OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Idi Amin ahuzunika, aeleza masikitiko yake-12

Muktasari:

  • Toleo lililopita tuliona jinsi ‘fungate’ la Idi Amin na Israel la tangu kabla ya Januari 1971 lilipovunjika Aprili 1972 na Ubalozi wa Israel mjini Kampala kufungwa, na hivyo kuanza uhusiano mbaya uliokamilishwa na uvamizi wa Entebbe. Endelea…

Taarifa za kijasusi za Israel zilidokeza kuwa Urusi wangewapa Uganda ndege nyingine za kivita lakini wangetoa masharti makali. Katika ukurasa wa 902 wa kitabu, ‘Encyclopedia of the Developing World’ kilichohaririwa na Thomas M Leonard inadokezwa kuwa Urusi walikuwa wamewekeza kiasi cha dola bilioni 20 eneo hilo katika kipindi cha miaka michache iliyopita na sasa, kinasema kitabu hicho, Warusi “wanalazimika kuchagua kati ya viongozi wasio na msimamo kama Idi Amin au vikundi vya kigaidi ili kuhakikisha uwekezaji huo una usalama.”

Hili lilimtisha sana Idi Amin kiasi kwamba alijaribu kuzungumza na Bar-Lev ambaye taifa lake la Israel ndilo lililoivamia Entebbe na kuteketeza ndege za kijeshi za Uganda zilizotengenezwa Urusi. Uvamizi wa Entebbe ulipunguza sana kujiamini kwa vikundi vya Wapalestina.

Wakati Idi Amin akizungumza kwa simu na Bar-Lev, waliokuwa wameshikiliwa mateka mjini Entebbe walikuwa njiani kurudi nyumbani kwao Israel.

Kwa masikitiko Idi Amin alimwambia Bar-Lev hivi: “Sasa hivi nimewabeba askari wangu waliouawa kwa risasi za watu wako. Umenilipa baya kwa mema yote niliyokutendea.”

Kufikia wakati huu baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa vilikuwa vinatangaza habari za kuhusu “ndege tatu za miujiza zilizotua huko Entebbe na kuleta machafuko makubwa yaliyoleta vifo na uharibifu kabla ya kuondoka tena.”

Kutoka Tel Aviv, msemaji wa IDF alitoa kauli yake kwa muhtasari: “Mateka wameokolewa na Jeshi la Israel (IDF) kutoka Entebbe.”

Mara baada ya kauli hiyo, simu nyingi zilianza kupigwa makao makuu ya IDF nchini Israel kutoka sehemu mbalimbali duniani. Kila mmoja alitaka kupata maelezo kuhusu operesheni hiyo iliyoishtua dunia na kuwashangaza marafiki na maadui wa Israel kwa wakati mmoja.

Ingawa sehemu kubwa ya dunia ilikuwa imeshajua kilichotokea Entebbe usiku wa jana na jinsi kilivyotokea, kwa mujibu wa mwandishi Uri Dan wa gazeti la ‘Maariv’ la Israel, Idi Amin alikuwa hajajua mambo mengi yaliyotendeka nchini kwake saa kadhaa zilizopita.

Alipopigiwa simu kutoka Israel na mwandishi Uri Dan alipokea msaidizi wake, kisha msaidizi huyo akaiunganisha simu hiyo kwenda Uwanja wa Ndege wa Entebbe ambako Idi Amin alikwenda kutembelea uwanja huo kuona uharibifu uliosababishwa na makomandoo wa Israel.

Alipokuwa akizungumza kwa simu Amin alisema: “Ninazungumza nawe kutoka uwanja wa ndege (Entebbe). Ninahesabu miili ya askari waliouawa usiku wa kuamkia leo.”

Amin alimwambia Dan kuwa yeye (Amin) ndiye alikuwa akiwalinda mateka hao ili wasiuawe na magaidi na kwamba yeye hana hatia. Alikanusha kushirikiana na magaidi wa Palestina.

Akionekana kuzungumza kwa sauti ya huzuni, Idi Amin alimwambia Dan, “Leo nilikuwa nimepanga kuongeza jitihada zangu za kuachiwa kwa mateka raia wa Israel. Kwa sababu hii moja nilirudi mapema zaidi kutoka kwenye mkutano wa OAU (Nchi Huru za Afrika uliokuwa unafanyika) nchini Mauritius. Lakini kilichobaki kwetu ni athari tu.”

Alipoulizwa idadi ya askari wake waliouawa katika mapambano na makomandoo wa Israel uwanjani Entebbe, Idi Amin alikataa kujibu swali hilo. Baadaye Dan aliandika kuwa huenda Idi Amin hakujua kwa hakika kilichotokea. Alipoulizwa zaidi kuhusu habari za shambulio la Entebbe, Idi Amin alisema: “Ndege zenu za kivita za Hercules zilikuja, na wanajeshi wetu hawakutaka kuzirushia risasi wala makombora, vinginevyo tungezitungua.”

Mahojiano kati ya Idi Amin na Uri Dan yalidumu kwa angalau dakika 30 na yalikuwa hivi:

Dan: Kwanini wanajeshi wako walikuwa uwanjani? Hao mateka walikuwa ni wa kwako au ni wa Wapalestina?

