Serikali yamwekea kigingi mkulima anayehoji ukomo wa urais

Mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, Patrick Mgoya aliyefungua kesi ya kupinga ukomo wa urais akitoka Mahakama Kuu baada ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa kwa mara ya kwanza na majaji watatu mahakamani hapo jana. Picha na Ericky Boniphace

Dar es Salaam. Serikali imemuwekea kigingi mkulima Patrick Dezydelius Mgoya aliyefungua kesi ya kikatiba inayohoji ukomo wa kipindi cha urais wa Tanzania.

Mkulima huyo, mkazi wa Mbezi Beach Dar es Salaam, amewekewa pingamizi la awali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali anayeiomba mahakama iitupilie mbali kesi hiyo bila hata kuisikiliza.

Pingamizi la Serikali lilibainishwa na wakili Daniel Nyakiha jana kesi hiyo ilipotajwa mara ya kwanza mahakamani tangu ilipofunguliwa mwezi uliopita.

Mkulima huyo amefungua kesi hiyo Mahakama Kuu dhidi ya AG, akiiomba mahakama itoe tafsiri sahihi ya ibara ya Katiba inayoweka ukomo huo wa urais.

Kesi hiyo ilitajwa mara ya kwanza jana mbele ya majaji watatu wanaoongozwa na Jaji Kiongozi, Dk Eliezer Felesh. Majaji wengine ni Dk Benhajj Masoud na Seif Kulita.

Hata hivyo wakili, Nyakiha aliieleza mahakama kuwa wamewasilisha majibu yao na pingamizi la awali lenye hoja nane.

Miongoni mwa hoja za pingamizi, Serikali inadai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, na mwombaji hana mamlaka ya kufungua shauri hilo kwa kutumia vifungu namba 3,4,5 na 6 vya Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu. Pia Serikali inadai kuwa hati ya kiapo inayounga mkono shauri hilo ina kasoro za kisheria zisizoweza kurekebishika, hasa sehemu ya uthibitisho wa taarifa zilizomo.

Serikali pia inadai kuwa kiapo hicho kina dosari za kisheria zisizoweza kurekebishika kutokana na kukiuka Amri ya 19, Kanuni ya 3 ya Kanuni za Mwenendo wa Mashauri ya Madai, Sura ya 33, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Pia, Serikali inadai kuwa mwombaji hana haki ya kisheria kufungua kesi hiyo na kwamba nafuu anazoziomba mwombaji haziwezi kutolewa kwa kuwa zinakiuka kifungu cha 44 cha Sheria ya Mawakili, Sura ya 341, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kutokana na pingamizi hilo la awali, mkulima huyo ameiomba mahakama apewe siku saba kujibu hoja hizo za pingamizi la Serikali na mahakama imemkubalia maombi hayo na kumwamuru awasilishe majibu yake Septemba 24, au kabla ya tarehe hiyo na ikapanga kusikiliza pingamizi hilo la Serikali, Septemba 30, mwaka huu.

Kwa hiyo Mgoya anapaswa kupangua hoja hizo za Serikali ili kuvuka hatua hiyo na apate nafasi ya kusikilizwa hoja zake za kuhoji ukomo huo wa urais.

Mgoya amefungua kesi hiyo chini ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Utekelezaji Haki na Wajibu, Sura ya 3 ya mwaka 1994 na chini ya Ibara ya 30 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo namba 19 ya mwaka 2019, Mgoya anahoji Ibara ya 40 (2) ya Katiba inayoweka ukomo wa mihula miwili tu ya miaka mitano mitano (10) ya uongozi katika nafasi hiyo ya urais.

Hivyo anaiomba mahakama hiyo itoe tamko na tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya ibara hiyo.

Pia anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana dhahiri ya masharti ya Ibara ya 42(2) ya Katiba, kwa kuhusianisha na masharti ya Ibara za 13, 21 na 22 za Katiba hiyo.

Vilevile anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana ya Ibara hiyo ya 40 (2) kwa kuhusianisha na Ibara ya 39 ya Katiba.

Katika hati yake ya kiapo kinachounga mkono kesi hiyo, Mgoya anadai kuwa shauri hilo linatokana na kukinzana kwa ibara mbalimbali katika Katiba ya nchi, ambazo anazitaja kuwa ni Ibara ya 13, 21, 22(2), 39 na 40(2).

Anafafanua kuwa Ibara ya 13 inatoa usawa mbele ya sheria na kwamba hakuna sheria ambayo itatungwa na mamlaka yoyote nchini, kuweka sharti ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa tahthira yake.

Kuhusu Ibara ya 21 anaeleza kuwa inaweka haki na uhuru wa kushiriki kikamilifu kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake na au yanayolihusu Taifa.

Kwa Ibara ya 22 (2) anasema inaeleza kuwa kila raia anastahili fursa na haki sawa kwa masharti ya usawa, ya kushika nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyo chini ya Mamlaka ya Nchi.

Mgoya anabainisha kuwa ibara hizo zote 13, 21 na 22(2) zinapatikana katika sehemu ya Tatu ya Sura ya Kwanza ya Katiba, ambazo mtu yeyote anaweza kutafuta nafuu katika mahakama hiyo kuhusu ukiukwaji wake.

Anadai kuwa lakini Ibara ya 40(2) ya Katiba inaweka ukomo wa muda wa mtu kuchaguliwa kuwa rais, kwamba mtu hawezi kuchaguliwa zaidi ya mara mbili kushikilia wadhifa wa urais.

Hivyo anadai kuwa masharti ya ibara hiyo ya 40 (2) yanakiuka haki za kikatiba za Ibara za 13, 21 na 22(2) za Katiba hiyo hiyo kwa kutoa mihula miwili tu ya raia kuchaguliwa kuwa rais kwa ukomo wa miaka 10 tu.

Mgoya anadai kuwa ukomo uliowekwa chini ya Ibara ya 40 (2) ya Katiba yanakinzana na haki ya kikatiba ya uhuru wa kushiriki katika shughuli za umma kwa kuchagua au kuchaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na usawa mbele ya sheria chini ya Ibara ya 21 na 13.