Breaking News

Polisi wanasa kilo 150 za bangi Serengeti

Sunday October 18 2020

 

By Anthony Mayunga, Mwananchi

Serengeti. Jeshi la Polisi Wilaya ya Serengeti limekamata bangi kilo 150 ikiwa imefungwa ndani ya magunia mawili na kuwekwa nguo mfano wa robota la mitumba wakati mtuhumiwa akisubiri magari ya kwenda Bunda na Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Daniel Shillah aliliambia gazeti la Mwananchi kwa njia ya simu kuwa mtuhumiwa Kitende Magabe ambaye ni mkazi wa Bunda Mkoa wa Mwanza alikamatwa juzi saa 5 asubuhi.

“Alikwepa kupandia stendi, akaenda Shule ya Msingi Mapinduzi na mzigo wake, kwa kuwa askari walikuwa na taarifa walimfuatilia mtuhumiwa huyo na kumnasa na mzigo wake, kwa sasa anahojiwa ili kutusaidia kubaini mtandao wake, nitatoa taarifa zaidi baada ya kukamilisha uchunguzi,” alisema Kamanda Shillah.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mmoja wa boda boda jina limehifadhiwa mtuhumiwa aliingia na mzigo huo akidaiwa kutokea Wilaya ya Tarime.

“Mwaka jana mwingine naye alishuka na mzigo kutokea Tarime akapanda bodaboda hadi Serengeti sekondari akasubiria gari huko ili apeleke mzigo Mwanza ndipo akakamatwa,inaonekana wanakwepa vizuizi vya Polisi wa Kirumi wanaamia kukatizia huku,”alisema.

Mmoja wa askari ambaye hakutaka kuandikwa jina lake alisema mbinu mpya ya kusafirisha dawa za kulevya kwa kufunga kama mitumba wameishaibaini ndiyo maana ilikuwa rahisi kumkamata mtuhumiwa.

Advertisement

“Kwa mtu wa kawaida usingeweza kumtilia shaka mtuhumiwa kutokana na ulemavu wake lakini tumeishabaini kuwa wanatumika sana kusafirisha magendo,” alisema.

Advertisement