Ndege ya Tanzania iliyoshikiliwa Canada yatua Mwanza

Saturday December 14 2019

 

By Peter Saramba, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Ndege mpya aina ya Bombardier Q-400 iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania imetua uwanja wa Mwanza nchini humo na kupokelewa na wananchi na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais John Mgufuli.

Viongozi wengine waliohudhuria mapokezi ya ndege hiyo iliyotua leo Jumamosi Desemba 14, 2019 saa 1 usiku kisha kupata heshima ya kumwagiwa maji ni pamoja na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri.

Ndege hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 78, kumi wakiwa wa daraja la biashara na wengine 68 daraja la kawaida.

Kuwasili kwa ndege kutoka nchini Canada ilikotengenezwa kunafanya idadi ya ndege mpya zilizonunuliwa na Serikali katika jitihada za kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kufikia nane.

Tangu iingie madarakani Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli Novemba 5, 2015 inatekeleza mradi wa kufufua ATCL ambapo imepanga kununua ndege mpya 11 za aina na ukubwa tofauti.

Ndege zingine tatu zilizosalia zinatarajiwa kuwasili nchini kwa nyakati tofauti mwaka 2020.

Advertisement

Ndege mpya imewasili baada ya kuachiwa kutoka nchini Canada ilikoshikiliwa kutokana na deni la mkulima Hermanus Steyn, raia wa Afrika Kusini ambaye alifungua kesi ya madai Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini akidai fidia ya dola 33 milioni.

Hii ni mara ya pili kwa Steyn kushikilia ndege za Tanzania baada ya kufanya hivyo kwa kuizuia ndege ya Tanzania aina ya Airbus A220-300 kuondoka nchini Afrika Kusini Agosti, 2019.

Serikali ya Tanzania kupitia kwa wanasheria wake ilifanikiwa kushinda hoja mahakamani na kufanikiwa kuikomboa ndege hiyo iliyokuwa ikishikiliwa katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo Septemba 3, 2019.

Mkulima huyo anadai fidia baada ya Serikali ya Tanzania kutaifisha mali zake mwaka 1980.

Advertisement