo ya juhudi za mama.

“Hizi ni kauli za kipumbavu za vyama vya uchaguzi, ambazo hatuna budi kuzidharau na kuzipuuza”.

Sera ya CCM

Akizungumzia mwelekeo wa miaka kumi wa Sera za CCM katika kipindi kijacho, Dk Bashiru alisema imejikita katika maendeleo ya viwanda ambayo yatakwenda kuchochea maendeleo ya vijiji na kuvifanya kuwa ni vitovu vya maendeleo kupitia msingi mkuu wa viwanda ni kilimo.

Aidha, alisema CCM kitaendelea kuwa chama cha kutetea haki za wanyonge kuboresha afya, elimu, miundombinu, maji na kuthamini utu wa watu wote.

Awali, akizungumzia ujenzi wa ofisi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Costancia Buhiye aliahidi ujenzi huo utakamilika licha ya ujenzi wake kusuasua kutokana na mwingiliano wa mchakato wa uchaguzi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali wakiongozwa na Mwenyekiti huyo chama wa mkoa aliyeongozana na Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Kanal Mstaafu Denis Mwila.