Magufuli asisitiza mara mbili hataongeza muda wa urais

Rais  John  Magufuli, akikagua eneo la mapokezi katika jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Chato lililopo eneo la Mlimani Chato mkoani Geita  baada ya kulifungua jana. Picha na Ikulu

Chato/Dar. Kwa wanaodhani kuwa Rais John Magufuli anatania katika suala la kutoongeza muda wa uongozi, huenda huu ni wakati sahihi kwao kuachana na dhana hiyo.

Kwa mara nyingine Rais Magufuli amerejea kauli yake ya kuondoka madarakani muda wake wa uongozi utakapokwisha, tena safari hii akitamka kauli hiyo mara mbili.

Rais Magufuli jana alikuwa wilayani Chato mkoani Geita katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa visima vya maji katika Shule ya Msingi Chato huku akieleza mambo yanayofanywa na Serikali na anavyopewa ushirikiano na wananchi na watendaji wake. “Sijabadilika naomba Mungu asinibadilishe, niendelee kumtegemea Mungu. Mimi ni Magufuli yuleyule niliyekuwa ninapita hapa nauza maziwa..., kazi hizi ni za kupita na maisha yetu ni ya kupita,” alisema.

“Kwa kuzingatia sheria na Katiba sitegemei kuongeza hata siku moja nikishamaliza muda wangu, narudia tena sitegemei kuongeza hata siku moja baada ya kumaliza muda wangu. Kwa sababu muda nitakaokuwa nimepewa kwa mujibu wa Katiba ndio nitakaokuwa nimepewa na Mungu kuwatumikia Watanzania,” alisema Rais Magufuli.

Huku akionekana kuwa makini alisema, “nimeona niliseme hili kwa uwazi kabisa ili wale wanaofikiria kuongezaongeza yale mawazo yawe yanawatoka. Watanzania milioni 55 kila mmoja anaweza kwa msaada wa Mwenyezi Mungu.”

“Hata mimi nimeyaweza haya kwa msaada wa Mungu, maendeleo tunayoyapata si nguvu zangu, ni za Mola wetu.”

Jana ni takribani mara ya nne, Rais Magufuli anasisitiza kutoongeza muda kipindi chake wa uongozi kikikamilika ambacho ni awamu mbili zenye miaka mitano mitano.

Tofauti na siku nyingine, jana Magufuli alirejea kauli hiyo mara mbili jambo lililoonyesha kuwa ameweka msisitizo zaidi.

Januari mwaka jana, alimuelekeza katibu wa itikadi na uenezi CCM, Humphrey Polepole kuwajulisha wana CCM na Watanzania kuwa anasikitishwa na hafurahishwi na mjadala uliokuwa unaendelea juu ya kuongezwa kipindi cha urais.

Aprili mwaka huu akizungumza na wananchi wilayani Newala mkoani Mtwara, Rais Magufuli alisema muda wake wa uongozi ukiisha ataondoka na yeye si Rais wa maisha.

Machi 23 akiwa jijini Dodoma, katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alimuonya mbunge wa Chemba, Juma Nkamia akimtaka aachane na kampeni ya kutaka muda wa urais kuongezwa akisema ndani ya chama hicho hakuna usultani.

Nkamia amekuwa akijitokeza kutaka muda wa urais uongezwe ili Rais Magufuli aongoze muda mrefu zaidi ya unaotambulika kikatiba wa miaka mitano katika kipindi kimoja au miaka 10 vipindi viwili.

Desemba 13, katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho jijini Mwanza, Polepole alitoa taarifa ikimnukuu Rais Magufuli akisema ataondoka madarakani muda wake wa uongozi utakapomalizika.

Rais Magufuli aliyeingia madarakani Novemba 5, 2015 kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano kitamalizika mwaka 2020 na cha pili 2025 iwapo atachaguliwa tena katika uchaguzi mkuu mwakani.

Rais Magufuli ambaye pia jana alizindua jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato alitoa mifano ya ujenzi wa daraja la Busisi, reli ya kisasa, ununuzi wa ndege 11 na utoaji wa elimu bure, kwamba si nguvu zake bali ni kwa uwezo wa Mungu.

Alisema ujenzi wa hospitali zaidi ya 352 kwa wakati mmoja wakati miaka ya nyuma ilishindikana si nguvu zake bali ni maombi ya Watanzania, akisisitiza mara kadhaa kuwa anamuamini Mungu na hana mkataba naye. “Mimi ni mtumishi wenu nitaendelea kuwa mtumishi wenu na nitaendelea kuwaeleza ukweli hadi mwisho wa kipindi changu...Tanzania ni tajiri dhahabu kila mahali, almasi, samaki wamejaa,” alisema.

Jengo la mahakama

Akizindua jengo hilo, Rais Magufuli aliwataka watumishi wa mahakama kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu na weledi huku akimtaka Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma kuendelea kuchukua hatua kwa watumishi wa mahakama wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.

Alisema mahakama ni chombo muhimu ambacho wananchi wanategemea kupata haki zao, kwamba wanapaswa kuwa waadilifu na weledi.

Pia, alipongeza juhudi za ujenzi wa mahakama hiyo na kumtaka Jaji Mkuu kuendeleza jitihada za kujenga na kuboresha miundombinu ya mahakama katika maeneo mbalimbali lakini akasema jitihada hizo hazitakuwa na tija kama kutakuwa na vitendo vya rushwa na kushindwa kutoa haki kwa wananchi wanyonge.

“Najua wakati mwingine huwa mambo yanacheleweshwa na watu wengine, unakuta kesi inatakiwa kupelekwa mahakamani haipelekwi, jeshi la polisi wanachelewesha, kwa hiyo vyombo vyote vya kutoa haki ni lazima mshirikiane kwa pamoja katika kuhakikisha haki za wananchi zinatendeka,” alisema Rais Magufuli.

“Mtu wa kawaida akiona atasema tunafungua Mahakama ya Chato pekee, lakini mahakama nyingi zimejengwa katika maeneo mbalimbali, mahakama nyingi zilikuwa kwenye hali mbaya lakini katika kipindi chako mmefanya kazi nzuri kuboresha miundombinu ya mahakama kote nchini,” alisema akimpongeza Jaji Mkuu.

Alisema wakati wa kusherehekea sikukuu ya Uhuru Desemba 9 mwaka huu ambapo alitoa msamaha kwa wafungwa alibainisha kuwa nusu ya watu waliopo magerezani ni mahabusu wanaosubiri kesi kusikilizwa.

“Kabla ya msamaha huo magereza yetu yalikuwa na watu 35, 803 ambapo wafungwa walikuwa 17, 547 na mahabusu walikuwa 18,256 kwa hiyo ukiangalia namba ya mahabusu ni kubwa hivyo mahakama hizo zitasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu wanaosubiri uendeshaji wa kesi zao,” alisema.

Kuhusu watumishi wa mahakama alisema katika kipindi cha miaka minne iliyopita Serikali imeteua majaji 11 wa mahakama ya rufaa na mahakama kuu 39 na kufikia idadi ya majaji 50.

Alisema pia Serikali imeajiri mahakimu 396 kuongeza idadi ya mahakimu kutoka 700 wa mwaka 2015 na kufikia 938 na kwamba idadi hiyo haitoshi.

Kwa upande wake Jaji Mkuu alisema jengo la mahakama hiyo litakuwa la kisasa kulingana na mahitaji ya huduma za karne ya 21 kwani litatumia Tehama iliyounganishwa na mkongo wa taifa wa mawasiliano.