TPSF ‘waziba’ nafasi ya Shamte, Takukuru waendelea kumng’ang’ania

Dar/Tanga. Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imemteua Angelina Ngalula kuwa kaimu mwenyekiti wa taasisi hiyo wakati taratibu za kisheria zikiendelea kufanyika dhidi ya mwenyekiti wake, Salum Shamte anayeshikiliwa na polisi mkoani Tanga.

Wakati bodi ikieleza hayo, Takukuru na polisi jana wameeleza kuwa uchunguzi dhidi ya Shamte na wenzake umechukua muda mrefu, hivyo wanaendelea kumshikilia.

Shamte alikamatwa mkoani Tanga wiki iliyopita kwa tuhuma za kuhusika kwenye upotevu wa Sh54 bilioni zikiwemo fedha za Serikali kupitia kampuni ya Katani Limited ambayo inadaiwa ana maslahi nayo.

Wengine waliokamatwa naye ni mkurugenzi wa kampuni ya Katani Ltd, Juma Shamte, mkurugenzi wa fedha, Fadhili Malima, ofisa uhusiano wa umma, Theodora Mtejeta na mjumbe wa bodi, Fatma Diwani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwenye vyombo vya habari na Ngalula, bodi ya wakurugenzi ilifanya kikao chake cha dharura Oktoba 23 na kuamua shughuli zote zitaendelea chini ya uongozi wa makamu mwenyekiti wakati taratibu za kisheria zikiendelea.

“TPSF inapenda kuwahakikishia wanachama wake, serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi kwa ujumla kwamba jambo hili halitakuwa na athari zozote katika utoaji wa huduma katika taasisi yetu.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 7, kifungu cha 5, kifungu kidogo (j) cha Katiba ya TPSF, makamu mwenyekiti wa sasa, Angelina Ngalula atakaimu nafasi ya mwenyekiti wakati wote ambao hayupo,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba TPSF kama taasisi ya juu imejizatiti katika kusukuma ajenda ya maendeleo ya sekta binafsi nchini. Shamte ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Biashara la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), alikamatwa kwa maelekezo ya mkuu wa mkoa wa Tanga, Martin Shigela.

Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Tanga, Christopher Mariba alisema Shamte pamoja na viongozi wengine wa kampuni ya Katani watafikishwa mahakamani wiki ijayo baada ya vyombo vya dola kukamilisha uchunguzi.

Alisema Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola bado vinaendelea na uchunguzi wa tuhuma zilizowasilishwa na mkaguzi wa hesabu kutoka Wizara ya Fedha ili kujiridhisha kabla ya kuwafikisha Mahakamani.

“Wapo watu mbalimbali waliotajwa kwenye ripoti ile, tunakwenda hatua kwa hatua, tukikamilisha tutawajulisha,” alisema Mariba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema kwa kuwa uchunguzi huo unahusisha vyombo mbalimbali imewachukua siku nyingi kuukamilisha.