Breaking News

Kero tano za Muungano zafutwa

Sunday October 18 2020

 

By Kelvin Matandiko,Mwananchi

Dar es Salaam. Hati tano zilizosainiwa jana kwa ajili ya makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi, zimetoa sura mpya kwa pande mbili za Serikali ya Tanzania na Zanzibar.

Akizungumza katika hafla ya kusaini hati hizo zinazolenga kuondoa kero za Muungano, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema baadhi ya kero hizo zimeendelea kuwapo kutokana na uwajibikaji mdogo wa watendaji wa serikali zote mbili.

“Wakati mwingine tunazungumza, tunayamaliza, lakini watendaji wanasimama kabla ya mazungumzo na kabla ya kero kumalizwa kwa hiyo watu walikuwa wanalaumu Muungano lakini kumbe ni watendaji wetu kwa hiyo tunaposaini na kuzitoa hati hizi ni muhimu kusimamia katika ngazi ya utendaji,”alisema Samia na kuongeza:

“Tuwasaidie wananchi kwa ujumla kuelewa sababu za muundo huu wa muungano, uzuri wake na upungufu wake, lazima tueleze ni upungufu gani unatokana na muundo wenyewe na ni upungufu gani unatokana na utekelezaji tu... sasa haya ndio yanatukumba kwenye muungano. “

Ufumbuzi wa kero hizo tano unatokana na vikao vya kamati ya pamoja ya serikali zote mbili februari 9 mwaka jana chini ya Makamu wa Rais anayesimamia wizara inayohusika na masuala ya Muungano nchini.

Katibu Mkuu Kiongozi, balozi John Kijazi alisema kuibuka kwa hoja za Muungano ni jambo lisiloepukika kutokana na mahitaji ya wakati husika na ndio maana serikali imeamua kuongeza kasi ya utatuzi wake huku akidai kuwa sasa zimebaki hoja sita.

Advertisement

Kwa upande wake, Katibu mkuu kiongozi Zanzibar Dk Abdulhamid Yahya Mzee alisema ushirikiano bado ni muhimu hata kwa wizara zisizokuwa za Muungano kwa lengo la kushughulikia changamoto, akitoa rai ya kuendeleza kasi hiyo kwa kipindi kijacho.

Hoja tano

Katika tukio hilo, Naibu Katibu mkuu ofisi ya Makamu wa Rais balozi Joseph Sokoine alitaja hoja moja baada ya nyingine zilizosainiwa na mawaziri wa pande mbili zinazohusika na utekelezaji wa hati husika.

Alitaja ya kwanza ilihusu Serikali ya Zanzibar kutopewa nafasi katika ushirikishwaji wa masuala ya kimataifa na kikanda na kwamba Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki haikutoa nafasi ya kutosha kwa Zanzibar.

Ufumbuzi wa hilo alisema serikali zote mbili zimetayarisha mwongozo wa ushirikishwaji wa Serikali ya Zanzibar kwenye masuala ya kimataifa na kikanda uliozingatia maeneo ya ziara za viongozi wa kitaifa, mikutano ya kimataifa, nafasi za masomo ya elimu ya juu nje ya nchi na utafutaji wa fedha za misaada au mikopo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali kutoka nje ya nchi.

Balozi Sokoine alisema mwongozo huo ulipitiwa na kamati ya pamoja ya serikali zote Februari 9 mwaka jana na kisha kusambazwa kwa pande zote mbili Juni 21 mwaka jana.

Hoja ya pili iliyowasilishwa ni kuhusu nafasi ya Zanzibar kuwasilisha miradi ya maendeleo ya kiuchumi kwa ajili ya kujumuishwa kwenye miradi ya kikanda inayotekelezwa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema ufumbuzi uliopatikana ni kwamba Zanzibar iliwasilisha miradi nane kati ya hiyo ili ijumlishwe kwenye miradi ya jumuiya hiyo na minne ilipewa kipaumbele cha kuandaliwa maandiko ya miradi, usanifu, tathmini ya gharama kwa ajili ya kuombewa fedha za utekelezaji.

Hoja ya tatu iliyoshughulikiwa ni kushusha gharama ya mizigo inayoingia Tanzania Bara kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Balozi Sokoine alisema ufumbuzi ulipatikana kwa kuweka viwango vilivyopitishwa Aprili 2013 chini ya iliyokuwa Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (Sumatra).

“Viwango vinavyotozwa kwa mizigo inayotoka Zanzibar viko chini ikilinganishwa na mizigo inayotoka nchi nyingine kuingia Tanzania Bara au mizigo inayotoka nchi nyingine kupitia bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi nyingine,”alisema.

Nne ni hoja ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta ya gesi asilia. Hoja iliyokuwapo ni namna ya kugawana mapato ya rasilimali hiyo pindi itakapopatikana. Ufumbuzi ulipatikakwa kuihusisha kampuni ya OPEC ya Uingereza kama mshauri mwelekezi kuhusu mgawanyo utakavyokuwa.

“Mapendekezo yaliyopatikana yaliwasilishwa kwa serikali mbili, hata hivyo kuna hoja nyingine iliibuka kwamba suala la mafuta na gesi liondolewe kwenye mambo ya Muungano. Baada ya majadiliano pande zote mbili za Serikali zilikubaliana kuliondoa suala la utafiti na uchimbaji mafuta na gesi katika orodha ya mambo ya Muungano.

“Kwa hivyo sheria ya mafuta ya mwaka 2015 ilitungwa na kuipa Zanzibar mamlaka ya kuanzisha chombo au vyombo vya kusimamia masuala ya mafuta na gesi kwa kutumia sheria ya Zanzibar ya mwaka 2016,” alisema.

Hoja ya tano ni kuhusu utaratibu wa vikao vya kamati ya pamoja ya kushughulikia masuala ya Muungano na ufumbuzi uliopatikana ni kuanzishwa kwa utaratibu wa vikao vya kamati ya pamoja ya Zanzibar na Tanzania ya kushughulikia masuala ya Muungano, huku ikiagiza hoja hiyo iondolewe katika orodha ya hoja za Muungano.

Dhamira ya serikali

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema Serikali ya Rais John Magufuli ndani ya miaka mitano imefanikiwa kuonyesha dhamira kwa vitendo katika kuimarisha Muungano huo.

Alisema mafanikio hayo yamechochewa na utendaji kazi wa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan anayesimamia wizara inayoshughulika na masuala ya muungano na mazingira.

“Kufuta hati hizi ni kielelezo tosha kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano namna zilizojikita katika kutatua changamoto mbalimbali za Muungano kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,”alisema Majaliwa.

Aliongeza: “Mfano ni kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani na kufuta malimbikizo ya deni lililokuwa limefikia Sh22.9 bilioni kwa shirika la umeme Zanzibar (ZECO) kutokana na umeme iliyoouzwa na Shirikala Umeme Tanzania (Tanesco).Pili, Rais Magufuli alifuta sherehe za Muungano wakati wa Covid-19 na kuelekeza Sh500milioni za sherehe hizo ipatiwe Zanzibar.”

Akinukuu sehemu ya hotuba aliotoa Mwalimu Julius Nyerere Machi 6, 1997 jijini Accra Ghana, alisema ‘‘Umoja hautatupatia utajiri, lakini utatufanya Waafrika tusipuuzwe na kudharauliwa.’’

Alisema Muungano huo ndio chimbuko la umoja na mshikamano wa kitaifa uliopo.

Advertisement