Picha kamili ya kesi inayomkabili Harry Kitilya na wenzake

Kamishna Mkuu wa wa zamani wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Harry Kitilya na wenzake  Shose Sinare na Sioi Solomoni wakiwa katika mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam jana wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu. Picha na Said Khamis

Dar es Salaam. Wakati kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Kamishna Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanne, ikitarajiwa kuanza kuunguruma kuanzia leo, Mwananchi linakuletea muhtasari wa picha kamili ya mashtaka yanayowakabili hatua kwa hatua.

Kesi hiyo namba 01 ya mwaka 2019 inatarajiwa kuanza kuunguruma katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Ufisadi, mbele ya Jaji Imaculate Banzi.

Hii ni hatua ya usikilizwaji kamili ambapo mahakama itaanza kupokea ushahidi kutoka kwa mashahidi wa upande wa mashtaka, watakaoitwa kuthibitisha mashtaka yanayowakabili washtakiwa, kabla ya washtakiwa kujitetea na kisha kusubiri hukumu ya mahakama.

Mbali na Kitilya, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mshindi wa Mashindano ya Urembo (Miss Tanzania), mwaka 1996, Shose Sinare, Sioi Solomon, Bedason Shallanda na Alfred Misana.

Washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 58. Kitilya peke yake anakabiliwa na mashtaka 43 yote ya utakatishaji fedha, Shose mashtaka tisa, matano ya utakatishaji fedha, mawili ya kughushi na mawili ya kuwasilisha nyaraka za uwongo.

Mengine ni shtaka la kuongoza uhalifu, la kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu Dola za Marekani 6 milioni, utakatishaji fedha Dola 6 milioni na shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara ya cha Dola 6 milioni yanawakabili washtakiwa wote.

Pia, kuna shtaka lingine la kughushi kwa Kitilya, Shose na Sioi na shtaka moja la kutumia nyaraka za uwongo kumdanganya mwajiri, linalowakabili Shallanda na Misana.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato wa kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya Uingereza.

Walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza April Mosi, 2016, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu, kwa ajili ya kukamilisha taratibu za awali ikiwamo kukamilisha upelelezi, wakikabiliwa na mashtaka manane.

Hata hivyo Januari 11, 2019 baada ya upelelezi kukamilika, walifutiwa mashtaka ya awali, kisha wakasomewa mashtaka mapya 58.

Februari 12, 2019, walisomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo vya ushahidi vitakavyotumiwa na upande wa mashtaka kisha jalada la kesi hiyo likafungwa rasmi mahakamani hapo siku hiyo, na ikahamishiwa Mahakama ya Ufisadi, kwa ajili ya usikilizwaji kamili.

Machi 13, kesi hiyo ilisikilizwa katika hatua ya awali katika Mahakama ya Ufisadi, ambapo washtakiwa walisomewa upya mashtaka yao, walitakiwa kuyajibu kwa mara ya kwanza kwa ama kukubali au kukana. Wote walikana mashtaka hayo. Kisha walisomewa maelezo ya awali ambayo ni muhtasari wa kesi nzima.

Muhtasari huo wa kesi ndio unaotoa picha kamili ya kesi nzima, ukibainisha mpango unaodaiwa kufanywa na washtakiwa hatua kwa hatua kufanikisha kile kinachodaiwa na upande wa mashtaka, kujipatia kiasi hicho cha Dola 6 milioni (zaidi ya Sh13 bilioni kwa sasa).

Wasifu wa washtakiwa kiutumishi

Ili kupata picha kamili ya tuhuma dhidi yao ni vyema kwanza kuwafahamu washtakiwa hao na nafasi zao za utumishi katika taasisi walizokuwa wakifanyia kazi na namna zinavyohusiana na tuhuma hizo.

Kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashtaka, Kitilya, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na ambaye kuanzia mwaka 2003 mpaka mwaka 2013 alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), ni mkurugenzi wa kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors Limited (Egma).

Kampuni hiyo ilianzishwa Oktoba 2011 ikijihusisha na shughuli za ushauri wa uwekezaji, huduma za uwezeshaji na upatikanaji wa fedha.

Mshtakiwa wa pili, Shose, katika kipindi cha mwaka 2011 mpaka 2013 alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa na Uwekezaji, huku mshtakiwa wa tatu, Sioi akiwa Mkuu wa Idara ya Sheria na Katibu wa Bodi ya Stanbic Bank Tanzania Ltd.

Mshtakiwa wa nne, Shallanda na wa tano, Missana walikuwa watumishi wa Wizara ya Fedha. Shallanda alikuwa Kamishna wa Uchambuzi wa Sera na Missana alikuwa Kamishna Msaidizi wa Usimamizi wa Madeni, katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2013.

Pia wote wawili walikuwa viongozi wa kamati mbili ndani ya wizara hiyo zinazohusiana na masuala ya madeni, ambazo ni Kamati ya Kitaalamu ya Usimamizi wa Madeni (TDMC) na Kamati ya Usimamizi wa Deni la Taifa (NDMC).

