Jaji Warioba: Matamanio ya Katiba Mpya bado yapo

Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba akizungumza wakati wa mahojiano maalum ofisini kwake jijini Dar es Salaam kuhusu miaka 20 tangu kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Picha na Anthony Siame

Dar es Salaam. Joto la Katiba Mpya lililokuwa limetulia nchini, limeanza kufukuta na mara hii ni Jaji mstaafu Joseph Warioba, ambaye ameibua mada hiyo kwa kueleza anaamini kuwepo kwa matamanio ya wananchi juu ya kutimizwa jambo hilo.

Warioba aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba amesema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 na Sheria ya Kura ya Maoni zikitumika vizuri zinaweza kuuhitimisha mchakato huo.

Mchakato huo ulioanza mwaka 2013 kwa kukusanya maoni ya wananchi nchi nzima, uliishia kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa iliyokuwa ifanyike Aprili 30 mwaka 2015 lakini iliahirishwa kwa sababu ya kutokukamilika kwa uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji mstaafu Damian Lubuva aliyetangaza uamuzi huo Aprili 2, mwaka 2015 wa kutofanyika kwa kura hiyo hadi tarehe itakapotangazwa na Nec baada ya kushauriana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec).

Licha ya Serikali na CCM mara kadhaa kusema mchakato huo utafanyika wakati mwingine sasa juhudi zinaelekezwa kutatua matatizo ya wananchi huku wanaharakati, vyama vya siasa vya upinzani na wadau wengine wamekuwa wakishinikiza kukamilishwa kwa mchakato huo.

Wamekuwa wakidai mchakato huo uanzie kwa kuangalia Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba kutokana na Katiba Pendekezwa iliyopo sasa inayopaswa kupigiwa kura ya maoni imeyaacha maoni mengi ya wananchi waliyoyatoa mbele ya Tume ya Jaji Warioba ilipofika kuwahoji.

Jana, Jaji Warioba akihojiwa na kituo cha televisheni cha ITV alizungumzia masuala mbalimbali ya kikatiba ikiwamo jinsi nchi inavyoweza kuhitimisha mchakato huo wa Katiba na Bunge Maalum la Katiba lilivyoondoa maoni ya wananchi alioona yanafaa kuwamo.

“Lazima tutakamilisha mchakato wa katiba, mchakato huwa ni mrefu, ilichukua miaka 10 hadi 13 kupata katiba mpya baada ya muungano. Tumeanza mwaka 2013, mimi ninaamini kazi kubwa imeshafanyika ya kufikia Katiba Mpya,” alisema Jaji Warioba.

Katika kusisitiza hilo, Jaji Warioba alisema, “tunachozungumzia sasa, ni kwamba wananchi waliombwa kutoa maoni yao kwa mara ya kwanza, wametoa maoni yao, tunajua aina ya katiba wanayoitaka, mchakato umefikia mahali, matokeo yake ni Katiba mpya, mimi nazungumzia tumalizie ngwe hiyo.”

Mwanasheria mkuu huyo wa zamani alisema, “huwezi kuzuia kuwa na mabadiliko ya katiba, mawazo ya wananchi yamefanyika, rasimu ipo, katiba pendekezo ipo, nasema huwezi kuzuia mabadiliko ya katiba.”

Anachokisema Jaji Warioba aliyezaliwa Septemba 3, 1940, Bunda mkoani Mara kinafanana na kile kilichosemwa hivi karibuni na Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) kwamba litaanza midahalo ya kudai Katiba mpya.

Hata hivyo, Novemba mosi mwaka 2018, Rais John Magufuli akizungumza katika kongamano la uchumi na siasa lililofanyikia Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), alisema hawezi kutenga fedha kwa ajili ya mchakato wa Katiba licha ya kutambua kiu ya wananchi kupata Katiba Mpya.

Alisema kutenga fedha ni sawa na kuwapeleka watu kulipana posho, ni vizuri fedha hizo zikatumika katika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Alisema wanaotaka kusaidia kutoa fedha kwa ajili ya mchakato huo wazilete zikatumika katika miradi ya maji na barabara.

“Sasa sifahamu baada ya rasimu ya Jaji Joseph Warioba, miaka minne iliyopita tunaendelea na hiyo rasimu au tunakwenda kuanza upya. Badala ya kulumbana kwa hayo ya katiba bora tufanye kazi sasa,” alisema Magufuli.

Jaji Warioba akijibu moja ya swali aliloulizwa na mfuatiliaji wa kipindi hicho aliyetaka kujua tofauti kati ya Rasimu ya Katiba na Katiba Pendekezwa, alisema, “ipo kubwa tu, inayojulikana sana Rasimu ya katiba yenye muundo wa serikali tatu, inayopendekezwa serikali mbili.”

Alisema kuna mambo ya msingi kabisa yalipendekezwa na Tume lakini yakaondolewa, “kama tunu za taifa zinapaswa kuangaliwa vizuri, misingi ya uongozi na miiko ya uongozi. Tume ilikuwa imeweka masharti Bunge likaenda kubadili.

“Mawazo yangu kwamba lazima ifike wakati yale mambo tuliyozungumza ya tunu yaangaliwe vizuri na misingi ya uongozi na miiko ya uongozi kwamba unakuta viongozi si waadilifu, waaminifu na tunataka iwe katika katiba,” alisema Jaji Warioba.

Tunu hizo ambazo zilikuwemo kwenye rasimu ya katiba ni; utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na Lugha ya Kiswahili ambayo ni lugha rasmi ya Taifa.”

“Tunu za Taifa ndiyo mtima na fahari ya Taifa. Wananchi walitaka ibara hii iwepo hasa walipokuwa wakizungumzia kumomonyoka kwa maadili na kupungua kwa uzalendo. Umuhimu wa kujumuisha Tunu za Taifa ni kuwezesha ziote mizizi na ziweze kuenziwa na kurithishwa vizazi baada ya vizazi,” inaeleza sehemu ya rasimu hiyo.

Katika Bunge Maalum la Katiba, ilizichambua tunu hizo na kupendekeza ziwe; lugha ya Kiswahili; Muungano; utu na udugu; amani na utulivu.

Akijibu swali lililohusu Tume huru ya uchaguzi, Jaji Warioba alisema wananchi waliona tume hiyo siyo huru kutokana na watendaji wake jinsi wanavyopatikana kwa kuteuliwa na Rais ambaye ni kiongozi wa chama hivyo wakapendekeza utaratibu mwingine.

Alisema baada ya kusikiliza maoni hayo, Tume ilipendekeza nafasi za viongozi wa tume ziwe zinaombwa kisha Jaji Mkuu anaendesha jopo la watu watakaowadahili na majina yao kupelekwa kwa Rais na kuteua miongoni mwao kisha yapelekwe bungeni kuthibitishwa.

Katika mahojiano hayo, Jaji Warioba aliulizwa swali la mtazamo wake juu ya wale wanaozungumzia ukomo wa urais ambapo alisema wana maslahi yao binafsi.

Jaji Warioba alimnukuu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akieleza kuwa Mwalimu alikuwa anasema ni “vizuri ukang’atuka ukiwa bado una nguvu zako kimwili na kiakili uweze kusaidia kushauri, ukikaa muda mrefu sana huleti mabadiliko, unaanza kuongoza kwa mazoea, lakini mabadiliko huwa yanaletwa na mawazo mapya, na mawazo mapya huwa yanatoka kwa vijana.”