Simu milioni 30 hatarini kuzimwa

Dar es Salaam. Takriban nusu ya laini milioni 44 za simu zinaweza kufungwa iwapo kasi ya utoaji vitambulisho vya Taifa haitaongezeka katika siku 49 kuanzia leo.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema itazizima laini hizo ifikapo Desemba 31 iwapo wamiliki watakuwa hawajajisajili kieletroniki kwa kutumia kitambulisho cha Taifa.

Hadi sasa zaidi ya laini milioni 30 hazijasajiliwa na mkurugenzi mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema zilizosajiliwa ni takriban milioni 13 kati ya takriban milioni 44 zinazotambuliwa na mamlaka hiyo.

Kutokana na kutokuwapo uwezekano wa kuongeza hata dakika moja, Kilaba alisema hamasa inapaswa kuwa kubwa ili wananchi wasishindwe kutekeleza majukumu yao.

“Tumetoa matangazo matatu kuwaelimisha wananchi zikiwa zimebaki siku chache kabla utekelezaji wa sheria haujafika,” alisema Kilaba.

“Tunafahamu changamoto ya vitambulisho vya Taifa iliyopo lakini kila mmoja anapaswa kuharakisha kupata namba (ya kitambulisho cha Taifa).”

Endapo Nida watatoa vitambulisho walau milioni 10, alisema huenda vikatosha kusajili idadi kubwa kwani wapo wengi wanaomiliki zaidi ya laini moja.

Changamoto zilizopo alisema si za watoa huduma, bali upatikanaji wa vitambulisho hivyo kwani kuna vifaa vya kutosha kusajili wateja wote wa simu za mkononi endapo watakuwa na kitambulisho.

Ili kuhakikisha hakuna anayeachwa kwenye mchakato huo, alisema huwa wanaenda hata minadani vijijini ili kusajili wananchi lakini wanakuta wengi hawana vitambulisho.

Hata hivyo, alisema katika laini zilizopo, inawezekana zipo baadhi ambazo zinatambulika kwa watoa huduma ila wahusika wakawa hawazitumii kabisa.

“Kitakachofanyika ni kuzima laini hizo Desemba 31 ili wachache watakaobaki waende kutafuta kitambulisho na kusajili laini walizonazo. Hiyo itatusaidia kujua laini hai na ambazo zinatumika ni ngapi nchini,” alisema.

Simu za mkononi ndizo zinazoibeba sekta ya fedha kwani kati ya asilimia 65 ya Watanzania wanaozitumia, asilimia 48 wanafanya hivyo kupitia simu za mkononi.

Taarifa ya TCRA kwa miezi sita iliyopita inaonyesha miamala ya zaidi ya Sh16 trilioni ilifanyika mpaka Juni. Mamlaka hiyo inasema kwa robo ya kwanza iliyoishia Machi 30, miamala milioni 243.52 iliyofanyika ilikuwa na thamani ya Sh7.82 trilioni huku miamala milioni 260.43 iliyofanyika kati ya Aprili na Juni ilikuwa ya Sh8.31 trilioni.

Akiwasilisha taarifa za fedha za nusu mwaka ulioishia Septemba, mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Vodacom, Hisham Hendi alisema M-pesa ni miongoni mwa huduma muhimu inayoiingizia mapato kampuni hiyo, lakini kuna changamoto.

“Tunaendelea kuwasajili wateja wetu kwa alama za vidole ili kutii sheria, lakini changamoto iliyopo ni gharama za kufanya hivyo pamoja na upatikanaji hafifu wa vitambulisho vya Taifa,” alisema Hendi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Huduma za M-pesa zilifanikisha miamala ya Sh29.1 trilioni ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 21.4 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana. Miamala hiyo iliingizia kampuni hiyo Sh182.02 bilioni.

Meneja uhusiano wa kampuni ya Airtel, Jackson Mmbando alisema kampuni zote za mawasiliano zinashirikiana na mamlaka husika kuhakikisha wateja wote wenye sifa wanasajiliwa kwa alama za vidole.

Kwa sasa, karibu ofisi zote za Nida hujaa wananchi wanaosaka vitambulisho hivyo ambavyo vimegeuka kuwa nyaraka muhimu inayotakiwa sehemu kadhaa kama utambulisho rasmi.

Kampuni za simu zimegawa ving’amuzi maalumu vya alama za vidole kwa mawakala wake ili kurahisiha usajili, lakini changamoto ni vitambulisho.