TDMC hutoa ushauri wa kitaalamu kwa NDMC kuhusu masuala ya madeni na ukopaji wa ndani na nje na NDMC ni chombo cha kumshauri Waziri wa Fedha, kuhusu masuala yote yanayohusiana na madeni na ukopaji wa ndani na nje.

Shallanda alikuwa mwenyekiti wa TDMC na pia katibu wa NDMC, wakati Missana alikuwa Katibu wa TDMC na mjumbe wa sekretarieti ya NDMC.

Mambo yalivyoanza

Katika mwaka wa fedha 2011/2012, Serikali ya Tanzania ilihitaji kupata mkopo wa fedha kwa ajili ya kuendesha miradi iliyokuwa ikiendelea.

Kutokana na hitaji hilo taasisi mbalimbali za kifedha, ziliwasilisha maandiko ya mapendekezo serikalini kupitia Wizara ya Fedha, namna ambavyo zingeweza kuisaidia Serikali kupata kiasi cha fedha kilichokuwa kikihitajika.

Standard Bank PLC London (Standard Bank) na Stanbic Bank Tanzania Ltd (Stanbic Bank) zilikuwa ni miongoni mwa taasisi zilizowasilisha mapendekezo hayo.

Stanbic Tanzania Ltd ni kampuni dada ya Standard Bank PLC London, ambazo ni benki tanzu za Standard Bank Group Ltd ambayo ni kampuni inayomilikiwa na kusajiliwa nchini Afrika Kusini.

Oktoba 2011, Standard Bank katika pendekezo lake la kwanza ilipendekeza kuwa ingewezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekani 300 milioni.

Katika pendekezo lake la pili ikishirikiana na Stanbic Tanzania Ltd, zilipendekeza kuwa zingeiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni kwa ada ya asilimia 1.4 ya kiasi cha mkopo ambao ungepatikana. Hata hivyo mapendekezo yote hayo hayakufanikiwa.

Kwa mujibu wa maelezo hayo ya awali, baada ya hatua hiyo kushindikana, inadaiwa kuwa ndipo washtakiwa hao katika kipindi cha kuanzia Februari 2012 mpaka Juni 2015, walipopanga uhalifu ulioisababishia hasara Serikali ya Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Juni 22, 2012, kwa mara nyingine tena, Stanbic Bank kwa kushirikiana na Standard Bank, ziliwasilisha pendekezo la uwezeshaji wa kifedha kwa Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013.

Katika pendekezo hilo zilipendekeza kuwa zingeiwezesha Serikali kupata Dola za Marekani 550 milioni kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 1.4 ya kiasi cha mkopo husika.

Hata hivyo, kabla ya kamati ya wataalamu (TDMC) haijakaa kujadili pendekezo hilo, Agosti 2, 2012, Shose inadaiwa aliandaa pendekezo lingine la ongezeko la ada ya uwezeshaji wa asilimia moja, kutoka asilimia 1.4 hadi 2.4, ambalo liliwasilishwa Wizara ya Fedha Agosti 6, 2013.

Pendekezo hilo lilikusudia kuonyesha kuwa limeandaliwa kwa pamoja na Standard Bank na Stanbic Bank.

TDMC ilipokaa Agosti 24, 2012 kujadili mapendekezo yaliyowasilishwa na benki mbalimbali likiwamo hilo la Standard na Stanbic, Shallanda na Misana waliwasilisha pendekezo la awali, halisi la mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni, kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 1.4.

Hivyo TDMC ilipendekeza iundwe timu ya majadiliano ya Serikali kupitia na kujadiliana kuhusu hilo.

Timu ya majadiliano ya Serikali, ilipokaa Septemba 11, 2012 kupitia na kujadili pendekezo la Standard Bank na Stanbic Bank, inadaiwa Shallanda na Misana mara hii waliwasilisha pendekezo la pili la kughushi lenye ongezeko la asilimia moja ya ada ya uwezeshaji, yaani asilimia 2.4.

Septemba 17, 2012, siku moja kabla ya kikao cha TDMC inadaiwa Shose aliandaa na kuwasilisha barua ya kimamlaka ya uwongo, kuhusiana na pendekezo la uwezeshaji mkopo huo wa Dola 550 milioni.

Barua hiyo ililenga kuonyesha kwamba Stanbic Bank kwa kushirikiana na Standard Bank zingeiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola 550 milioni kwa ada ya asilimia 2.4 ya kiasi cha mkopo, ikiwa na ongezeko la udanganyifu la asilimia moja ya ada ya uwezeshaji.

Pendekezo hilo liliwasilishwa katika Wizara ya Fedha siku hiyohiyo Septemba 17, 2012.

TDMC ilipokaa tena Septemba 18, 2012, kupokea mrejesho wa timu ya majadiliano ya Serikali, siku moja baada Shose kuwasilisha barua hiyo ya kimamlaka ya kughushi, ndipo ilipoelekeza kwamba Stanbic Bank pamoja na Standard Bank ziombwe kuwasilisha barua ya kimamlaka.

