Kigwangalla atia moto kauli za kujichukulia sheria mkononi

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangala (kushoto) akiangalia vipande vya meno ya tembo vilivyokatwa eneo la Chamazi, Dar es Salaam ambapo jumla ya vipande 339 na meno mazima 74  ya tembo pamoja na meno mawili ya kiboko yalikamatwa na kikosi kazi. Wa pili kushoto ni  Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda. Picha na Anthony Siame

Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla ametaka aendelee kunukuliwa kauli yake kwamba angekutana na mmoja wa majangili waliokamatwa Septemba 3, “angempiga risasi na kumuua”.

Kauli hiyo ni kama inazidisha mjadala kuhusu kauli za viongozi zinazoonekana kuwa tata ambazo pia zinaweza kuchochea vurugu.

Kwa kauli hiyo Kigwangalla imeingia kwenye orodha ya viongozi waliotoa kauli kama hiyo kwa nyakati tofauti baada ya mkuu wa wilaya ya Kigamboni, Ruth Msafiri kusema vibaka wavunjwe miguu huku mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila akisema mtu anayeingia nyumbani kwako kwa nguvu, amechagua kifo na hivyo huna budi kumuua.

Kigwangalla alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam wakati akieleza jinsi wizara yake kwa kushirikiana na vikosi mbalimbali vya kuzuia ujangili walivyokamata vipande 338 vya meno ya tembo yenye thamani ya Sh4.40 bilioni. Kwa mujibu wa Dk Kigwangalla Idadi ya vipande hivyo ni sawa na tembo 117.

Na jana, alipoulizwa na Mwananchi, alisema alichomaanisha ni sahihi na kusisitiza kuwa angekutana porini na jangili huyo aliyemtaja kwa jina la Haidary, angempiga risasi na kumuua.

“Bwana Haidary na wenzake wameenda kuwinda twiga pale Kisarawe, mtu ana jeuri ya kuwinda twiga, mnyama ambaye ni nembo ya Taifa katika zama hizi za (Rais John) Magufuli? Mtu wa aina hii akinikuta porini namuua na yeye hapo hapo. Si jambo la mzaha ni dharau kupindukia,” alisema.

Katika utawala wa sheria mtuhumiwa hutakiwa kufikishwa mahakamani ili aelezwe makosa yake na kujitetea na iwapo anapatikana na hatia, mahakama iamue adhabu anayostahili kulingana na kosa lake. Lakini Kigwangalla na viongozi hao wawili wameendelea kushikilia kauli zao.

“Jambo hili ni kinyume na utawala wa sheria ambao moja ya kanuni zake kuu ni uhuru wa mahakama,” alisema Anna Henga, mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC).

Alisema viongozi hao wanachochea watu kujichukulia sheria mikononi. “Ukisema mtu avunjwe miguu maana yake unaondoa mamlaka ya mahakama. Ni mahakama pekee ina uwezo wa kuhukumu,” alisema.

Mratibu wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu nchini (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa alitaka viongozi hao wakamatwe na kushtakiwa kwa uchochezi.

Alisema matamko ya viongozi hawa hayana tofauti na kinachoendelea Afrika Kusini, ambako baadhi ya watu wameingia mitaani na kuua wageni kwa madai kuwa wanachukua ajira zao.