Mbowe, Chadema katika mawimbi yatakayoamua hatima yake

Dar es Salaam. Chama kikuu cha upinzani, Chadema kiko juu ya mawimbi ambayo kumalizika kwake kunaweza kukaiacha katika fukwe salama au mbaya, huku nchi ikiwa inaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na takribani mwaka mmoja ukiwa umesalia kabla ya uchaguzi mkuu.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanafuatilia kwa karibu kinachoendelea ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani, kukiwa na wasiwasi kwamba uamuzi wowote kwa sasa unaweza kuwa na matokeo makubwa – mazuri au mabaya—kwa mustakabali mzima wa siasa za upinzani nchini.

“Kama mipango thabiti ya kuitoa Chadema katika mkwamo wake wa sasa haitawekwa, basi athari zake zitakuwa kubwa sana si tu kwa chama hicho, bali upinzani kwa ujumla ifikapo mwaka 2020,” anaonya mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda.

“Kama busara haitatumika, 2020 utakuwa mwaka mbaya kabisa kuwahi kutokea kwa upinzani wa nchi hii. Chadema ikiwa dhaifu ni wazi kwamba upinzani utakuwa dhaifu na hiyo ni hatari sana kwa hatma ya Tanzania kama taifa,” anasema Dk Mbunda.

Kuahirisha uchaguzi

Chadema inatarajia kufanya uchaguzi wa viongozi wake kwa ngazi mbalimbali Desemba mwaka huu, baada ya Kamati Kuu kuusogeza mbele uchaguzi huo kwa kile Chadema ilichoeleza kuwa ni kushindwa kukutana kwa wanachama wake katika maeneo mbalimbali kutokana na mikutano yao kuingiliwa na Jeshi la Polisi.

Tangu marufuku ya kufanya siasa itangazwe siku chache baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani, vyama vya siasa vimekuwa vikikabiliana na mamlaka kuhusu kuzuiwa kuendeshaji shughuli zao, kitu ambacho kilimsukuma hata Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kuikemea tabia hiyo na kuwataka polisi waache mara moja.

Chadema wametumia vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikitajwa na ripoti mbalimbali za hali ya haki za binadamu nchini, kama sehemu ya utetezi wao kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye amekishutumu chama hicho kukiuka Katiba yake na Sheria ya Vyama vya Siasa kwa kushindwa kufanya uchaguzi huo ambao awali ungefanyike Septemba 14.

Tayari Chadema imemuandikia Msajili kueleza sababu za kushindwa kutekeleza takwa hilo la kikatiba. Pamoja na mambo mengine, Chadema imemweleza Msajili kwamba utaratibu wa kusogeza uchaguzi mbele umebainishwa bayana katika katiba yake ambao Kamati Kuu (CC) ya chama hicho iliuzingatia wakati wa kufikia uamuzi huo. Wakati Mwananchi inakwenda mitamboni, hakukuwa na taarifa za Msajili kujibu barua hiyo ya Oktoba 15 kutoka Chadema.

Utata mrithi wa Mbowe

Sekeseke la Chadema na Msajili linakuja wakati ambao chama hicho kinaonekana kugawanyika katika suala la nani awe mrithi wa mwenyekiti wake wa sasa, Freeman Mbowe, huku kukiwa na wale wanaomtaka mbunge huyo wa Hai aendelee kuwa mwenyekiti wao, wale ambao wanadhani amefanya makubwa na sasa ni muda muafaka wa kupata mrithi wake. Tayari baadhi wamejitokeza kutaka kufanya hivyo.

Mbowe, ambaye amekuwa akikiongoza chama hicho tangu mwaka 2004 akirithi nafasi hiyo kutoka kwa marehemu Bob Makani, hajaweza kuweka wazi nia yake kama atagombea au la. Hata hivyo, kwenye matamko yake kadhaa kuhusu suala hilo, kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni amekuwa akibainisha kwamba endapo wanachama watataka aondoke, basi atafanya hivyo.

Hata hivyo, Mbowe, ambaye anaonekana kama kiongozi wa kimkakati na ambaye upinzani dhidi ya uongozi wake ndani ya chama hicho umepungua kwa kiasi fulani kutokana na yale aliyopitia, ikiwemo kukaa gerezani kwa miezi kadhaa, alishaweka bayana msimamo wake kwamba kamwe hataondoka kama mwenyekiti wa Chadema endapo kama wanaohitaji hilo ni “makada wa CCM”.

Hisia kwamba kuna nguvu nje ya Chadema ambayo ingependa kuiona Chadema bila ya uongozi wa Mbowe ni kubwa, hususani miongoni mwa viongozi wakuu wa chama hicho. Ni kutokana na hisia hizi ndiyo maana baadhi yao wanadhani hatua iliyochukuliwa na Msajili kuhoji uamuzi wa kikatiba wa chama hicho ni sehemu tu ya mkakati madhubuti wa kufanikisha mpango ambao unalenga kunufaisha watu wengine wasio wanachama wa Chadema.

