Queen aahidi kuipa kipaumbele sekta binafsi

Friday October 23 2020
queen pic

Singida. Mgombea urais wa Alliance for Democratic Change (ADC), Queen Sendiga amesema akichaguliwa kuunda Serikali, ataipa nafasi kubwa sekta binafsi katika shughuli za kujenga uchumi tofauti na ilivyo sasa.

Mgombea huyo amesema uchumi wa kisasa utakaotoa fursa kwa wananchi wengi zaidi unahitaji ushiriki wa kila mdau, hivyo Serikali yake itatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi kwa kuipa nafasi kubwa kwenye shughuli muhimu zitakazosaidia kuongeza mzunguko wa fedha, kutoa ajira hivyo kupunguza umasikini.

Hayo yote amesema yatawezekana kwa kuboresha urafiki kati ya Serikali na sekta binafsi, hivyo kusaidia kukuza uchumi wa ndani utakaowagusa wananchi.

“Kwa sasa kuna uadui kati ya Serikali na sekta binafsi, japokuwa wanacheka kwa nje ila ndani wana maumivu. Idadi ya kampuni zinazofunga biashara na kusababisha wimbi kubwa la vijana kurudi mtaani kwa kukosa ajira inazidi kuongezeka,” alisema Queen.

Mgombea huyo aliyemaliza ziara ya kuomba kura mkoani Singida kisha kuelekea Manyara alisema kinachotakiwa ni kubaini na kuainisha fursa za kutosha zilizopo katika kila mkoa zikiwemo za kilimo na nyingine zitakazotoa ajira nyingi na kuipa nafasi sekta binafsi kuzitumia ili vijana wanufaike.

Mgombea huyo wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema hayo alipohutubia na kuwaomba kura wananchi wa Singida Msufini katika viwanja vya Otu.

Advertisement

“Naomba mnichague Oktoba 28 mtakapoenda kupiga kura ili kwa pamoja tukakuze uchumi wa watu wetu na nchi kwa ujumla,” alisisitiza mgombea huyo.

Kuhusu ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kujenga uchumi wa nchi, baadhi ya wananchi wamesema iwapo vikwazo vya kufanya biashara vitaondolewa, mchango wake utakuwa mkubwa zaidi.

“Kuna changamoto kuanzia kwenye kurasimisha mpaka ulipaji kodi. Taratibu zilizopo hazimsaidii wala kumshawishi mfanyabiashara kuzifuata hivyo kuwanyima wengi fursa ya kukua. Watu hawapendi kuwa wamachinga ila sheria zilizopo zinawalazimisha,” alisema Richard Shillah mkazi wa Kindai mjini hapa.

Mkazi mwingine, Agness Francis alisema pamoja na taratibu za kuzingatiwa kuwa nyingi, bado ofisi zinazotoa huduma zipo Dar es Salaam hivyo kuongeza gharama hata kabla biashara husika haijaanzishwa.

“Huwezi kupata mkopo benki mpaka uwe na hati ya nyumba au kiwanja. Kuwa na nyumba au shamba sio tatizo ila kupata hati lazima jasho likutoke. Ni kazi kwelikweli. Utalazimika kusafiri huku na kama unaitaka kwa haraka na uwezo wa kulipia unao,” alisema mfanyabiashara huyo wa mafuta ya alizeti.

Advertisement