Morrison sio bure kuna kitu

Muktasari:

Katika mchezo dhidi ya Namungo, Morrison ndiye aliyeifungia Simba, bao la pili kwa shuti la mguu wa kulia huku la kwanza akilisababisha yeye kutokana na penati ambayo ilipatikana baada ya kufanyiwa madhambi katika eneo la hatari.

STRAIKA Chris Mugalu ameendeleza kasi yake ya kufumania nyavu, baada ya usiku wa juzi kuifungia timu yake mabao mawili kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Mlandege, lakini wakati akifanya hivyo, mambo yanaendelea kuwa tofauti kwa nyota aliyetua kibabe katika timu hiyo, Bernard Morrison ‘BM3’.

Wakati Mugalu aliyesajiliwa naye katika kipindi kimoja akiendelea kuwatungua makipa wa timu pinzani, mabao yameonekana kukauka kwa Morrison ambaye wengi walitegemea angekuwa tishio katika kufumania nyavu kutokana na makali aliyoyaonyesha ndani ya muda mfupi alioichezea Yanga.

Winga huyo Mghana tangu alipoifungia Simba bao katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo FC, Agosti 30 hajaweza tena kufanya hivyo katika mechi saba mfululizo zilizofuata za Simba katika Ligi Kuu na zile za kirafiki dhidi ya Mlandege, Biashara United, African Lyon, Ihefu SC, Gwambina, JKT Tanzania na Mtibwa Sugar.

Katika mchezo dhidi ya Namungo, Morrison ndiye aliyeifungia Simba, bao la pili kwa shuti la mguu wa kulia huku la kwanza akilisababisha yeye kutokana na penati ambayo ilipatikana baada ya kufanyiwa madhambi katika eneo la hatari.

Lakini baada ya hapo, nuksi ya kutofumania nyavu imeonekana kumuandama Morrison kwani ameshindwa kufunga bao katika jumla ya dakika 319 alizocheza kwenye mechi saba (7) za kirafiki na za Ligi Kuu ambazo alicheza.

Ilianzia katika mechi dhidi ya Ihefu ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 aliyocheza kwa dakika 67 na baadaye akashindwa kufunga katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo nayo alikuwa uwanjani kwa dakika 67.

Mambo yakaanza kugeuka kwa Morrison katika mechi nne zilizofuata ambazo Simba ilicheza dhidi ya Biashara, Gwambina, African Lyon na JKT Tanzania kwani zote alianzia benchi na licha ya kuingizwa uwanjani hakuweza kufunga bao.

Katika mechi dhidi ya Biashara, Morrison aliingia katika dakika ya 72 na kushindwa kufunga, akacheza kwa dakika 22 dhidi ya Gwambina bila bao na kisha katika mchezo dhidi ya African Lyon hakufanya hivyo licha ya kucheza kwa dakika 28.

Lakini katika mchezo wa juzi wa kirafiki dhidi ya Mlandege, benchi la ufundi la Simba lilimpa fursa ya kucheza kwa dakika 90, lakini licha ya timu hiyo kushinda mabao 3-1, Morrison aliondoka patupu huku mabao hayo yakifungwa na Chris Mugalu aliyepachika mawili na moja likifungwa na Ibrahim Ame.

Kitu kikubwa na cha kujivunia ambacho Morrison amekifanya katika mechi hizo saba alizocheza ni pasi ya mwisho moja ambayo ilizaa bao la Chris Mugalu katika ushindi wa mabao 3-0 ambao Simba waliupata dhidi ya Gwambina FC.

SVEN AMTETEA

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck hata hivyo amemtetea Morrison na kusema takwimu hizo sio kitu anachotilia sana maanani isipokuwa namna wachezaji wanavyocheza.

“Takwimu hazihitimishi kila kitu katika mchezo wa soka ingawa zinasaidia kumjengea mchezaji hali ya kujiamini.

Jambo la muhimu la kuliangalia ni mchango wa mchezaji ndani ya uwanja na namna alivyocheza. Unaweza kuwa na takwimu nzuri na usicheze vyema,” alisema Sven ambaye anajiandaa na vijana wake kuifuata Tanzania Prisons kwa mechi yao ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa Sumbawanga mkoani Rukwa.