Kauli aliyotoa Bashiru juu ya dola kimantiki ni sahihi

Ni wiki kadhaa zimepita tangu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally atoe kauli iliyoeleweka ndivyo sivyo kwa watu wengi.

Mtu anaweza kuniuliza kwa nini nasema hivyo. Nikiri kuwa kauli yoyote ya kisiasa yenye vinasaba vya ubaguzi na uonevu ni dalili za kushindwa kuhimili siasa za ushindani zinazosimama katika dhana ya demokrasia.

Mwanasiasa makini anatambua mipaka ya kazi zake na pia, anahitaji kuchunga kauli zake mbele ya umma.

Kiongozi wa kisiasa mwenye dhamira ya kuchonganisha upande mmoja na mwingine, huyo ni dhaifu kifikra na hafai kuwa kiongozi.

Ifahamike kuwa kauli hasi ya kisiasa ni hatari kwa amani ya Taifa. Mathalani wapo wanasiasa wanaotoa kauli za kisiasa zenye muktadha uliojaa kiburi, majivuno na shibe ya hovyo.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyau wakati fulani aliwaambia Waisrael wanakula chakula sana kama mamba, kauli hiyo ilisababisha Waisrael wafanye maandamano makubwa, lakini Netanyau baada ya kubaini kuwa kafanya kosa, alitumia busara kumaliza kadhia kwa kujitokeza hadharani na kuomba msamaha.

Kwa mfano huo, hili ni fundisho juu ya ukakasi wa kutumia kauli na lugha mbovu za kisiasa na athari zake ndani ya jamii. Machi 6, Dk Bashiru alifanya mahojiano na moja ya chombo cha habari, alisema CCM kama chama chochote kinachoongoza serikali kitashindwa kutumia dola kubaki madarakani, itakua ni uzembe wake yenyewe.

Lakini alionya kinachotakiwa si kutumia dola kunyanyasa washindani wako. Kimantiki na kisiasa kwa mwanasiasa makini, kauli hiyo ina maana kubwa ndani yake na inafikirisha. Wapo watakaohoji tatizo lilianzia wapi? Ni pale kwenye dhana ya hofu na tafsiri hasi kutoka kwa makundi ya vyama vya upinzani na wanaharakati ambao kwa siku za hivi karibuni wamejenga dhana mpya ya “Kuonewa Kisiasa”.

Dhana hii ni batili na haina ukweli wa kitafiti ndani yake. Tukirejea kwenye kauli ya Bashiru, wapo wanaosema kiongozi huyo ajitokeze hadharani na kuomba radhi juu ya kauli hiyo.

Binafsi nasema hana haja ya kufanya hivyo, kwa sababu alichokisema ni sahihi.

Ifahamike kuwa kila nia na lengo la chama chochote cha siasa duniani ni kushika dola na ili ushike dola, sharti umma wa wananchi wakuamini na kukupa ridhaa ya kuwaongoza kwa kipindi fulani.

Na hapa nchini, ili upewe dola, lazima upitie mchakato wa kidemokrasia kwa maana ya kushiriki kwenye uchaguzi mkuu kama itakavyokuwa mwaka huu.

Ipo wazi kuwa kupitia jukwaa la demokrasia kila chama hunadi sera zake na kuitanganza ilani yake kuwa kama kitaaminiwa na kupewa dhamana na wananchi, kitaitumia dola kusimamia ilani ya chama kuwaletea maendeleo Watu wake.

Huu huu ni utamaduni ambao upo tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Leo hii ukikutana na Viongozi wa Chadema, ACT-Wazalendo, CUF, NNCR-Mageuzi na ukawauliza swali hili, kwanini mnashiriki kwenye uchaguzi mkuu, watajibu tunahitaji kushika dola.

Kushika dola iweje watajibu hili kutumia dola kuwatumikia Watanzania, kama hivyo ndivyo wapi alipokosea Dk Bashiru.

Cha msingi hapa ni kufuatilia kwa umakini utekelezaji wa kauli yake ya mwisho, kuwa chama kisitumie dola kunyanyasa wengine.

Ila kama kitaondolewa madarakani, ni uzembe wake wa kushindwa kutekeleza kile kilichomo katika Ilani yake kwa kutumia dola.