Breaking News

Trump ainyima fedha WHO, dunia yamshukia

Thursday April 16 2020

 

By Mwandishi Wetu/AFP

Wakati wanasayansi duniani wakiharakisha kupatikana kwa chanjo ya ugonjwa hatari wa virusi vya corona, Rais wa Marekani, Donald Trump, ameamuru nchi yake isiipe fedha Shirika la Afya Duniani (WHO), akilituhumu kwa kushindwa kushughulikia janga hilo.

Hata hivyo, uamuzi wake, ambao umekuja wakati viongozi duniani wakifikiria kupunguza masharti ya kuzuia wananchi wao kutotoka ndani, umekosolewa na viongozi wengi.

Idadi ya waliofariki kwa corona duniani kote hadi jana jana mchana ilikuwa zaidi ya watu 125,000, huku zaidi ya watu milioni mbili wakiwa na maambukizi.

Viongozi duniani wanafikiria lini waondoe marufuku hiyo ya kutoka ndani ili kuanzisha kazi ya kufufua uchumi, lakini wakiepuka kurejea kwa mlipuko wa virusi vya corona.

Huku dunia ikipambana kuushinda ugonjwa huo, Trump ameiwashia moto WHO baada ya kuzuia malipo yaliyofikia Dola za Marekani 400 milioni (sawa na zaidi ya Sh800 bilioni) mwaka jana.

“Fedha hizo zitazuiwa kwa kusubiri kuangaliwa upya nafasi ya WHO kuwa ilishughulikia vibaya na kuficha taarifa za kusambaa kwa virusi vya corona,” alisema Trump na kulituhumu shirika hilo kwa kuweka mbele masuala ya kisiasa kuliko kuchukua hatua za kuokoa maisha ya wanadamu.

Advertisement

Aliongeza kusema: ‘‘Mlipuko ungeweza kudhibitiwa wakati kukiwa na vifo vichache kama WHO ingeweza kushughulikia kwa usahihi hali ilivyokuwa China ambako ugonjwa huo uliibukia.’’

Mashambulizi hayo yenye utata ya Trump yamekuja wakati Marekani ikiwa imefikisha idadi ya vifo 2,228 ndani ya saa 24, kwa mujibu wa takwimu za Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.

Lakini bado Trump ameahidi kuinua sehemu kubwa ya uchumi wa

taifa hilo kubwa duniani, akisema Marekani itafungua tena maeneo yake kadhaa, huku maeneo yaliyoathiriwa vibaya kama New York yakichukua muda mrefu kidogo.

Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) limeonyesha hatari ya uchumi kuyumba, likisema marufuku ya kutoka ndani inaweza kuondoa Dola za Marekani 9 trilioni katika uchumi wa dunia, ambao unaonekana kuelekea kuanguka kwa mara ya pili tangu miaka ya 1980.

Viongozi wamshambulia

Miongoni mwa watu waliomshambulia ni pamoja na tajiri maarufu duniani, Bill Gates ambaye aliandika katika akaunti yake ya Twitter kuwa kuzuia fedha “ni sauti ya hatari.”

Amelaumiwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas ambaye alionya dhidi ya kile alichokiita: ‘kulaumu wengine” kwa janga hilo.’

“Kulaumu wengine hakutasaidia. Virusi havijui mipaka,” Maas aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alipokea uamuzi huo wa Trump kwa mtazamo tofauti.

“Huu si wakati wa kupunguza rasilimali za uendeshaji wa shirika la afya la dunia au taasisi yoyote ile ya kibinadamu katika vita dhidi ya virusi vya corona,” alisema Guterres na kuongeza:

“Ni imani yangu kwamba Shirika la Afya Duniani lazima lisaidiwe kwa kuwa ni muhimu katika vita ya dunia ya kuishinda Covid-19.”

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Zhao Lijian alisema kuwa China imesikitishwa na tangazo la Marekani la kuzuia fedha kwa Shirika la Afya Duniani.

“Hali ya ugonjwa huu wa dunia ni hatari. Ni muda muhimu sana. Uamuzi huu wa Marekani utadhoofisha uwezo wa WHO na kudharau ushirikiano wa kimataifa katika kupambana na ugonjwa huu,’’ alisema.

Aliongeza:“Tunaishauri Marekani kutekeleza majukumu yake kwa dhati na kusaidia juhudi zinazoongozwa na WHO kupambana na ugonjwa huu.”

Advertisement