Msimamo wa Msigwa na undugu na Rais Magufuli

Mbunge wa Iringa Mjini akizungumza na waandishi katika makao makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam jana. Picha na  Erick Boniphace

Dar es Salaam. Baada ya Rais John Magufuli kumlipia faini Peter Msigwa, mbunge huyo wa Iringa Mjini amesema kitendo hicho kisiwaondoe watu katika hoja ya msingi na kwamba yeye hawezi kununulika “kwa vipande 30” vya fedha.

Mchungaji huyo wa Kanisa la Vineyard, amesema masuala ya kifamilia kati yake na Magufuli yanaeleweka na hawezi kuyazungumzia hadharani kwa kuwa Taifa ni kubwa kuliko familia yake.

Alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu tukio hilo lililoibua mjadala kuhusu mustakabali wake ndani ya Chadema baada ya mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Gerson Msigwa kwenda mahakamani juzi akiwa na baadhi ya ndugu zake kumlipia faini hiyo ya Sh40 bilioni, zikiwamo Sh38 milioni zilizotolewa na Rais.

Pia baadaye mchana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alikwenda katika Gereza la Segerea kwa ajili ya kumtoa.

Ilikuwa ni baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kumuhukumu mchungaji huyo na wenzake wanane kulipa faini ya jumla ya Sh350 milioni au wakishindwa kwenda jelamiezi mitano.

Lakini jana Msigwa alijikita zaidi katika harakati zao alizosema za kudai demokrasia, utawala bora na uwazi, mambo ambayo alisema ni makubwa zaidi kuliko masuala ya kifamilia.

“Kwa hiyo masuala ya familia ya mimi na Magufuli yanazungumzwa kifamilia, huwa hayatoki hadharani,” alisema mbunge huyo.

“Kwa hiyo, siko tayari kuacha masuala ya msingi ya demokrasia, good governance (utawala bora) na transparency (uwazi) nianze kuzungumza masuala ya familia. This nation is bigger than my family (Taifa hili ni kubwa kuliko familia yangu. Kwa hiyo tusiache vitu vya msingi tukaanza kuzungumza vitu vya nini... na waandishi wa habari mlione hili tatizo kuwa kubwa.”

Mchungaji Msigwa aliweka bayana kuwa uhusiano wake wa kifamilia na Magufuli ni jambo ambalo linaeleweka na kwamba hata chama chake kinajua, lakini hilo haliwezi kusababisha aache kuzungumzia mambo ya msingi ya nchi.

Alivyotoka gerezani

Juzi mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa alifika Mahakama ya Kisutu akiwa na kaka wa mbunge huyo, Mchungaji Benert Msigwa na kulipa Sh38 milioni zilizotolewa na Rais Magufuli pamoja na Sh2 milioni zilizotolewa na familia.

Hiyo ni baada ya Msigwa na wenzake wanane, kuhukumiwa Machi 10 kifungo cha miezi mitano jela au kulipa faini baada ya kutiwa hatiani kwa mashtaka 12 kati ya 13.

Baada ya hukumu hiyo Chadema ilianza kuchangisha fedha kwa wananchi ili kuwalipia viongozi hao waliohukumiwa Jumanne.

Hata hivyo, suala la Msigwa pekee ndilo lililoibua utata baada ya kulipiwa mara mbili.

Viongozi wa Chadema walidai kuwa magari ya Serikali ndiyo yalikwenda kumchukua Msigwa, ingawa baadaye inaaminika aliondoka na gari la wakili wake.

Jana asubuhi waliachiwa wenzake John Mnyika, katibu mkuu wa Chadema, Naibu katibu mkuu (Zanzibar), Salim Mwalimu na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Waliyonena baada ya kuachiwa

Akizungumzia suala la kuachiwa kwao, katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema kiwango cha fedha kilichochangwa ndani ya siku mbili kimeonyesha ni kwa namna gani wananchi wanavyoweza kufanya uamuzi.

“Umma una nguvu, kama tumeshnda jaribio hili tusonge mbele ili kushika dola,” alisema Mnyika.

Alisema ili kupunguza msongamano gerezani ipo haja ya kuangalia upya kesi za uhujumu uchumi.

“Kesi zinazoitwa za uhujumu uchumi zifanyiwe kazi mapema ili kuamua hatima za watu, ikiwezekana watoke ili kupunguza msongamano usiokuwa na maana,” alisema.

Kwa upande wake, mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, John Heche alisema kwa namna kesi hiyo ilivyokuwa inaendeshwa alikuwa ameshajiandaa kufungwa.

“Kulikuwa na kesi ndogondogo ndani. Sitampigia mtu magoti kwa tulichofanyiwa. Tukiwa gerezani tumeona mengi,” alisema.

Alisema wakati anachukuliwa baada ya kulipiwa faini alikuwa analima hata mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alimuacha akilima.

Naye Salum Mwalimu alisema kitendo cha kuwekwa ndani kumeibua joto la uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

“Tumetoka gerezani sasa joto hili litaendelea hadi uchaguzi mkuu, yapo mambo tuliojifunza tukiwa ndani hatutanyamaza,” alisema Mwalimu.

Chadema wafunga namba za kuchangia

Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria, Hezekia Wenje alisema baada ya kufanikiwa kulipia viongozi wao, wamefunga laini walizokuwa wanatumia kuchangisha.

Wenje alisema walifikisha Sh312 milioni tangu walipoanzisha michango Jumanne iliyopita baada ya viongozi hao kuhukumiwa.

“Namba za simu tulizokuwa tunatumia kuchangisha tumezifunga rasmi tunawashukuru wote waliotuchangia.

“Tumefanikiwa kuwalipia viongozi ambao wametoka na pia Mwenyekiti wa Chadema Taifa, ambaye tunategemea atatoka wakati wowote,” aliongeza Wenje.