VIDEO: Moto mpya Membe, Makamba, Kinana

Dar es Salaam. Moto umeanza upya ndani ya CCM baada ya kutulia kwa muda.

Halmashauri Kuu ya CCM imeagiza makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, Yusuf Makamba pamoja na waziri wa zamani, Bernard Membe waitwe kuhojiwa.

Na Membe, ambaye ni mmoja wa makada wa CCM waliojitokeza kuwania urais mwaka 2015, amesema hana tatizo na wito huo ingawa hajaupata, huku Makamba akisema hawezi kuuzungumzia kwa kuwa hajaupata.

Vigogo hao, waliokuwa mjadala hvi karibuni baada ya sauti za baadhi yao kusambaa mitandaoni wakizungumzia kupasuka kwa CCM, watahojiwa na Kamati ya Usalama na Maadili kuhusu tuhuma za kimaadili.

Kinana na Makamba pia waliwasilisha malalamiko yao CCM wakidai uongozi hauwalindi dhidi ya mtu ambaye amekuwa wakiwadhalilisha na ambaye walimuelezea kuwa analindwa na mtu mwenye mamlaka.

Wakati vigogo hao wakitakiwa kuhojiwa, Halmashauri Kuu imewasamehe na kuwaonya wabunge wa tatu, January Makamba (Bumbuli), William Ngeleja (Sengerema) na Nape Nnauye (Mtama) ambao kwa nyakati tofauti walimuomba msamaha mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli.

“Kikao cha Halmashauri Kuu Taifa kimewataka wanachama hao (January, Ngeleja na Nape) kujirekebisha na kutorudia makosa yao ama sivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za chama ikiwamo kufukuzwa uanachama,” imesema taarifa ya Halmashauri Kuu ya CCM.

Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu wito huo, Membe alisema: “Nimepata habari hiyo, ninasubiri kwa hamu kubwa sana barua ya wito wa kikao hicho.”

Lakini Makamba, alisema: ”Sijapata huo wito, nikipata nitazungumza.”

Kuitwa kwa makada hao ni kuibua upya sakata lililoonekana kutulia ndani ya CCM. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ali aliwahi kumlaumu Membe kutoonekana tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu.

Dk Bashiru, akiwa mkoani Geita, alimtuhumu Membe hadharani kuwa anakwamisha mkakati wa urais 2020 wa Rais Magufuli, huku akimtaka afike ofisini kwake.

Lakini waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje alimjibu kuwa CCM ina utaratibu wake wa kuitana.

Ujumbe huo wa Twitter uliotumwa na mtu mwenye jina kama la Membe ulisema atakapokwenda ofisini kwa Dk Bashiru, mtu anayemtuhumu kuandaa mkakati wa kumng’oa Rais Magufuli, naye awepo ili athibitishe tuhuma hizo.

Hivi karibuni ziliibuka sauti za viongozi mbalimbali, zikiwamo zinazosadikika kuwa ni za wabunge hao, zikizungumzia waraka ulioandikwa na Makamba na Kinana kuhusu uongozi wa CCM kutowalinda dhidi ya vitendo vya kudhalilishwa.

Makatibu hao wa zamani waliandika waraka huo kwa katibu wa Baraza la Ushauri wa Viongozi wa CCM, Pius Msekwa wakizungumzia mmoja wa wanaharakati ambaye amekuwa akiwachafua bila hatua kuchukuliwa.

Makamba na Kinana waliokuwa watendaji wakuu wa chama hicho tawala katika awamu ya nne, walitumia katiba ya CCM, toleo la 2017 ibara ya 122 kuwasilisha malalamiko yao ambayo yalizua mjadala ndani na nje ya chama hicho.

Msekwa aliwaandikia barua vigogo hao akijibu malalamiko yao waliyoyawasilisha kwake wakidai kudhalilishwa kwa mambo ya uzushi, uongo na mtu aliyejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

“Kama mnavyofahamu, baraza hili hufanya kazi kwa njia ya vikao rasmi na kwamba katibu peke yake hana mamlaka ya kutoa maamuzi yoyote. Kwa hiyo, nitawasilisha barua yenu kwa wajumbe wa baraza ili kupata maelekezo yao juu ya nini kifanyike,” alisema spika huyo wa zamani aliyeongoza Bunge kati ya mwaka 1994 hadi 2005.

Baada ya suala hilo kuanza kupoa, Rais Magufuli alisema January na Ngeleja walimfuata na kumuomba msamaha, na baadaye Nape akafuatia kwa kwenda mwenyewe Ikulu kumuomba msamaha kiongozi mkuu huyo wa nchi.

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa na katibu wa itikadi na uenezi, Humphrey Polepole inaeleza kuwa hatua hiyo imefikiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika jijini Mwanza chini ya uenyekiti wa Magufuli.

Mbali na Membe, kuitwa kwa makatibu hao wastaafu kumekuja miezi michache baada ya malalamiko yao ya Julai 14, 2019, wakimlalamikia mtu waliyedai kuwa anatumia vyombo vyake vya habari kuwachafua.

Msekwa aliwataka makatibu hao kujibu mapigo.

Kuitwa kwao kunaashiria msuguano mkali ndani ya chama hicho kwa kuzingatia nafasi za makatibu hao wakuu waliokitumikia chama hicho kwa nyakati tofauti.

Mbali na Makamba aliyekuwa katibu tangu mwaka 2006 hadi 2011, Kinana, aliyeshika wadhifa huo tangu mwaka 2012 chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, alitumia muda mwingi kukirejesha kwenye misingi yake huku akipambana na mawaziri aliowaita kuwa mizigo.

Kinana alionyesha nia ya kustaafu mara baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani Novemba 2015, uamuzi alioutekeleza Mei 27, 2018 na baadaye nafasi yake kuchukuliwa na Dk Bashiru Ally.

Katika hatua nyingine, taarifa hiyo pia imesema licha ya hamasa kubwa waliyokuwa nayo wajumbe wa Halmashauri Kuu kutokana na kazi ya Serikali ya CCM, Rais Magufuli amesisitiza kutoongeza kipindi chake cha urais.

Kauli hiyo ya Rais imekuja ikiwa ni siku moja tangu Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda kusema kama Katiba ingeruhusu angeshauri Magufuli aongezewe japo miaka mitano.

Lakini taarifa hiyo imesema: “Magufuli amesisitiza kazi ya Urais ni ngumu sana na yeye ataheshimu utamaduni na desturi za CCM, kanuni, katiba ya CCM na Katiba ya nchi na kwamba CCM ni kiwanda cha kuzalisha viongozi na kwa utaratibu ambao chama kimejiwekea kitampata mtu bora zaidi atakayepokea uongozi baada yake.”

Uteuzi wa wagombea

Taarifa hiyo imesema awali Kamati Kuu ya chama hicho ilifanya uteuzi wa majina ya Wagombea wa nafasi za uongozi katika Chama na Jumuiya wakiwemo wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha ambao ni pamoja na Batilda Buriani, Zelothe Zelothe na Bakari Msangi.

Nafasi nyingine ni wagombea wa nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Iringa zinazogombewa na

Mafanikio Paulo Kinemelo, Hilary Kipingi na Lucas Lwimbo.

Nyingine ni wagombea wa nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Mtwara ambao ni Petro Mwendo, Mustafa Mohamed, Selemani Sankwa, huku nafasi za wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Wazazi Mkoa wa Dodoma wakipitishwa Damas Kasheegu, Baraka Mkunda, Christopher Mullemwah.

Nyingine ni za wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Pwani ambapo waliopitishwa ni Mary Joseph, Fredrick Makachila na Samaha Said