Mnyika katibu mkuu Chadema, Kigaila na Mwalimu manaibu wake

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe leo Ijumaa  Desemba 20, 2019 amemteua mbunge wa Kibamba, John Mnyika kuwa katibu mkuu wa chama hicho akichukua nafasi ya  Dk Vicent Mashinji.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe leo Ijumaa  Desemba 20, 2019 amemteua mbunge wa Kibamba, John Mnyika kuwa katibu mkuu wa chama hicho akichukua nafasi ya  Dk Vicent Mashinji.

Mbali na Mnyika, Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni  amemteua Benson Kigaila kuwa naibu katibu mkuu (Bara) nafasi iliyoachwa na  Mnyika huku Salum Mwalimu akiendelea kuwa naibu katibu mkuu Zanzibar.

Akizungumza na wajumbe wa baraza kuu la chama hicho, Mbowe amesema amemteua Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche kuwa mjumbe wa uongozi katika sekretarieti ya kamati kuu.

Katika mkutano huo ulioanza jana mchana katika ukumbi wa Mlimani City, pia walichaguliwa wajumbe wanane wa kamati kuu.

Akitangaza matokeo hayo,  Dk Mashinji amesema wajumbe walikuwa  412 lakini 405 ndio waliopiga kura huku kura mbili zikiharibika.

Amesema walioshinda kwa upande wa Zanzibar ni Yahya Alawi na  Zeus Mvano Abdallah huku Samson Mwambwene na Sarah Katanga wakichaguliwa kupitia kundi la walemavu.

Wengine ni Gibson Meseyeki, Patrick Ole Sosopi, mbunge wa Viti Maalum,  Grace Kihwelu na Susan Kiwanga (Mlimba).