Mwinyi aingia Ikulu, Nyerere aaga Taifa 1985

Safari ya kung’atuka madarakani kwa Mwalimu Julius Nyerere baada ya kuhudumu kwa miaka 24 kwa nafasi ya urais wa Tanganyika na baadaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilianza Jumatatu ya Oktoba 14, 1985.

Ilikuwa ni baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 27 na mgombea pekee wa nafasi ya urais, Ali Hassan Mwinyi akaibuka mshindi.

Kampeni hizo zilianza kwa kuchelewa kwa siku saba kutoka Oktoba 7 hadi 14 kutokana na uhaba wa mafuta ya petroli na dizeli.

Katika kampeni hizo, Mwalimu Nyerere aliwataka wananchi wote waliojiandikisha, kujitokeza na kumpigia Mwinyi kura za “Ndiyo” ili kukamilisha utaratibu wa kikatiba wa kubadilisha viongozi.

Akiwahutubia maelfu ya wakazi wa mkoa wa Iringa katika Uwanja wa Samora, Nyerere alisema kura nyingi za “Ndiyo” ni ishara ya imani kubwa ya wananchi.

“Tukianza kwa kumwamini, atajiamini na kufanya kazi nzuri tutakazomtuma. Si jambo rahisi kuwaambia watu wafunge mikanda wakati watu wana njaa,” alisema.

“Lakini niliwaambia hivyo (mfungemikanda), kwa kuwa nilikuwa najua wananchi wana imani na mimi.”

Kampeni zilichelewa kuanza kwa siku saba kutokana na uhaba wa mafuta wakati huo.

“Hali ya uchumi ilikuwa mbaya,’’ anasema mwanasiasa mkongwe, Njelu Kasaka katika mazungumzo na Mwananchi kuhusu uchaguzi huo wa mwaka 1985.

“Hali hiyo ilisababishwa na mafuta ya petroli kuingizwa machache na hakukuwa na vituo vya mafuta kama sasa.

“Kulikuwa na vituo vichache vya mafuta ya dizeli na petroli na ili uyapate kulingana na gari ulilonalo, tulikuwa tunapewa kadi maalumu tulizokuwa tunatumia kwenda vituoni kujaza.”

Anasema kadi zilikuwa za aina mbili; za wenye magari madogo waliopewa lita 50 kwa wiki na wenye magari makubwa lita 70 kwa wiki.

“Ilikuwa ukijaza mafuta Jumatatu, unapaswa kujaza tena Jumatatu, lakini yakiisha kabla ya Jumatatu, unapaki gari lako na kila mtu alikuwa anapewa kituo maalumu cha kujaza,” alisema Kasaka.

“Uhaba huo wa mafuta ulisababisha kampeni kuchelewa kwa sababu hatukuwa na fedha za kigeni za kununua mafuta ya kutosha.”

Mwanasiasa huyo anasema kipindi kile waliokuwa wanamiliki magari walikuwa wachache pia, na aliyetaka kununua gari alilazimika kuomba kibali na kueleza sababu. Uhaba huo wa mafuta uliendelea hadi miaka ya 1990.

Hata hivyo anasema pamoja na changamoto hiyo, lakini nchi ilifanikiwa kufanya uchaguzi na matokeo yakatangazwa.

Akikumbuka uchaguzi huo, Kasaka alisema kampeni za wakati ule zilifanywa na wenyeviti wa mikoa na wilaya na makatibu wao, mgombea wa urais alifanya mikutano michache zaidi.

Anasema waliokuwa wanafanya kampeni walikuwa wagombea nafasi za ubunge, katika kila mkutano wenyeviti na makatibu hao walikuwa wanahudhuria kwa lengo la kumwombea kura mgombea urais.

Kasaka, mmoja wa waasisi wa Kundi la G55 lililotaka kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika mwaka 1993, anasema wagombea ubunge walikuwa wanapewa fursa ya kujieleza na kuulizwa maswali matatu.

Kasaka anasema tofauti na ilivyo sasa, marais waliofuatia, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na sasa John Magufuli wao waliomba ridhaa kwa wananchi kwa wao wenyewe kupiga kampeni nchi nzima hadi ngazi za wilaya na vijiji, lakini wakati wa chama kimoja haikuwa hivyo.

