Lema anyimwa dhamana, DC atoa maelezo ya vifo Manyoni

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa

Dodoma/Singida. Sakata la mauaji ya watu 14 katika wilaya ya Manyoni mkoani Singida limechukua sura mpya baada Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa kutoa maelezo ya mazingira ya vifo hivyo yanayotofautiana na ya madai ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Singida.

Lema, mwishoni mwa wiki alidai kuwa watu 14 waliuawa wilayani humo kwa kuchinjwa na mmoja kwa kuchomwa moto.

Alisema hayo wakati wa mazishi ya Katibu wa Chadema wa Jimbo la Manyoni Mashariki, Alex Jonas ambaye pia aliuawa kinyama.

Hata hivyo, jambo hilo limemwingiza matatani Lema, ambaye kwa sasa anashikiliwa na polisi wa Singida wakati ambao DC Mwagisa ametoa sababu tofauti zilizopelekea vifo hivyo.

Wakati Lema, alisoma orodha ya watu 14 waliofariki kwa kuuawa tangu mwaka jana, Mwagisa amedai watu 13 ndio wamefariki lakini kwa sababu tofauti na alizoeleza Lema.

Jeshi la Polisi Mkoani Singida limemnyima dhamana Lema kwa kile kilichodaiwa mamlaka za juu hazijatoa kibali.

Lema anatuhumiwa kusambaza taarifa za mauaji ya watu 14 wa wilaya ya Manyoni mkoani huko na kulilaumu jeshi hilo kwa kutochukua hatua.

Akizungumza na Mwananchi jana, wakili wa Lema, Hemed Nkulungu alisema mteja wake alihojiwa kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi 7:24 mchana katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa huo.

Alisema ingawa kosa la mteja wake linadhaminika lakini baada ya mahojiano hayo alirudishwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani humo.

“Kesho (leo) tutaendelea kupambana na kama atafikishwa mahakamani basi tutaomba impe dhamana mteja wetu kwa sababu kosa lake linadhaminika,” alisema.

Mapema jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike alisema Lema anashikiliwa kwa tuhuma za upotoshaji wenye lengo la kulichonganisha jeshi hilo na wananchi.

Lema alikamatwa juzi jioni mjini Arusha na kisha kusafirishwa hadi Singida.

Njewike alisema Lema akiwa Manyoni kuhudhuria mazishi ya kada wa chama chake, alitoa taarifa ya upotoshaji, kwamba Jeshi la Polisi halikuchukua hatua zozote dhidi ya matukio ya mauaji ya wakazi 14 wilaya ya Manyoni.

Alisema mauaji ya watu hao 14 yote yameyafanyiwa kazi na mengi yamesababishwa na wivu wa mapenzi.

“Moja kuna mama aliua mtoto wake wa miezi miwili baada ya baba wa mtoto huyo kutelekeza familia. Watuhumiwa wa mauaji hayo, karibu wote kesi zao zipo mahakamani. Wengine wapo mahabusu. Kasoro watuhumiwa wawili tu ambao bado tunaendelea kuwasaka,” alisema.

Njewike alisema Lema atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Maelezo ya mkuu wa wilaya

Akizungumza jana na Mwananchi, Mwagisa alisema Serikali imekuwa ikifanyia kazi tatizo la mauaji yanayotokea wilayani humo na kuwa baadhi ya kesi ziko mahakamani, nyinginewatuhumiwa bado wanatafutwa na kesi nyingine Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP) amezifuta.

Alisema si kweli kuwa watu hao waliuawa kwa kuchinjwa kama Lema alivyodai bali wengine walikufa kwa sababu mbalimbali za wivu wa mapenzi, kuchomwa moto au kuchomwa na vitu vyenye ncha kali.

“Unaposema kuwa wamechinjwa ina maana kuwa watu wametenganisha kichwa na kiwiliwili, jambo ambalo si kweli. Watu hawa walikufa kwa njia tofauti na Serikali imekuwa ikichukua hatua kwa kila tukio linalojitokeza,” alisema.

Akitoa mchanganuo wa vifo hivyo, Mwagisa alimtaja Sechelela Moses kama miongoni mwa watu waliokufa, kuwa aliuawa kwa wivu wa mapenzi wakati Abdalah Liyama alifariki katika ugomvi uliotokea baada ya kulewa pombe.

Mwagisa alisema kuwa Maritin Motekwa aliuawa kwa kuchomwa moto wakati Hamad Hussein alifariki baada ya kushambuliwa na watu wenye hasira kwa fimbo na mawe.

Alimtaja Mika Saimon kuwa aliuawa na mtoto wake katika ugomvi wa mali uliojitokeza na kwamba DPP aliondoa kesi hiyo mahakamani Februari mwaka huu ikiwa ni miongoni mwa kesi 87 zilizofutwa wilayani humo.

Kuhusu mauaji ya Emmanuel Meso, DC alisema kesi inaendelea mahakamani na chanzo cha mauaji hayo ni imani ya kishirikina ambapo Meso aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na kisha kuondolewa sehemu za siri.

Mwagisa alizungumzia pia mauaji ya John Logion, akifafanua kuwa kifo chake kilitokana na kwenda katika shamba la Antony Lipiti na kuiba mihogo.

Alisema bado mmliki wa shamba hilo anatafutwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.

“ Kuna Michael Charles huyo aliuawa katika ugomvi wa kifamilia na upelelezi bado unaendelea,” alieleza Mwagisa.

Alimtaja mtu mwingine aliyeuawa kuwa ni Issa Abdallah, ambaye alikutwa amekufa nyumbani kwa mama yake ambaye alikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Alisema kesi hiyo ilifutwa na DPP ikiwa ni kati ya mashauri 87 yaliyoondolewa Februari mwaka huu alipokuwa wilayani Manyoni.

Mwagisa alieleza Jumanne Thadei ni mtu mwingine aliyeuawa kwa wivu wa mapenzi baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Mkuu huyo wa wilaya pia alimzungumzia Andrew Leonard kuwa alikutwa na wananchi akiwa amekufa na kwamba kesi yake iko mahakamani huko Manyoni.

“Mtu mwingine aliyetajwa kwenye orodha ya Lema ni Rajabu Abbas, huyu alifariki katika hospitali ya St Gasper mkoani Singida baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali kutokana na wivu wa mapenzi.

“Hawa watu walifariki baada ya kifo cha Jonas (Katibu wa Chadema Manyoni Mashariki) aliyekutwa ameuawa kwa kitu cha ncha kali usiku wa kuamkia Februari 26 mwaka huu ambapo upelelezi unaendelea kuwabaini watuhumiwa,” alieleza mkuu huyo wa wilaya.

Hata hivyo, alifafanua kuwa Nyambelelo Njezo, ambaye anatajwa kuuawa bado yupo hai na ni mshtakiwa katika kesi ya mauaji na kwamba yuko gerezani.

Orodha hiyo ya mkuu wa Wilaya imeyataja majina yaleyale yaliyotajwa na Lema katika maziko ya kada wa chama ambaye pia aliuawa.

Katika msiba huo pia walitajwa baadhi ya makada ambao wa Chadema waliowahi ama kuuawa au kushambuliwa na kulilaumu Jeshi la Polisi kwa kutochukua hatua.