Magufuli kusukuma sheria bima ya afya iwe kwa wote

Rais John Magufuli akionyesha tuzo aliyokabidhiwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) wakati wa maadhimisho ya siku ya madaktari nchini yaliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile. Na Mpigapicha Wetu

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kuboresha sheria ili kummlazimisha kila Mtanzania kuwa na bima ya afya.

Hilo lilikuwa moja ya mambo matatu aliyotangaza jana baada ya kuagiza wateule wake kuacha kuwaweka mahabusu watumishi wa Serikali kwa makosa ya kikazi na kueleza ndoto yake ya kutaka nchi iwe kituo cha utalii wa afya.

Katika taifa lenye zaidi ya watu milioni 50, ni asilimia 33 tu wanaonufaika na mpango wa bima ya afya, ambao huhusisha malipo ya awali kwa kampuni ya bima hiyo ambayo baadaye humtengea mlipaji kiwango cha fedha atakachotumia kwa mwaka ili atibiwe bila ya kulipia fedha taslimu.

Mnufaika hupewa kadi maalumu ambayo huitumia anapokwenda hospitalini kupata matibabu badala ya kubeba fedha taslimu.

“Tunajaribu kuangalia namna gani tunaweza kuboresha hiyo sheria ikiwezekana watu wote iwe compulsory (lazima) watu wote kuwa na bima ya afya,” alisema Magufuli katika mkutano ulioandaliwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).

“Lakini pia kuna changamoto katika mfuko (wa bima ya afya, NHIF)wenyewe na hili lazima nilizungumze.

“Fedha zinazokusanywa mle sina uhakika kama zinatumika vizuri, ndiyo maana unakuta bima ya afya lakini wanaenda kujenga majengo na majengo yanakuwa very expensive (ghali sana) badala ya kujenga viwanda. Lakini hili nataka kuwaambia tunalifanyia kazi.”

Rais alikuwa akijibu ushauri uliotolewa na Rais wa MAT, Dk Elisha Osati kabla ya kumkaribisha mgeni huyo rasmi azungumze.

Dk Osati alimwomba Rais Magufuli kufikiria kuweka sheria itakayomlazimisha kila Mtanzania akate bila ya afya ili aweze kupata matibabu, ambayo yamekuwa mzigo kwa watu wenye kipato cha chini.

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) hulazimika kutumia hadi Sh600 milioni kulipia wanaoshindwa kumudu gharama za matibabu.

Rais Magufuli alikutana na tatizo hilo alipotembelea Muhimbili kuwajulia hali watu waliojeruhiwa katika ajali ya moto mkoani Morogoro. Akiwa Muhimbili, mwanamke mmoja alimlilia akimsihi amsaidie kutoa maiti ya ndugu yake iliyozuiwa kwa kushindwa kulipia Sh5 milioni.

Hadi kufikia Desemba 2018, Mfuko wa Bima yaAfya (NHIF) ulikuwa na wachangiaji 899,654 na ulikuwa unahudumia wanufaika milioni 4.2, sawa na asilimia 8 ya idadi ya watu, wakati Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ulikuwa na wanufaika milioni 13.5.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ya Januari 29, 2019, mifuko yote miwili inahudumia wanufaika milioni 17.7, sawa na asilimia 33 ya idadi ya watu.

Ingawa kuna kampuni binafsi za bima zinazotoa huduma hizo, ni wananchi wachache wanaozitumia kupata huduma ya afya.

Ndoto ya utalii wa afya

Rais Magufuli pia alizungumzia ndoto yake ya kutaka kuigeuza Tanzania kuwa kituo cha utalii wa afya, kama ilivyo India.

“Tanzania ina madaktari wazuri, lakini walikuwa wanapunguziwa uwezo kwa sababu ya sisi Serikali kutonunua vifaa. Kukiwa hakuna vifaa hata ungekuwa mtaalamu utafanyaje?” alisema Rais.

“Nataka niwaahidi. Vifaa, madawa vitakuja na vitaendelea kuja.”

Alisema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa na utoaji wa vifaa vya kisasa ili Tanzania iwe kati ya nchi za Afrika zitazopokea wagonjwa kutoka nje.

Alisema Serikali lazima ifanye uwekezaji wa kutosha ili madaktari hao wafanye kazi yao kwa ufanisi huku wakifaidi elimu yao.

Alisema kutokana na kuimarisha huduma za afya, idadi ya wagonjwa waliokuwa wakisafirishwa kwenda nje ya nchi imepungua kutoka zaidi ya watu 200 mpaka chini ya 60 kwa mwaka.

Alisema pia wagonjwa wa nchi jirani wamekuwa wakija kupata matibabu kama ya maradhi ya moyo.

“Wagonjwa zaidi ya 200 saa nyingine mpaka 300 ukiachia wale waliokuwa wanasindikiza walikuwa wanapelekwa kule. Mtu anaugua mafua na anapelekwa kule kwa fedha za Watanzania,” alisema.

Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikiweka mkazo katika huduma ya afya. Mwaka 2018/19 Wizara ya Afya ilipangiwa Sh866.2 bilioni na kati ya hizo Sh561.8 bilioni, sawa na asilimia 65, zilielekezwa katika miradi ya maendeleo. Mwaka huu wa fedha, Wizara ya Afya imeidhinishiwa Sh990.7 bilioni.

Rais Magufuli aliwataka madaktari hao kutumia utaalamu wao kuanzisha viwanda vidogo ili badala ya kuendelea kuagiza dawa nje ya nchi, zianze kuzalishwe ndani.

