Mkapa afichua sababu ya kumtetea Mahalu

Rais mstaafu Benjamin Mkapa ameeleza sababu iliyomfanya kuamua kusimama mahakamani kumtetea aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu.

Mkapa alifanya kitendo hicho Mei 6, 2012 na kuibua mjadala mkubwa katika medani ya sheria na siasa nchini kuhusu rais aliyeondoka madarakani kupanda kizimbani kutoa utetezi.

Kitendo hicho kilimfanya kuwa Rais wa kwanza Tanzania kusimama mbele ya mahakama kutoa ushahidi katika kesi inayohusu tukio lililotokea wakati wa utawala wake.

Mkapa aliongoza nchi kuanzia mwaka 1995, wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi tangu siasa za ushindani zirejeshwe mwaka 1992, hadi mwaka 2005 alipomkabidhi Jakaya Kikwete.

Profesa Mahalu na Grace Martin aliyekuwa ofisa utawala wa ubalozi huo, walikuwa walishtakiwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60 (Sh5 bilioni) katika mchakato wa ununuzi wa jengo la ubalozi nchini Italia.

Katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu)” alichozindua juzi, Mkapa anasema alichukua uamuzi huo kwa kuwa alikuwa anafahamu ukweli wa jambo hilo lilitokea chini ya utawala wake.

Mahalu, ambaye alishinda kesi hiyo, alikuwa anatuhumiwa kwa kufanya malipo ya ununuzi wa jengo hilo kinyume cha taratibu za serikali kwa kufanya sehemu ya malipo hayo katika benki moja ya Italia na mengine benki ya nje ya nchi hiyo kutokana na maombi ya muuza jengo hilo.

“Mimi ndio nilitoa idhini ya kufanya malipo kwa utaratibu huo baada ya kupewa maelezo na Profesa Mahalu, ambaye kutokana na mwenye jengo kusisitiza utaratibu huo kwani lilikuwa jambo la kawaida nchini Italia,” anasema Mkapa katika kitabu hicho.

Mkapa anasema tuhuma dhidi ya Mahalu zilitolewa katika mazingira ya kutatanisha kwa kuwa kuna mtu alipiga simu katika redio moja na kudai alikuwa ana ushahidi wa tuhuma dhidi ya Profesa Mahalu na ndio maana Takukuru ikaanza kuchunguza.

Mkapa anaeleza kuwa alifanya jitihada za kuwaona Takukuru ili kuwaomba waachane na kesi hiyo kwa kuwa hakukuwa na tatizo na malipo hayo, lakini waliamua kuendelea nayo.

Alisema kutokana na hali hiyo ndipo alipokata shauri na kuamua kupanda kizimbani kwa nia ya kumtetea Mahalu.

“Nilishangaza wengi kwa uamuzi wangu wa kwenda mahakamani kumtetea Profesa Mahalu. Ninaelezwa hata Rais Jakaya Kikwete hakuamini pale aliposikia kuwa ninakwenda mahakamani,” anasema Mkapa.

Mkapa na msafara wake ulioongozwa na maofisa wa itifaki, aliwasili mahakamani kutoa ushahidi wake siku hiyo.

Alikula kiapo maalumu katika kesi hiyo iliyosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ilvin Mugeta ikiongozwa na Alex Mgongolwa, mmoja wa mawakili wa Profesa Mahalu.

Mkapa alijibu maswali kwa kujiamini na kwa umakini mkubwa huku mara kadhaa akiwavunja mbavu wasikilizaji kwa jinsi alivyowajibu mawakili wa Serikali.

Mkapa alisema kuwa Serikali yake ilifahamu ununuzi wa jengo hilo na taratibu za malipo baada ya kufahamishwa na Profesa Mahalu na kwamba lilinunuliwa kwa maagizo ya Serikali yake.