OPERESHENI ENTEBBE DAKIKA 90: Ndege za kivita zaanza safari kutoka Tel Aviv kwenda Entebbe-6

Meneja wa Shirika la Ndege la Israel (El Al) katika ofisi za shirika hilo za mjini Nairobi aliambiwa ahakikishe ameandaa mafuta ya kutosha kwa ajili ya ndege za kijeshi za Israel ambazo zingejaza mafuta hayo zikiwa njiani kutokea Entebbe mara baada ya mashambulizi.

Kwa kuwa ndege walizotumia ni za kijeshi na za abiria, Waziri Mkuu Yitzhak Rabin aliwaza kuwa zile za kiraia kama Boeing 707 zingeweza kujaza mafuta mjini Nairobi kabla ya kwenda Uganda, lakini zile za kijeshi zikijaza kabla ya shambulio zingefanya watu wajiulize maswali mengi na hivyo kuathiri mpango wote. Hatimaye ikaonekana shambulio lifanyike kwanza ndipo ndege zijazwe mafuta wakati zikitoka Entebbe. Wazo la kujaza ndege mafuta zikiwa angani lilipingwa kutokana na hofu kwamba zingeonekana kwenye rada za nchi mahasimu wa Israel.

Mchana wa Jumamosi, hata kabla hajajua sawasawa matatizo ya kisiasa na ya kidiplomasia ambayo yangesababishwa na operesheni ya kuivamia Uganda, huku akiwa hajatoa idhini ya mwisho ya kushambulia, Waziri Mkuu alimuuliza tena mnadhimu mkuu wa Jeshi la Israel (IDF), Luteni Jenerali Mordechai “Motta” Gur; kamanda wa jeshi la anga (IAF), Benny Peled na washauri wake wa masuala ya kijasusi kama kuna njia nyingine yoyote ya kuzijaza mafuta ndege hizo katikati ya safari.

Lakini wakati wakijadili hilo wakapata habari ‘njema’ kutoka Nairobi kuwa hakukuwa na kipingamizi cha kujaza mafuta. Ili kuwa na uhakika zaidi, iliamuliwa kuwa ndege moja ya kivita ibebe mafuta na itangulie Kenya ikatue kwenye uwanja wa ndege za jeshi la Kenya karibu na Mombasa kwa sababu kama ndege ya Jeshi la Israel ikionekana imetua kwenye Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta kungezusha maswali mengi.

Majasusi wa Israel walichunguza na kupata ratiba za ndege zote ambazo zingetua kwenye Uwanja wa Entebbe kwa siku hiyo ya shambulio. Waligundua kuwa ndege ya Shirika la Ndege la Uingereza ingetua saa 8:30 usiku wa kuamkia Jumapili na kisha iondoke kwenda Mauritius. Hii iliwalazimu makomandoo wa Israel wafikirie kufanya shambulio lao na kuondoka eneo hilo kabla ya kutua kwa ndege hiyo.

Ndege ambazo zingetumika katika operesheni hii ni aina ya Hercules. Ndege hizi zilikuwa zinatumiwa na IAF tangu mwaka 1971. Mmoja wa wanajeshi wa IAF ambao walitumia ndege hizo ni Ariel Sharon ambaye baadaye alikuja kuwa Waziri Mkuu wa 11 wa Israel. Mojawapo ya ndege hizo ilibeba tani 20 za mafuta kwenda Kenya kwa ajili ya ndege ambazo zingeivamia Entebbe.

Ndege nyingine zilizotumika ni Boeing 707 ambazo zilikuwa mbili. Hizi zilibeba madaktari na maofisa wengine. Hata hivyo hizi Boeing zilitua Nairobi zikingoja zile za kijeshi zilizokwenda kushambulia Entebbe.

Majira ya jioni ya Jumamosi ya Julai 3 makomandoo wa Israel wa kikosi cha uvamizi walikusanyika kwa siri kupewa amri ya mwisho. Luteni Kanali Yehonatan “Yonni” Netanyahu ambaye alikuwa kamanda wa kikosi cha kushambulia aliipitia kwa mara ya mwisho ramani ya Uwanja wa Ndege wa Entebbe, hususan eneo ambalo mateka walikuwa wanashikiliwa.

“Tatizo ninaloliona,” alisema Yehonathan (Yonathan au Jonathan), “ni namna ya kuwafikia mateka kwa kasi ya hali ya juu sana na kuwaangamiza watekaji. Ni suala la sekunde chache tu kati ya kufanikiwa na kushindwa.”

Akichangia maoni ya Jonathan, ofisa mmoja wa Jeshi la Israel alisema “Hii inanikumbusha uokoaji wa Sabena kule Lod (Kusini mwa Tel Aviv). Kulikuwa na shida ya kuchambua kati ya wateka nyara na abiria wa kawaida. Abiria wengi waliokolewa kwa sababu jambo hilo lilichukua sekunde chache.”

Jonathan akamjibu, “Ndio maana una vitambulisho vya magaidi … Umepata wakati wa kuvikariri. Hawa washenzi hawapaswi wapate hata nukta ya kufyatua risasi hata moja. Bomu moja tu la kurushwa kwa mkono linaweza kumaanisha maafa makubwa sana kwetu. Muda ni jambo muhimu sana.”