Awatoa hofu juu watumishi wa umma

Rais pia alitolea uamuzi kero kubwa ambayo imekuwa ikisumbua watumishi wa sekta ya afya na wengine wa umma kutokana na viongozi wateule kuamuru wawekwe mahabusu wanapoona wamefanya makosa ya kiutumishi.

Katika maelezo yake, rais wa MAT, Dk Osati alimuomba Rais Magufuli kutoa maelekezo kwa viongozi hao, hasa wakuu wa wilaya na mikoa, ili wawe wanafuata sheria na miongozo.

Akijibu ombi hilo, Magufuli alisema tayari ndani ya Serikali wameshaambiana kuhusu jambo hilo na ndiyo maana siku hizi hawafanyiwi hivyo isipokuwa kwa wale wanaotenda makosa ya jinai.

Rais Magufuli alisema haiwezekani mtu ambaye si mtaalamu kuwatishia kuwaweka ndani madaktari bila kupima makosa.

Alisema utaratibu huo haufai na si tu kwa madaktari peke yao, bali kada nyingine za utumishi wa umma kama walimu na wahandisi.

“Haifurahishi na wala haiji. Unafanya operation (upasuaji) ukishatoka kule umemuhudumia vizuri, yule mtu by emergence (kwa dharura) imetokea damu zinavuja, unawekwa ndani si atakufa na huyu unayemuuuguza,” alisema Rais Magufuli.

“Najua akikuweka ndani kesho na wewe utamuweka ndani. Msifanye hivyo mtakuwa mnabeba dhambi kwa sababu kazi yenu ni kazi ambayo Mungu amewabariki.”

Aliwataka viongozi kuacha kuwaweka mahabusu wataalamu hao, lakini akasema hiyo haimaanishi kwamba madaktari wanaofanya makosa ya jinai hawapaswi kukamatwa.

“Yule aliyembaka mwanamke mwenye mimba ni lazima awekwe ndani. Yaani warembo wote waliopo Rukwa hawaoni mpaka anamtafuta mtu anamimba. Halafu akiwekwa ndani mtu analalamika? Kuna story ya namna hiyo? Naifanyia kazi,” alisema.

Alikitaka chama hicho cha madaktari kuwa na utaratibu wa kuwaonya wanaoenda kinyume na taaluma zao kabla hawajafanyiwa hivyo na wanasiasa.

“Unakuta mtu anaingia ni mlevi mnamuachia tu kwamba akinywa gongo ndipo operation inafanyika vizuri? Sasa hao muwasaidie ninyi huko, hapo ndipo tutaenda vizuri,” alisema.

“Lakini naungana nanyi kwamba si vizuri kila mwanasiasa anapofika pale anasema ‘nitakuweka ndani’. Si sawa.”

Madaktari watoa kero

Katika mkutano huo, ambao Rais Magufuli alitangaza ajira kwa madaktari 1,000 kati ya 2,000 wanaosubiri, alisikiliza kero na maoni ya madaktari.

Mmoja wa waliosungumza ni Dk Godfrey Nyaga ambaye alisema mwaka 2013 alifungua chuo kwa ajili ya kutoa mafunzo ya utabibu mkoani Mwanza akiwa na lengo la kuwaandaa wataalamu wa kada hiyo.

Hata hivyo, alisema wanafunzi wake walikuwa wakifanya mitihani ya Nacte lakini mwaka 2015 alibaini kwamba mitihani hiyo ilikuwa na kasoro. Alisema aliandika barua kwa mamlaka husika kutaka kasoro hizo zishughulikie.

Alisema mwaka uliofuata alikataa kupokea mitihani hiyo baada ya kuona suala lake halikushughulikiwa. Wanafunzi waliokuwa wakisoma chuo chake walipelekwa vyuo vingine kufanya mtihani huo.

“Nilianza kufuatilia na kufikisha malalamiko yangu serikalini, nilikwenda mpaka kwa katibu mkuu Wizara ya Afya Dodoma, akanielewa lakini baadaye aliniandikia barua yenye mambo tofauti na tuliyozungumza,” alisema Dk Nyaga.

Daktari huyo alisema alifikisha kilio chake kwa Rais Magufuli ili waliohusika katika suala hilo wachukuliwe hatua huku akitaka kulipwa fidia ya Sh24 milioni kutokana na hasara aliyoipata baada ya kufungwa kwa chuo chake.

Akijibu hoja hiyo, Rais Magufuli aliagiza wizara hiyo kumlipa Dk Nyaga kiasi hicho cha fedha ndani ya siku mbili wakati mambo mengine yakishughulikiwa.

Mwingine aliyepata nafasi ya kuzungumza ni Dk Rodrick Rubangila ambaye alisema kuna changamoto kubwa katika ushirikiano baina ya hospitali binafsi na zile za umma ambazo zinaonekana kama adui.

Alisema hospitali binafsi zipo kwa ajili ya kushirikiana na zile za umma katika kutoa huduma za afya, hivyo alitaka mamlaka za Serikali kubadili mtazamo wao na kuwaona kama wenzao katika kuwahudumia Watanzania.

“Wenzetu serikali wanatuona sisi hospitali binafsi kama tuko kwa ajili ya kutafuta hela tu na si kutoa huduma. Kuna changamoto kubwa katika mfumo wa PPP. Ifahamike wazi kwamba tupo kwa ajili ya ku-complement,” alisema Dk Rubangila.

Kwa upande wake, Dk Priscilla Msele alisema tangu ameajiriwa mwaka 2007, hajawahi kupandishwa daraja kwa madai aliyoambiwa kwamba hajafanyiwa categorization.