Waumini wa hoja hii wanabainisha madhila kadhaa ambayo Mbowe ameshakutana nayo mpaka sasa na hali kadhalika Chadema kwa ujumla ambayo wanadai, yanalenga kuaminisha wanachama na umma kwamba uwezo wa Mbowe kama kiongozi ni wenye shaka na hivyo anaweza kuwa mzigo, badala ya msaada, kwa chama hicho.

Dk Mbunda anaona mantiki katika hoja hii, lakini anasema ni mambo hayohayo ambayo yalipaswa kumfanya Mbowe aachie uongozi kwa kuwa kama kiongozi, alishindwa kuchukua hatua zozote za kukabiliana nayo.

Hoja hii inapingwa vikali na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema, Yericko Nyerere ambaye anadhani isingekuwa ni uongozi thabiti wa sasa ndani ya Chadema chini ya Mbowe, chama hicho kingekuwa katika hali tofauti kwa sasa.

Uwepo wa nia ovu

Kwa watu kama Nyerere, hoja ya kuwepo kwa “nia ovu” ya kuhakikisha Mbowe anaondoka Chadema kwa njia yoyote inapata nguvu kutokana na uwezo mkubwa aliopewa Msajili na sheria mpya ya vyama vya siasa nchini, hususan mamlaka aliyopewa ya kusimamia chaguzi za ndani za vyama vya siasa ambayo vyama hivyo vinadai ni njama za serikali ya CCM kuchagua nani wa kushindana naye. Ikiwa Chadema inasubiri majibu ya utetezi wake kwa Msajili, haijulikani ni kwa namna gani hili linaweza kufanyika kwa sasa.

Lakini huu ni upande mmoja tu wa shilingi. Mwingine ni ule wa kundi la vuguvugu la kudai demokrasia ya kweli ndani ya chama ambao wafuasi wake wanahoji ukiukwaji wa misingi ya kidemokrasia ndani ya chama hicho, ikiwemo kushambuliwa kwa wale wote wanaonekana kutounga mkono hoja ya kutaka Mbowe aendelee kushikilia nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa Chadema.

Wafuasi wa vuguvugu hili pia walionyesha kukerwa na ripoti za ubadhirifu wa fedha ndani ya chama hicho zilizosambaa katika mitandao ya kijamii hivi karibuni ambazo, hata hivyo, hazikuweza kuthibitishwa na ambazo baadhi ya viongozi wa Chadema walizipinga vikali, wakisema ni mkakati wa kuwavuruga.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa wamelieleza Mwananchi kwamba kitu muhimu kwa sasa ni Chadema kumaliza suala la nani atakuwa mwenyekiti wa chama hicho na hivyo kujiweka sawa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 na mipango ya kuunda muungano wa upinzani.

Mhadhiri wa sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Luisulie anasema Chadema ilichelewa kuweka mambo yake sawa na hiyo inaweza kuwa na madhara, hususani katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Ni muhimu wakalishugulikia suala hili kwa uangalifu kwani linaweza kukigawa chama au kukiiunganisha,” anasema Dk Luisulie.

Hakuna katiba imekiukwa

Kwa upande wake, Nyerere anadhani kwamba mjadala unaoendelea sasa kuhusu hatma ya Chadema ni kielelezo tosha cha ukuu wa chama hicho na uimara wake wa kuipa kashikashi CCM.

“Hakuna kifungu cha katiba wala sheria kilichovunjwa, si za Chadema wala nchi. Chama kipo imara katika kusimamia misingi ya kikatiba na kisheria kwani hicho ndo kitu pekee kinachoweza kudhihirisha utayari wake wa kushika dola,” anasema Nyerere.

Kuhusu suala la nani atakuwa mwenyekiti wa chama hicho, Nyerere anasema kwamba kila mtu ana haki ya kugombea na atachaguliwa kwa kuzingatia misingi iliyowekwa na katiba ya chama.

“Tunaamini kwamba hili litapita na chama kitakuwa imara zaidi ya sasa,” anasema huku akibainisha kwamba kwa sasa hakuna mvutano wowote wa kiuongozi ndani ya chama hicho na wala hakuna aliyekatazwa kugombea kama inavyodaiwa.

Dk Mbunda anaonya kwamba kama hakutakuwa na umakini wa jinsi Chadema itakavyoweza kushughulika na suala lake, inaweza kupoteza ushawishi kwa wananchi na hivyo nafasi yake kuchukuliwa na ACT-Wazalendo.

Lakini, kama anavyoamini Yericko Nyerere, mawimbi haya ya sasa yanaweza kuongeza nguvu zaidi kwa Chadema iwapo busara itatumika kuupangua mgogoro huu unaonekana kuwa mkubwa, tofauti na mingine iliyokikumba chama hicho kabla ya uchaguzi wa 2015.