Waandishi wawili, Mitchell Geoffrey Bard na Moshe Schwartz katika ukurasa wa 135 wa kitabu chao ‘1001 Facts Everyone Should Know About Israel’, wameandika kuwa ndege ya Sabena ilitekwa na magaidi wa Palestina Jumatatu ya Mei 8, 1972 ikiwa njiani kutoka Brussels kwenda Tel Aviv. Madai ya watekaji hao ni kuachiwa kwa mamia ya wafungwa wa PLO waliokuwa wakishikiliwa na Israel. Katika kuwaokoa mateka wa ndege hiyo, makomandoo wa Israel walitoboa na kumwaga mafuta ya ndege na kutoa upepo wa matairi kisha wakaingia katika ndege hiyo wakijifanya ni mafundi wa ndege. Katika uokozi huo magaidi wawili na abiria mmoja waliuawa. Walioongoza uokozi huo ni Benjamin Netanyahu na Ehud Barak—baadaye wote wawili walikuja kuwa mawaziri wakuu wa Israel katika vipindi tofauti.

Ingawa walikuwa wanajiandaa kwa shambulio dhidi ya nchi nyingine ambayo iko umbali wa maelfu ya kilomita, makomandoo hao walionekana kama wako kwenye burudani na walikuwa wakiizungumza Entebbe kana kwamba iko mtaa wa pili kutoka walipokuwa. Ilionekana kama vile walisahau operesheni yao ni ya nchi iliyoko Bara la Afrika na si Israel kwenyewe. Walianza kutaniana kuwa umbali ni tatizo la rubani na si la wapiganaji.

Baadaye wakaanza kuwazungumza mateka. Wakasema huenda kungetokea mapambano makali ya silaha kati yao na watekaji wakisaidiwa na polisi na wanajeshi wa Uganda. Miongoni mwa maswali waliyoulizana ni namna ya kuwaonya watekaji walale chini. Je, watatumia kipaza sauti? Au watavamia tu na kuanza kupiga kelele? Watawezaje kuwahamisha mateka kutoka waliposhikiliwa hadi kwenye ndege? Zitahitajika machela ngapi? Vipi kuhusu wazee na watoto? Watabebwa au wataweza kutembea wenyewe kwa haraka?

Mjadala wa mwisho uliwahusisha kamanda wa IAF, Jenerali Benny Peled, na mkuu wa tawi la operesheni, Meja Jenerali Yekutiel Adam. Michango yao katika mjadala ilikuwa ya kisayansi. Hapa ndipo walipopanga namna ndege zingekwenda Entebbe na kurudi. Zingeondoka muda gani kutoka Tel Aviv na zingewasili Entebbe muda gani. Wangefanya nini ikiwa kungetokea chochote kisichotazamiwa katikati ya safari yao mbali na makwao.

Kamanda mkuu wa operesheni hiyo, Brigedia Jenerali Dan Shomron, ambaye alikuwa amefanya kazi karibu saa 24 kila siku kwa karibu juma lote la wakati wa utekaji huo alianza kuwapanga watu wake.

Kikosi cha Jonathan Netanyahu kilipangiwa kazi ya kuvamia jengo walimoshikiliwa mateka na kuwaokoa bila kumbakiza hata mmoja. Kikosi 629 kingekabiliana na mashambulizi yoyote kutoka kwa majeshi ya Uganda. Kikosi Maalumu cha Anga kilikuwa na makomandoo ambao kazi yao ni kuteketeza ndege za Idi Amin, kulinda ndege za Israel, kufanya mawasiliano na madaktari na wauguzi na wataalamu wa miundombinu.

Jambo moja lilikuwa dhahiri kwao. Iwapo ndege za Israel zingeshambuliwa zikiwa Entebbe, makomandoo wa Israel wangekwama Uganda na hali zao zingekuwa mbaya zaidi kuliko hata za wale mateka. Kwa sababu hii peke yake walipanga kuwe na msaada maalumu wa ndege za akiba iwapo hali hiyo itatokea.

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Shimon Peres aliita operesheni hii kuwa ni ya “masafa marefu zaidi, itakayotumia muda mfupi zaidi, kwa ujasiri mkubwa zaidi, na kwa fikra kali zaidi.” Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Israel (IDF), Luteni Jenerali Mordechai Gur, aliitaja operesheni hii kama “hatari iliyozingatiwa” katika vita dhidi ya ugaidi.

Bila idhini ya Waziri Mkuu Yitzhak Rabin, ndege zisingeondoka Israel. Aliitisha kikao cha dharura cha baraza la mawaziri na kuwaeleza. Kikao hicho kilianza saa nane kamili mchana. Kilipomalizika hatimaye, idhini ya kuivamia Uganda ikatolewa dakika 15 baadaye.

Saa 9:30 alasiri marubani wa ndege zile, wakiwa tayari kwenye vyumba vyao vya rubani, wakasikia neno “Zanek!” likimaanisha “Ruka”. Ndege zikaanza safari ya kuelekea Entebbe, Uganda kwa kazi maalumu.

Itaendelea kesho