Idi Amin: Mateka hawakuwa mikononi mwa Jeshi la Uganda. Walikuwa mikononi mwa Wapalestina. Kama wanajeshi wangu wangetaka kupigana, wangepigana. Hawakupigana, lakini waliuawa. Wanajeshi wangu walikuwa umbali wa yadi 200 kutoka kwenye jengo (walimoshikiliwa mateka), Wapalestina ndio walikuwa ndani ya jengo. Hilo waeleze watu wako utakaporudi Israel.

Dan: je, una nia ya kuja Israel kufafanua jambo hili, yaani jambo lililosababishwa na kilichotokea?

Idi Amin: Kwa nini nije? Sina sababu ya kuja huko. Hili jambo liko dhahiri kabisa. Nilikuwa mwema sana kwa mateka hao. Nitasaidiana na yeyote duniani kwa ajili ya kupata amani. Nasikitika sana mmeua watu wangu.

Dan: Kwa nini uliruhusu wateka nyara wakatumia ardhi yako kwa wiki nzima?

Idi Amin: Ni jana tu nilizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ... niliendelea na mazungumzo mengine ya kuwaweka huru ... Leo ndiyo siku wangeachiwa.

Kisha sauti ya Idi Amin ikakatika kidogo kana kwamba alikaribia kulia lakini baadaye akaendelea kuzungumza.

“Tuliwatunza sana mateka hao. Tuliwajali sana. Tuliwapa chakula. Tuliwapa mahitaji hata ya choo, na tuliwalinda ili angalau mbadilishane mateka. Lakini sasa nimebakiwa na nini? Badala ya kunishukuru kwa yote niliyofanya, mmeamua kuua watu wangu.”

Kwa sekunde chache aliegemeza kichwa chake katika mikono yake miwili kisha akakinyanyua na kusema: “Mungu atamsaidia kila mtu anayetaka kuleta amani. Mungu alipanga watu wangu wafe leo. Ni mbaya sana ... Hii ni mbaya sana ... Sana. Nakusanya maiti zao. Najua ni Mungu amependa iwe hivyo, na nitamsaidia yeye na mwingine yeyote kuleta amani. Sitaki kuwe na vita, kwa sababu wote ni watoto wa Mungu. Hata Mashariki ya Mbali pia sitaki kuwe na vita. Nataka nijenge amani kati yenu (Waisraeli) na Wapalestina.”

Uri Dan akamuuliza: “Kwanini basi unashirikiana na Wapalestina hata ukawaruhusu wengine wajifunze urubani wa ndege za kivita za Migs?”

Idi Amin: Sishirikiani na Wapalestina. Walioteka ndege hiyo hawakuwa Wapalestina pekee. Kulikuwa na Wajerumani, Wafaransa na wengine. Na si kweli kwamba Wapalestina ni sehemu ya marubani wa Uganda. Marubani wa Uganda ndio wanaorusha ndege za Uganda.

Dan: Kama hushirikiani na Wapalestina ilikuwaje hata wanajeshi wako wakauawa?

Idi Amin: Wanajeshi wangu walikuwako hapa uwanjani kulinda maisha ya Waisraeli. Niliokoa maisha yao. Na ukitaka waambie hivyo. Na wakitaka watakuambia hivyo. Na watakapokuwa wamefika nyumbani waambie nawatakia maisha ya furaha. Nilimwambia hata Kanali (Baruchi) Bar-Lev, ambaye muda mfupi uliopita niliongea naye kwa simu. Kama wanajeshi wangu wangezishambulia zile ndege, lazima wangewaua wanajeshi wenu. Lakini hatukutaka kupigana. Tunaweza kupigana tunapotaka kupigana. Lakini tulichotaka ni kumaliza tatizo lenu. Nasikitika … Nasikitika sana kwa kilichotokea. Mmefanya kitendo kibaya sana.

Dan: Mheshimiwa Rais, lakini unadhani ilikuwa ni muhimu kwako kuwapa usalama maharamia kwa wiki nzima katika nchi yako wakiwashikilia mateka wa nchi nyingine? Badala ya kuwafukuza nchini kwako? Kwa nini uliwaruhusu Wapalestina kuingia nchini kwako kufanya uharamia kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi yako?

Idi Amin: Hawakuingilia masuala ya ndani ya Uganda. Nilitaka tu kulinda watu wako. Lakini Wapalestina—na si Wapalestina tu, ni pamoja na Wazungu—Wajerumani na Wafaransa—walitega mabomu katika jengo, na wakatishia kulilipua. Niliwaweka kwenye jengo hilo kwa sababu nilitaka wapate mahitaji mazuri. Lakini si kweli kwamba nilishirikiana nao. Nilijaribu kuokoa maisha ya abiria (wa ndege iliyotekwa).

Dan: Je! Unakusudia kutangaza hali ya hatari?

Idi Amin: (Alinyamaza)

Dan: Je! Hauogopi kwamba, baada ya operesheni kama hii, na baada ya pigo kama hilo, unaweza kupoteza urais wa Uganda?

Idi Amin: (Baada ya kusita kidogo kujibu) Hapana, hapana! Kwa kweli sivyo! Wanajeshi wangu wako pamoja nami, na wananisaidia, na hakuna shida hata kidogo.

Dan: (Anarudia swali) Je, utatangaza hali ya hatari?

Idi Amin: Ndiyo.

Kwa hilo swali la kutangaza hali ya hatari au la, dakika chache baadaye alitafakari na kisha akajibu “Kwanini nitangaze?”

Itaendelea kesho