Ombi la walemavu wasioona lazaa matunda NEC

Muktasari:

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wasioona mkoani Tabora, waliweka azimio kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iandae utaratibu utakaowawezesha kupiga kura bila msaada wa mtu mwingine kwa kutumia alama zao.

Kila ifikapo siku ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu nchini, Watanzania wenye ulemavu wa kuona, husaidiwa na ndugu na jamaa zao kutekeleza haki hiyo.

Na wengine husaidiwa na mtu yeyote amkutae kituoni. Hali hiyo ilikuwa ikiwaumiza na wakati mwingine walikuwa hawajui kama kweli haki yao ya kumchagua kiongozi amtakaye ilikuwa ikitimia.

Huenda wengi wao walikuwa hawawachagui viongozi wawawatakao kwa sababu yule msaidizi wake alikuwa na uwezo wa kutumia mwanya huo kutekeleza mapenzi yake binafsi badala ya huyu anayemsaidia.

Kutokana na uwezekano wa kudanganywa na watu wanaowasadia au kutokuwa na usiri kwa mtu wanayetaka kumpigia kura, wasioona mkoani Tabora, walitaka kuwe na lengo au mkakati wa kuwawezesha kupiga kura wenyewe pasipo kusaidiwa na mtu, lengo likiwa ni pamoja na kutunza usiri kwa mtu wanayempigia kura.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wasioona mkoani Tabora, waliweka azimio kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iandae utaratibu utakaowawezesha kupiga kura bila msaada wa mtu mwingine kwa kutumia alama zao.

Azimio au mkakati huo safari hii katika uchaguzi, umezaa matunda baada ya NEC kuwawezesha kupiga kura pasipo kupata usaidizi wa mtu hivyo kutunza hata usiri wa mtu wanayemchagua.

Tume hiyo imetoa mafunzo kwa wasioona katika mikoa sita nchini ukiwamo wa Tabora ambao wasioona wapatao 50 wamepata mafunzo ya siku moja ya namna ya kutumia kifaa maalumu cha kupigia kura ambacho kitawasaidia kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Makilishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Hadija Twaha alisema NEC imekuwa na dhamira njema ya kuwasaidia wasioona nchini na ndio maana imeamua kutoa mafunzo kwa wasioona ingawa ni wachache ndio wanapata mafunzo hayo.

Hadija mwenye ulemavu wa kutoona ambaye pia ni Mweka Hazina wa Chama wa Wasioona (TLB), anasema walikuwa na lengo la kutoa mafunzo kwa wasioona wengi nchini lakini imekuwa sio rahisi kutokana na changamoto za muda, vifaa na rasilimali fedha.

Anasema waliomba mafunzo hayo yatolewe kwa wasioona nchi nzima lakini imeshindikana na sasa yametolewa kwa mikoa sita pekee tena kwa watu wapatao jumla mia mbili na hamsini.

“Pamoja na changamoto hizo, hata hivyo bado tunashukuru kwa hiki kidogo tulichopata kwa kuwa kitatusaidia na kuwa chachu kwa waliopata mafunzo na hata wale wasiopata mafunzo kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi itakapofika,” anasema.

Hadija aliyesimamia na kuwezesha mafunzo mkoani Tabora, anasema amefurahi kwamba yamekuwa na tija kwa wasioona kwa sababu yamekuwa na msaada mkubwa kwao huku wengi wakiahidi kutumia haki yao ya kikatiba kwenda kuwachagua wanaowataka Oktoba 28.

Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Tabora, Bosco Ndunguru anasema ni fursa muhimu kwa wasioona kufanya uamuzi wao pasipo kuingiliwa au kushawishiwa na mtu au kikundi cha watu.

Anasema wameweka mazingira mazuri kwao ili wapewe kipaumbele pindi wanapokwenda kupiga kura na kwa vile wamepata mafunzo, itakuwa rahisi kwao kupiga kura kwa urahisi na kuendelea na shughuli zao.

Ndunguru ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, aliyeyafungua mafunzo hayo anasema kwa kuwa wapo wengine ambao hawakupata mafunzo, watatumia mkakati wao wa kuwapa kipaumbele kupiga kura huku wale wanaotaka kusaidiwa, wakiruhusiwa pasipo kuwekewa masharti yoyote.

“Sisi kwetu hatuna tatizo na wasioona, uwe umepata mafunzo au hujapata, utasaidiwa na kuruhusiwa kuwatumia watu unaowataka kuwasaidia katika kupiga kura,” anasema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Tabora, Mariam Mathias anasema fursa waliyopata wasioona ya kupewa mafunzo ya kutumia kifaa maalum cha kupigia kura, yatawasaidia kuondokana na lawama za kuchagua wagombea kwa kujulikana.

“Tulikuwa tukijulikana ni kina nani tumewachagua (wagombea)jambo ambalo limekuwa wakati mwingine likitupa matatizo,” anasema.

Mariam anabainisha kwamba mwaka 2015, waliweka azimio kuwa mwaka huu uwe wa mageuzi kwa kupiga kura wao binafsi bila kusaidiwa, jambo ambalo limezaa matunda.

Mshauri wa wasioona mkoani Tabora na mchambuzi wa masuala ya watu wenye ulemavu, Donatus Rupoli amesifu mpango wa wasioona kupiga kura pasipo kutumia usaidizi kwa sababu unawasidia kutunza siri ya kura yake.

Rupoli ambaye naye ni mlemavu wa macho, anasema jambo la kupiga kura ni siri na haitakiwi mtu mwingine ajue mwenzake kampigia nani kura, lakini kifaa hicho ni mkombozi kwao kwa sasa.

Anaomba jitihada zaidi ziongezwe ili katika chaguzi zinazofuata, wasioona wote waweze kutumia kifaa hicho kupigia kura na wao wawe na siri za wanaowachagua.

“Kama tukipiga kura pasipo kujulikana, tutakuwa sawa na wenzetu wanaoona ambao wanapiga pasipo kuwa na wasiwasi kwa vile hawajulikani ni nani wamempigia,” anasema.

Yassin Issa aliyeshiriki mafunzo hayo, anasema yamekuwa na msaada mkubwa na watayatumia kwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura kuwachagua wanaowataka kuongoza.

Rashid Ngereza, anasema amefurahia mafunzo waliyoyapata na ni fursa nzuri kwao kupiga kura.

“Mimi nilikuwa nasita kupiga kura kwa kuhofia usalama wangu baada ya kupiga kura kwa kuwa hakukuwa na usiri jambo lililoniogopesha lakini kwa kifaa hiki sina hofu tena,”anasema

Mwenyekiti wa shirikisho la watu wenye ulemavu Amos Masudi anasema huo ni mwanzo mzuri na wanapenda jitihada zaidi ziongezwe ili wengi zaidi safari ijayo washiriki upigaji kura.

Anawataka wasioona akiwemo yeye mwenyewe,kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya kidemokrasia kuwachagua watu wanaowaona wanafaa kuongoza katika nafasi za udiwani, ubunge na urais.

Katika mafunzo hayo, wasioona, walionyeshwa namna ya kutumia kifaa hicho kupiga kura huku wakitumia karatasi za kura za mfano ambazo tayari zimewasili Mkoani Tabora.

Kutokana na baadhi kupata mafunzo hayo yaliyotolewa na NEC,wasioona sasa hawana sababu tena ya kubaki nyuma katika upigaji kura bali watashiriki kwa vitendo kuwachagua viongozi wanaowataka kuwaongoza.