Magonjwa yaliyotangazwa janga la dunia

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa tahadhari kwamba lazima Dunia ijiandae kwa uwezekano wa virusi vya corona (covid 19) kuwa janga la Dunia.

Ingawa imesema kwa sasa ni mapema kuuita mlipuko wa virusi hivyo kuwa janga, lakini nchi zinapaswa kuwa katika maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Shirika hilo hutangaza ugonjwa kuwa janga pale maambukizi ya ugonjwa yanaposambaa kwa urahisi kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine na katika maeneo mengi ya dunia.

Mpaka sasa virusi hivyo vimeshaua watu zaidi ya 2,700 duniani kote na umeshasambaa katika nchi zaidi ya 30.

Mpaka sasa maambukizi mengi ya ugonjwa huo yapo nchini China ambako zaidi ya watu 77,000 wana maambukizi tangu ugundulike Desemba 31 mwaka jana katika mji wa Wuhan nchini China.

Virusi hivyo huenezwa kwa njia ya hewa na kusababisha joto la mwili kupanda pamoja na mafua na baadaye mgonjwa kufariki dunia.

Kinga ya ugonjwa huo inayoshauriwa mpaka sasa ni kufunika mdomo na pua kwa kitambaa safi, kufunika mdomo wakati wa kukohoa, kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka na kuepuka mikusanyiko.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema ugonjwa huo una uwezekano wa kuwa janga. Hata hivyo alisema kwa sasa kutumia neno ‘janga’ haifai kwa sababu inaweza kusababisha hofu.

‘’Ujumbe muhimu ambao unaweza kutoa matumaini kwa nchi, kutia moyo na kuzipa nguvu ni kwamba virusi hivi vinaweza kudhibitiwa, kusema ukweli kuna nchi nyingi ambazo zimefanya hilo,” alisema Ghebreyesus akikaririwa na BBC.

Wakati WHO ikitoa tahadhari hiyo, nchi za Korea Kusini, Italia na Iran zimepata ongezeko kubwa la maambukizi ya virusi hivyo na vifo, huku nchi nyingine za Mashariki ya Kati zikiripoti maambukizi ya kwanza.

Ugonjwa kutangazwa kuwa janga si jambo jipya, kwani WHO ilishawahi kutangaza magonjwa mbalimbali kuwa janga la dunia.

Mwaka 1981 ilitangaza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kuwa janga la dunia. Maambukizi ya virusi hivyo yaliripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Marekani ambapo mpaka sasa watu milioni 75 wameambukizwa, huku milioni 32 wakifariki dunia mpaka sasa.

Ikiwa imepita miaka zaidi ya miaka 30 tangu kugunduliwa kwa ugonjwa huo, mpaka sasa hakuna kinga wala tiba iliyogunduliwa.

Kwa sasa watu wenye maambukizi ya ugonjwa huo wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo (ARV’s) ambazo wanapaswa kutumia kwa maisha yao yote.

Wanasayansi wanaendelea na juhudi za kutafuta tiba ya ugonjwa huo na chanjo iliyogunduliwa hivi karibuni ambayo bado inafanyiwa utafiti imeonyesha matumaini.

Ugonjwa wa Kifua Kikuu nao ulitangazwa kuwa janga la dunia na maadhimisho yake hufanyika kila mwaka Machi 24.

Inakadiriwa kila mwaka zaidi ya watu milioni 10.4 huugua ugonjwa huo na wagonjwa milioni moja kati yao ni watoto wenye umri chini ya miaka 18. Ugonjwa huo umeshapatiwa tiba na kinga.

Shirika hilo lilitangaza ugonjwa wa Polio kuwa janga katika miaka 1980, baada ya kuathiri takriban watu 350,000 katika nchi 125 kila mwaka.

Ugonjwa huo unasababishwa na virusi vinavyoshambulia mishipa ya fahamu na hata kusababisha mtu kupooza na hata kufa.

Juhudi za kuangamiza ugonjwa huo zilianza mwaka 1988 na tangu wakati huo idadi ya maambukizi imengua kwa asilimia 99.

Pia WHO iliwahi kutangaza homa ya Ebola kuwa dharura ya kimataifa baada ya kuwapo kwa taarifa ya kuwepo mgonjwa wa Ebola katika mi wa Goma, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Zaidi ya watu 1,600 walifariki dunia katika mlipuko wa ugonjwa huo mwaka 2014.

Mlipuko mkubwa zaidi katika eneo la Magharibi mwa Afrika ulitokea kati ya mwaka 2014 na 2016 na uliwaathiri watu 28,616 hususan katika mataifa ya Guinea, Liberia na Sierra Leone.

Ebola ni ugonjwa unaoambukizwa na virusi ambapo aliyepata maambukizi hupata dalili za homa, uchovu, maumivu ya viungo na koo. Pia mgonjwa hutapika, kuharisha na kutoka damu.

Watu huambukizwa kwa njia ya kugusana, njia ya mdomo na pua, pia kwa njia ya damu, matapishi, kinyesi,majimaji ya kwenye mwili wa mtu mwenye Ebola

Wagonjwa hupoteza maisha kutokana na kupungukiwa na maji mwilini na viungo kushindwa kufanya kazi.

WHO ilisema kuwa hatua ya kutangaza ugonjwa kuwa janga inazisukuma nchi nyingi duniani kujiunga na juhudi za kukabiliana na maradhi hayo.

Mwaka 1918 mafua ya Hispania yaliyoua watu takriban milioni 50 duniani kote yalitangazwa kuwa janga la dunia.

Pia mafua ya Asia yaliyogunduliwa nchini Singapore mwaka 1957 yaliua watu milioni 1.1 ulimwenguni kote.

Mafua ya Hongkong yaliibuka mwaka 1968 na watu 500,000 waliambukizwa katika nchi hiyo pekee kabla ya kuenea katika bara la Asia na Ulaya.

Wakati huo wanajeshi wa Marekani waliotoka katika vita nchini Vietnam waliambukizwa virusi hivyo na kuvisambaza nyumbani na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.

Pia ugonjwa wa mafua ya ngurume mwaka 2009 ugonjwa huo uliua watu 200,000. Ugonjwa huo uligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Mexico.

Kuliwahi kuwapo kwa ugonjwa wa Ndui ambao ulisababisha vifo vingi duniani na walioathirika zaidi walikuwa watoto, lakini sasa umetokomezwa.

Katika karne ya 20 ilikadiriwa kuwa watu zaidi ya milioni 300 walikufa kutokana na ugonjwa huo, wale ambao waliugua na kupona wengi wao walibaki na makovu mabaya.

Mpango wa chanjo duniani kote ulioongozwa na WHO, ulifanyika ili kutokomeza ugonjwa huo na ilipofika mwaka 1970 matukio ya watu kuambukizwa ugonjwa huo yalikuwa machache.

Mwaka 1978 shirika hilo la afya lilitangaza kutokuwepo kwa ugonjwa huo tena duniani kote.

Akiuzungumzia ugonjwa huo Ghebreyesus alisema: “ndui ni ugonjwa pekee wa binadamu uliotokomezwa, ushahidi wa kile ambacho tunaweza kufanikiwa iwapo mataifa yatafanya kazi pamoja.

“Inapokuja magonjwa ya milipuko tuna wajibu wa pamoja na mustakabali wa pamoja. Kwa janga hili, tunakumbuka mashujaa duniani kote waliokutana na kupigana dhidi ya ndui na kufanya vizazi vijavyo kuwa salama,” alikaririwa na Shirika la Umoja wa Mataifa.