Kutangazwa kwa matokeo

Novemba 1, 1985 ilikuwa siku ya kutangazwa kwa matokeo ya urais. Shughuli hiyo ilifanyikia ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Chifu Adam Sapi Mkwawa alimtangaza Mwinyi kuwa mshindi baada ya kupata asilimia 92.2 ya kura zote milioni 5.18.

Kura za “Ndiyo” zilikuwa milioni 4.8 na za “Hapana” zilikuwa 215,626 wakati kura 188,259 ziliharibika.

Idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 6,901,555.

Chifu Mkwawa alisema matokeo hayo yalionyesha zaidi ya nusu ya wapiga kura waliojitokeza, wamemkubali mgombea pekee wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Hivyo basi, kwa mujibu wa fungu la 41, ibara ya 3(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sasa natangaza rasmi kuwa ndugu Ali Hassan Mwinyi amechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Chifu Mkwawa ambaye sasa ni marehemu.

Shughuli hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali akiwamo Mwalimu Nyerere, Rais mteule wa Zanzibar, Idris Abdul Wakil; Waziri Mkuu Dk Salim Ahmed Salim na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad ambaye sasa ni mwenyekiti wa ACT- Wazalendo.

‘Mtumishi na si mtawala’

Wakati mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi alipomuomba Mwalimu Nyerere aseme lolote baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Nyerere alisema, “Ndugu wananchi, siwezi kusema”.

Mwinyi alipopewa nafasi ya kuzungumza, aliahidi kuwa katika kipindi atakachokuwa madarakani, atakuwa “mtumishi na si mtawala”.

Alitoa ahadi hiyo katika hotuba yake fupi ya shukrani baada ya kutangazwa kurithi rasmi kiti kilichoachwa na Mwalimu Nyerere.

“Nakubali kuubeba mzigo wa kuwa mtumishi wa Watanzania wote na si mtawala. Nitajitahidi kulitumikia Taifa, kwa kusaidiana na viongozi wenzangu bila upendeleo wa dini, ukabila, rangi au mahali mtu alikozaliwa,” alisema Mwinyi.

“Niliamini nitashinda uchaguzi huu, lakini si kwa asilimia kubwa kama ilivyotokea. Nimefurahishwa kupita kiasi. Ushindi huu ninauchukulia kuwa ni deni kwa Watanzania na nawashukuru waliopiga kura za ‘Ndiyo’ kwa imani yao kwangu.”

Huku akishangiliwa na wananchi na viongozi waliojitokeza, Mwinyi pia aliwashukuru waliopiga kura za kumkataa.

“Najiona nina deni nisiwavunje moyo kwa kubahatisha. Naahidi nitawatumikia wote hawa sawasawa, hata kama ningewajua,” alisema.

Kwa sababu wananchi wengi walimuamini sana Nyerere, Kasaka anasema walionekana hawana imani na uhakika na hali ambavyo ingekuwa katika uongozi wa Mwinyi na wengi walidhani nchi isingeweza kuendelea bila Mwalimu.

“Watu walikuwa na wasiwasi, hawakujua kama Mwinyi ataiendesha nchi vizuri. Imani yao ilikuwa kwa Nyerere ambaye aliendelea kuwa mwenyekiti wa chama hivyo walijua atadhibiti akiona hali inatetereka,” alisema Kasaka,

Anasema baada ya Mwinyi kuanza kazi, kwa bahati mbaya nchi ilikuwa na hali mbaya ya uchumi, Serikali ilikuwa haina fedha za kutosha, viwanda havizalishi vizuri, hivyo mwaka 1986 ilibidi aingie katika majadiliano na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF).

Kasaka anasema lengo la majadiliano hayo lilikuwa ni kulegeza masharti ya kiuchumi na akafanikiwa. Bidhaa zikaanza kuingia nchini kidogokidogo na kuufanya uchumi huria.

“Baada ya hapo sasa ndiyo kampuni zikaanza kuagiza bidhaa na malighafi kutoka nje na hali ya uchumi ikaanza kurejea na baadaye wananchi wakaanza kumuamini sasa,” anasema Kasaka.

Mwalimu Nyerere alivyoliaga Taifa

Siku moja kabla ya Mwinyi kuapishwa, Rais Nyerere aliwashukuru Watanzania wote kutokana na imani na ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha miaka 24 ambacho alikuwa Rais.

Nyerere alilihutubia Taifa Jumatatu Novemba 4, 1985 katika ukumbi wa Diamond Jubilee.