Baadaye Septemba 19, 2012, Shallanda na Misana waliwasilisha katika kikao cha NDMC pendekezo la Standard na Stanbic Bank, lenye ada ya uwezeshaji la kughushi la asilimia 2.4.

NDMC ikafanyia kazi taarifa hizo za uwongo, ilipendekeza kwa Waziri wa Fedha kuidhinisha hilo la Standard Bank na Stanbic Bank la uwezeshaji wa mkopo wa Dola 550 milioni kwa ada ya kughushi ya asilimia 2.4.

Pendekezo hilo liliidhinishwa na Waziri wa Fedha Septemba 25, 2012 ambapo benki hizo ziliombwa barua ya kimamlaka ili liweze kufanyiwa kazi na Serikali.

Barua hiyo hatimaye ilisainiwa Novemba 15, 2012 baada ya kuwa imejadiliwa na kufanyiwa mashauriano.

Masharti ya barua hiyo ya kimamlaka, mkopo huo ulihusu mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni tu kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4.

Hata hivyo Machi 2013, barua hiyo iliendelezwa na kuhusisha nyongeza ya Dola za Marekani 50 milioni na hivyo mkopo huo kufikia Dola za Marekani 600 milioni.

Mgawo wanaodaiwa kujipatia

Ili kuwezesha ulipaji wa asilimia moja iliyoongezwa katika ada ya uwezeshaji upatikanaji mkopo huo kwa kampuni ya Egma, inadaiwa Kitilya, Shose na Sioi waliandaa makubaliano ya uwongo ya ushirikiano.

Makubaliano hayo yalikusudia kuonyesha kwamba Stanbic Bank ilianzisha ubia wa kushirikiana na Egma, katika mipango ya kuwezesha Serikali katika upatikanaji mkopo wa Dola 550 milioni.

Mkataba wa makubaliano hayo ambao unadaiwa kuandaliwa na Sioi Septemba 21, 2012, uliendelezwa zaidi na Kitilya na Shose na hatimaye ulisainiwa Januari 2013, lakini ulirejeshwa tarehe nyuma kuonekana kwamba ulisainiwa Novemba 5, 2012.

Ilikusudiwa katika makubaliano hayo kuonyesha kwamba Egma ilifanya mipango ya majadiliano na kuandaa mkutano ikihusisha kugharamia, kuwezesha ufahamu wa masuala ya kitaalamu katika uwezeshaji wa mikopo kwa Serikali, kushughulikia nyaraka mbalimbali zilizokuwa zikihitajika katika mamlaka husika nchini Tanzania.

Kufuatia ubia huo uliokusudiwa baina ya Stanbic na Egma, ilikuwa ni sharti kwamba Egma ilipwe ada ya uwezeshaji ya asilimia moja ya kiasi cha mkopo husika.

Februari 2013, Standard Bank PLC iliiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola 600 milioni katika Soko la Mitaji la Kimataifa. Machi 8, 2013 mazao ya mkopo uliopatikana yalilipwa kwa Serikali baada ya nyaraka zote za mkopo kukamilika.

Machi 12, 2013 Serikali iliilipa Stanbic Bank Dola za Marekani 14,400,000, ikiwa ni ada ya asilimia 2.4 ya uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo huo kwa kiasi cha mkopo uliopatikana (Dola 600 milioni).

Machi 15, 2013, Shose alihamisha Dola za Marekani 6 milioni (sawa na asilimia moja ya ada ya uwezeshaji upatikanaji mkopo, waliyoiongeza kwa kughushi), kutoka akaunti ya Nostro Stanbic Bank, kwenda kwenye akaunti ya Egma.

Akaunti hiyo ya Egma ilifunguliwa Machi Mosi, 2013 kama akaunti ya makusanyo kwa lengo maalumu la kupokea ada ya makubaliano ya ushirikiano huo Egma na Stanbic) yaani ile asilimia moja wanayodaiwa kuiongeza.

Kabla ya kufunguliwa kwa akaunti hiyo, Egma ilikuwa na akaunti nyingine mbili katika benki ya Stanbic ambazo inadaiwa kwamba zilifunguliwa Septemba 2012.

Ingawa akaunti hiyo ya makusanyo ilifunguliwa na Egma, lakini watia saini hawakuwa na uwezo wa kutoa fedha bila idhini ya Shose.

Hivyo baada ya fedha hizo kuwa zimelipwa kwa udanganyifu katika akaunti hiyo kuanzia Machi 18, 2013, Shose aliidhinisha miamala mbalimbali na alielekeza uhamishwaji fedha kwa viwango tofauti na kwa nyakati tofati kuingia na kutoka katika akaunti hizo nyingine za EGMA ndani ya Stanbic.

Hivyo upande wa mashtaka unadai kuwa, kwa uovu wa kuongeza ada ya mkopo asilimia moja, kutoka asilimia 1.4 mpaka 2.4, kwa udanganyifu, washtakiwa walijipatia kwa udanganyifu Dola za Marekani 6 milioni (Sh13.4 bilioni) na kuisababishiia Serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.