Mkapa aonya udini, ukabila na umaskini

Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa

Dar es Salaam. Katika maisha ya Watanzania si rahisi kuona waziwazi masuala kama ya udini, ukabila na ukanda, lakini Benjamin Mkapa, ambaye ameliongoza Taifa hili kwa miaka kumi, anaona kuna dalili ya mambo hayo hatari kwa mshikamano wa nchi.

Pia anaonya kuhusu umaskini, akisema ni kitu kingine kinachoweza kuiingiza nchi katika machafuko iwapo hakitashughulikiwa.

Tanzania, ambayo ina takriban makabila 120 na dini kubwa mbili, ni moja kati ya nchi chache barani Afrika ambazo hazijatumbukia katika migogoro inayotokana mambo hayo, Kiswahili kikihusishwa na mafanikio hayo.

Lakini katika kitabu cha “My Life, My Purpose (Maisha yangu, Kusudi Langu)”, Mkapa anaonyesha wasiwasi wa mambo hayo kukua na kuonya kuwa yakiendelea yanaweza kuvuruga amani ya nchi.

Mkapa anasema tangu kuasisiwa kwa Taifa la Tanzania, kumejengwa misingi imara ya umoja ambayo imekuwa mfano kwa mataifa mengine.

Bila ya kuweka bayana, Mkapa anasema katika miaka ya karibuni kumekuwa na viashiria vya kuibuka kwa udini, ukabila na ukanda.

“Kuna dalili za watu kuanza kubaguana kwa misingi ya kidini na ukabila katika taifa letu. Hili jambo ni la hatari,” anaeleza Mkapa, ambaye alikuwa Rais wa Tanzania kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.

Anasema lazima Taifa lichukue hatua za dhati za kuhakikisha tunu ya umoja wa kitaifa inalindwa.

Suala la ukabila na udini ni nyeti nchini kutokana na muingiliano mkubwa wa watu katika ndoa na makazi, ingawa mitandao ya kijamii inaonyesha dalili za tofauti za kimakundi, hasa kiitikadi.

Hivi karibuni, gazeti hili lilikariri wasomi, wanasiasa na viongozi wa dini wakitaka wananchi kuacha mara moja kauli za chuki na za kufurahia mabaya yanayowatokea wenzao.

Kisiasa, vyama vya upinzani vinadai kubaguliwa kuendesha shughuli hizo na wiki iliyopita, vyama vinane vilijitoa katika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa vikidai kutotendewa haki na wasimamizi wasaidizi baada ya wagombea zaidi ya asilimia 90 wa chama tawala kutangazwa washindi kutokana na wapinzani wao kukutwa na kasoro zinazoonekana kushabihiana katika maeneo tofauti, hasa kuandika kifupi cha majina ya vyama vyao.

Mkapa pia amezungumzia hatari ya umaskini kwa amani ya Taifa, akisema umaskini wa wananchi wengi ni kati ya masuala yanayozaa chuki na mpasuko katika nchi.

Anashauri Serikali kufanya mipango madhubuti ya kuinua maisha ya wananchi. “Viongozi wana dhamana ya kuandaa mikakati ya kuinua maisha ya watu ya wananchi, kwa kuwa umaskini katika nchi unaweza kuondoa utulivu,” anasema Mkapa, ambaye katika enzi yake aliandaa mikakati kama Mkukuta na Tasaf kujaribu kupambana na tatizo hilo.

Mkapa anashauri viongozi wa CCM na upinzani kuchukulia suala la umaskini wa wananchi kuwa ni tishio la amani ya nchi.

Ametoa mfano wa nchi jirani zilizowahi kuingia katika machafuko kutokana na umaskini na tofauti za itikadi za kisiasa.

“Jirani zetu Kenya, Uganda, Msumbiji, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zote ziliiingia katika machafuko kutokana na matatizo ya kisiasa ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na umaskini wa wananchi wa mataifa hayo,” anaeleza Mkapa.

“Sisi Watanzania tusijione tupo katika kisiwa, tukifikiria yale yaliyotokea nchi nyingine, hayawezi kutokea hapa. Kwa kweli lolote linaweza kutokea,” anasema Mkapa.

Mkapa anashauri zaidi kuwepo uchumi shirikishi ili kusaidia kuinua maisha ya walio wengi nchini.

Amesema wananchi wanapaswa kupewa fursa za kiuchumi ili nao wapige hatua kimaisha.

Mkapa anaonya kuhusu hali ya sasa ya mashamba na kampuni makubwa kumilikiwa na watu wenye asili ya kiasia.

“Hali hii inanipa wasiwasi kuwa suala hili linaweza kusababisha wivu na kusababisha mgawanyiko katika taifa,” anasema Mkapa.

Mkapa anasisitiza kuwa vita vya kupambana na umaskini, lazima viongezwe ikiwa ni njia mojawapo ya kudumisha umoja na amani ya Taifa.

Mkapa anashauri, hata hivyo, ni vizuri kwa Watanzania kurejea kwenye Azimio la Arusha lililoandikwa mwaka 1967 na chama cha Tanu ikiwa kipindi kifupi baada ya taifa kupata uhuru.

Anadai anasikitishwa kuona kuwa kizazi cha sasa kimeshindwa kulitumia Azimio la Arusha, ambapo kama wakiliongelea basi inakuwa kwenye suala la maadili ya viongozi pekee.

Mkapa anadai kuwa azimio lile lilikuwa linagusa masuala yote ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Pia anaongeza kuwa azimio hilo linatoa mwongozo wa rasilimali kutumika vizuri kwa manufaa ya nchi.

Anaamini kuwa azimio hilo bado lina nafasi yake kama kweli taifa linataka kuzuia mpasuko.