VIDEO: Mbowe, Mwambe kujadiliwa na wajumbe 600 leo

Muktasari:

Leo mchana Jumanne Desemba 17, 2019 mkutano wa Baraza Kuu la Chadema  utajadili na kupitisha majina ya wagombea wa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa chama hicho.

Dar es Salaam. Leo mchana Jumanne Desemba 17, 2019 mkutano wa Baraza Kuu la Chadema  utajadili na kupitisha majina ya wagombea wa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa chama hicho.

Katika nafasi ya mwenyekiti, Freeman Mbowe na Cecil Mwambe watajadiliwa na ama kupitishwa au kukatwa kuwania nafasi hiyo kubwa ya chama katika uchaguzi utakaofanyika kesho Jumatano Desemba 18, 2019.

Baraza hilo linaloundwa na wajumbe 600, pia litawajadili aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na mbunge wa viti maalumu, Sophia Mwakagenda wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti.

Upande wa Zanzibar aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo ni Said Issa Mohammed ambaye anaitetea.

Katika mkutano huo unaofanyika ukumbi wa Mlimani City wajumbe wote wamevalia fulana za mikono mirefu mpya zenye rangi ya bendera ya chama hicho (nyekundu, bluu bahari, nyeupe na nyeusi)

Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, Boniface Jacob amesema  fulana hizo zimeanza kuvaliwa leo, “hizi fulana  ni sare maalumu kwa ajili ya vikao vya baraza kuu, mkutano mkuu. Huenda mwakani tukaja na sare nyingine.”

Wajumbe wa mkutano huo wamekaa katika makundi kumi kulingana na kanda za uongozi za chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.