Uchaguzi mkuu wapaisha bajeti ofisi ya Waziri Mkuu 2020/2021

Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki (wa pili kulia) akimmiminia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi kitakata mikono kwa ajili ya kujilinda na maambukizi ya virusi vya corona, walipohudhuria kikao cha bunge, jijini Dodoma jana. Picha na Anthony Siame

Dodoma. Ofisi ya Waziri Mkuu imeomba kuidhinishwa Bajeti ya Sh312.8 bilioni kwa mwaka 2020/21 ikiwa ni ongezeko la Sh163.9 bilioni ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2019/20 ya Sh149 bilioni, ongezeko lililoelezwa na Kamati ya Bunge kuwa limechangiwa na gharama za uchaguzi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwasilisha bajeti hiyo bungeni Dodoma jana akitaja vipaumbele vya mpango wa maendeleo wa mwaka 2020/21 ambavyo vimejikita katika ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.

Majaliwa alisema pia bajeti hiyo imelenga uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mpango wa maendeleo.

Alisema katika kufikia malengo ya mpango, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika kutekeleza miradi ya kielelezo ya kimkakati pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), mradi wa kufua umeme wa MW 2,115 Rufiji, kuboresha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga.

Ongezeko la bajeti

Licha ya maelezo hayo, Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ilisema mabadiliko katika bajeti ya maendeleo ya ofisi hiyo, pamoja na sababu nyingine yanatokana na kuongezeka kwa bajeti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, lengo likiwa ni kuiwezesha menejimenti ya uchaguzi kutekeleza majukumu yanayoikabili mwaka huu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa alisema, “mpango wa ofisi ya Waziri Mkuu katika miradi ya maendeleo katika mwaka huu umebaini kuwa bajeti ya maendeleo inayoombwa imeongezeka kwa Sh162.7 bilioni.”

“Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 287.3 ya bajeti ya maendeleo iliyoidhinishwa na Bunge mwaka 2019/2020, lakini ni kutokana na kazi hiyo maalumu.”

Akizungumzia suala la uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba, Majaliwa alisema maandalizi yanakwenda vizuri na katika maboresho ya daftari la wapiga kura awamu ya kwanza waliandikishwa watu 10,285,732.

Alisema maandalizi yanahusisha kuboresha daftari la wapiga kura lililofanyika nchi nzima kati ya Julai 18, 2019 na kukamilika Februari 23, 2020.

“Kazi hiyo ilikwenda sambamba na ufutaji wa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo katika daftari la kudumu la wapiga,” alisema Majaliwa.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, waliofutwa baada ya kupoteza sifa ni 16,707 na akatumia hotuba hiyo kutangaza kuwa uboreshaji kwa awamu ya pili utaanza Aprili 5, 2020 na kukamilika Juni 26,2020.

“Natoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari hilo, ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka,” alisema.

Majaliwa aliwaomba viongozi wa vyama vya siasa kuonyesha mfano wa kuendesha siasa za kistaarabu zenye lengo la kuwaunganisha Watanzania na si kuwatenganisha kwa kuwa “hakuna kiongozi aliyewahi kupata sifa nzuri kwa kuwa chanzo cha mifarakano”.

Ahadi za Serikali

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema mambo mengi ambayo yaliahidiwa na Serikali ya awamu ya tano yametekelezwa sambamba na ahadi zilizomo katika ilani ya uchaguzi ya CCM 2015-2020.

Alisema ndani ya kipindi cha miaka mitano mafanikio makubwa yamepatikana na yamesaidia kuimarisha hali ya kiuchumi na kijamii ndani ya nchi ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi hususani ya usafiri na usafirishaji.

Alisema katika kipindi hicho, serikali ililenga kuwa na vipaumbele ambavyo ni ujenzi wa Reli ya SGR, ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania na ufufuaji wa mali za ushirika, ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, ulinzi wa maliasili na rasilimali na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu, afya na maji ambayo alisema yanapelekea mafanikio ya kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Aliliomba Bunge kuidhinisha Sh312.8 bilioni kwa ajili ya Ofisi yake zikiwamo za pamoja na shughuli za kimaendeleo.