Maalim Seif, kamanda wa polisi wamjibu waziri mikutano ya hadhara

Mshauri mkuu wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu baada ya swala ya Ijumaa Tumbe mkoani Kaskazini kisiwani Pemba jana. Maalim Seif yuko katika ziara yake ya ukusanyaji maoni ya ilani ya chama hicho. Picha na Muhammed Khamis

Dar/mikoani. Wakati Maalim Seif Sharif Hamad akihoji sababu za Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kushangaa polisi kutozuia mikutano anayoifanya kisiwani Pemba, kamanda wa polisi wa eneo hilo amesema uchunguzi unaonyesha hakuna kosa lililofanyika.

Kamanda huyo wa Mkoa wa Kaskazini kisiwani Pemba, Sheikhan Mohamed Sheikhan amesema amewahoj viongozi wa ACT-Wazalendo na kuona walifanya mikutano yao bila ya kuvunja sheria.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo jana baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu agizo la Masauni alikotoa juzi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kumuondoa na kumshusha cheo Sheikhan na kamanda wa Mkoa wa Kusini pia kisiwani Pemba, Hassan Nassir Ally.

Naibu waziri huyo alitaka wachukuliwe hatua kwa sababu walishindwa kuzuia mikutano ya Maalim Seif pamoja na kutojengwa nyumba za polisi kisiwani Pemba licha ya Serikali kutoa maagizo.

Lakini Maalim Seif alihoji jana sababu za waziri huyo kutohoji mikutano ya katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally kisiwani Pemba.

Maalim Seif, aliyeanza kwa kukosoa amri ya Masauni kuhusu makamanda hao kwa maelezo kuwa inalenga kuwatia hofu polisi alisema kwanini Dk Bashiru alipotembelea Pemba na wafuasi wa CCM kufanya maandamano na mikutano ya hadhara hakuchukua hatua.

“Hakuna popote wafuasi wa ACT walipofanya mikutano ya hadhara au maandamano,” alisema

“CCM na (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) SMZ wametishika na uungwaji mkono wa ACT hapa Pemba ambako Dk Bashiru alidai kufunga mitambo ya ushindi. Inaonekana ziara yangu Pemba imetoa fuse katika mitambo ya Dk Bashiru.”

Maali Seif alisema kinachoendelea sasa ni wasiwasi uliopo CCM na SMZ kuhusu nguvu ya ACT-Wazalendo visiwani Zanzibar.

Mwananchi pia ilizungumza na msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime kuhusu agizo la Masauni.

“Jeshi la Polisi limepokea maelekezo ya Masauni kuhusu makamanda aliowataja na limeanza mara moja kuyafanyia kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu,” alisema.

‘Hakukuwepo uvunjifu wa sheria’

Naye kamanda wa polisi wa mkoa wa Kaskazini, Sheikhan alisema jeshi hilo halikuchukua hatua dhidi ya Maalim Seif wakati wa ziara zake kwa sababu hakukuwepo na uvunjifu wa sheria wala mikutano ya hadhara.

Alisema polisi walifika katika maeneo ambayo Maalim Seif alifanya mikutano yake na hakuna sehemu ambayo kulibainika kufanyika mikutano ya hadhara zaidi ya ile ya ndani.

Alisema wanachama wa ACT-Wazalendo walikuwa wameketi kwenye viwanja vya ofisi zao vilivyozungushiwa uzio maalumu kuonyesha ni mikutano ya ndani.

Kamanda Sheikhan aliwataka viongozi na wananchi wote kisiwani humo kuzingatia sheria na kanuni huku akionya kuwa jeshi hilo halitasita kumchukulia hatua za kisheria kiongozi na mwanasiasa yeyote atakayevunja sheria.

Viongozi ACT wahojiwa, waachiwa

Katika hatua nyingine, mwenyekiti wa ACT-Wazalendo wa mkoa wa Kaskazini, Rashid Khalid Salim aliiambia Mwananchi jana kuwa waliitwa na kuhojiwa polisi kuhusu ziara na mikutano ya Maalim Seif na kuachiwa baada ya kuwathibitishia polisi kuwa mikutano yao ilikuwa ya ndani.

‘’Wingi wa watu ndio unaowashtua na yote yamekuja kwa sababu ya watu na mapenzi yao kwa Maalim Seif. Hakuna jengine,” alisema Salim.

Katibu wa Kamati ya Sheria wa ACT-Wazalendo wa Wilaya ya Micheweni, Kombo Mwinyi aliiomba Serikali kutotumia nguvu nyingi kuuzima au kukabiliana na umma unaomuunga mkono Maalim Seif tangu alipohamia chama kipya akitokea CUF.

“Kinachosababisha wana ACT-Wazalendo kujazana hadi kukaa nje ni ufinyu wa ofisi zetu,” alisema Mwinyi.

Imeandikwa na Peter Saramba, Bakari Kiango na Mohammed Khamis