“Asanteni sana Watanzania wote, wananchi waliojiunga pamoja katika vijiji, katika vikundi vya ushirika, taasisi, mashirika yanayosaidia na wafanyakazi wote waaminifu,” alisema Nyerere.

“Nawashukuru kwa umoja wenu katika mapambano yote ambayo yametukabili na bado tukaifikisha Tanzania hapa ilipo.”

Mwalimu Nyerere alisema katika kipindi chote ambacho alikuwa akiagana na wananchi na marafiki mbalimbali wa nje ya nchi, amekuwa akipata sifa nyingi, ambazo alisema zilitokana na mambo ambayo Watanzania wameyafanya.

“Hakuna malaika ambaye angeweza kujenga Tanzania peke yake hata kama malaika huyo angekuwa anasaidiwa na kuungwa mkono na baraza la mawaziri ambao wote ni malaika,” alisema Nyerere.

Alisema mambo mbalimbali ambayo yamefanywa na Tanzania ni matokeo ya uamuzi wao kutumia haki ya demokrasia kumchagua Rais na wale ambao kwa kutimiza haki ya demokrasia walipiga kura ya “Hapana”, lakini wakaonyesha imani yao kwake baada ya matokeo ya uchaguzi kutokana na kuheshimu utaratibu wa demokrasia.

“Imani kwa Rais ni fadhila muhimu kwa amani na utulivu katika nchi yoyote. Lakini si kila nchi inapata fadhila hiyo,” alisema.

“Fadhila hiyo niliithibitisha zaidi wakati sehemu ya nchi yetu ilipovamiwa mkoani Kagera. Umoja wenu na vitendo vyenu kukabiliana na uvamizi vilinisaidia nikiwa Amiri Jeshi Mkuu.”

Licha ya uvamizi wa Kagera, Tanzania ilikumbana na matatizo kama kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukame na kushuka kwa bei za mazao hasa katika kipindi cha miaka sita, lakini Watanzania hawakuhamaki wala kutaka kuuza uhuru, alisema Nyerere.

“Tanzania imekuwa ikijenga jeuri ya kizalendo na kujivunia uhuru wake. Hatukujenga tabia ya kujikomba ili tukabiliane na matatizo yetu. Kutokana na Tanzania kutetea haki zaidi kwa upande wa nchi zinazoendelea,” alisema Nyerere.

“Wakati fulani nilishukuriwa na viongozi wengi wa nchi zinazoendelea baada ya kuzungumza Umoja wa Mataifa masuala ambayo yalikuwa yanazigusa nchi hizo. Hawakushukuru kwa ajili ya ufundi wangu wa kusema, bali kwa sababu nilikuwa nimesema nao maneno ambayo wao wasingeweza kuyasema.

“Sisi Tanzania tunasema ukweli japo juhudi za nchi zinazoendelea kutaka haki zaidi hazijafanikiwa, nchi nyingi zaidi zimeanza kuelewa.”

Mwalimu aliwachekesha wananchi na viongozi waliokuwapo ukumbini aliposema “hivi sasa si rahisi kuwatambua Wakristo na Waislamu kwa majina kwa sababu wapo Wakristo wenye majina ya Kiislamu na Waislamu wenye majina ya Kikristo”.

Aliwashukuru pia viongozi waliomsaidia kuongoza Serikali na hata mahali pengine kubeba lawama kutokana na kutekeleza uamuzi wake au kutokana na makosa yake.

Aliwashukuru pia wananchi kwa kumchagua Ali Hassan Mwinyi kuwa Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na akawataka kumsaidia.

Akabidhiwa sarafu maalum

Siku hiyo ukumbini hapo, Mwalimu Nyerere alikabidhiwa zawadi mbalimbali na wawakilishi wa mikoa yote, vikiwamo vifaa vya kilimo, vyakula, mifugo na magari.

Lakini alisema baadhi ya zawadi itabidi ziuzwe na fedha zake kuwekwa katika akaunti maalumu, nyingine zitakuwa katika sehemu maalumu ya kumbukumbu atakayojengewa na Serikali kijijini Butiama na nyingine atazitumia pamoja na Mama Maria.

Hata hivyo, alisema anaamini pia Watanzania wasingependa Rais wao wa kwanza awe tajiri ghafla.

Kesho tutaangazia jinsi Mwinyi alivyoapishwa na kuunda baraza la mawaziri pamoja na Mwalimu Nyerere alivyoondoka Ikulu ya Dar es Salaam kurudi kijijini kwake Butiama Mkoa wa Mara.