Vincent Mashinji alivyoingia CCM

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole (kulia) akimueleza jambo aliyekuwa Katibu Mkuu Chadema, Dk Vicent Mashinji ambaye ameomba kujiunga CCM katika mkutano uliofanyika katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo Lumumba Jijini Dar es salaam. Picha na CCM

Dar es Salaam. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji jana alitangaza kuhamia CCM.

Video zilizosambazwa mitandaoni, zilimwonyesha Dk Mashinji akiingia katika ofisi ndogo za za CCM Lumumba jana asubuhi akiwa anatembea kutoka upande wa poli wa barabara.

Alikuwa amevalia suruali nyeusi na fulana yenye michirizi myekundu na myeusi ambayo hutumiwa kama sare ya Chadema huku akizungumza na simu.

Baada ya kufika mlangoni, alionekana kubabaika kidogo akitafuta mlango wa kuingilia, baadaye alitokea mtu aliyemwelekeza kuingia ndani.

Baadaye aliingia katika shughuli ya kumpokea mbele ya waandishi wa habari, ilioongozwa na Humphrey Polepole, katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM.

Akizungumzia kujiondoa kwa Chadema, Dk Mashinji alisema akiwa katika chama hicho aliandaa sera mbadala, lakini kwa bahati mbaya kulikosekana uelewa jinsi ya kuitekeleza.

Alisema kwa kuona upungufu huo, akaamua kutafuta chama mbadala anachoweza kuhamia badala ya kukaa na kulumbana asubuhi hadi jioni.

“Niliona ni heri nije hapa Lumumba, tuongee na kuona kama naweza kutoa mchango kwa taifa langu. Nimuombe mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kama ataridhia anipe nafasi ya kujiunga na CCM ili niweze kuchangia maendeleo ya nchi yangu,” alisema Dk Mashinji.

Baada ya hapo, Polepole alimpa fursa ya kwenda kubadilisha fulana, hivyo alivua sare ya Chadema na kuvaa shati la kijani linalotumiwa na CCM.

Akizungumza katika hafla hiyo, Polepole alisema “Mimi nikuhakikishie kwa niaba ya wakuu wa chama wakiongozwa na ndugu Magufuli nimekupokea rasmi karibu sana CCM.”

Katika mazungumzo yake na Mwananchi, Dk Mashinji akijibu swali aliloulizwa atakumbuka yapi akiwa Chadema, daktari huyo wa magonjwa ya binadamu na mtaalamu wa dawa za usingizi alisema, “nitaimisi sana sekretarieti yangu, wako vizuri na nawapenda sana.

“Ni wataalamu ingawa wako katika mazingira yanayowarudisha nyuma. Wanafanya kazi kitaalamu, wanashauri vizuri. Hao jamaa ni instrument sana ya chama...Kuondoka kwangu hakutakiwi kuwatisha, waendelee na shughuli zao.”

Pia alimwachia ujumbe mfupi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema, “Mbowe ajenge taasisi na si kujenga watu.”

Dk Mashinji aliteuliwa na Mbowe na kupitishwa na Baraza Kuu la Chadema Machi 12,2017 kuchukua nafasi ya Dk Slaa akiwa katibu mkuu wa nne.

Alichukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Willibrod Slaa ambaye alijiuzulu nafasi hiyo Septemba 1 mwaka 2015.

Dk Mashinji ni nani?

Dk Mashinji alizaliwa katika Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza. Alisoma elimu ya msingi katika Shule ya Iligamba Januari 1981 hadi Oktoba 1987 na kisha kuendelea na masomo katika Shule ya Sekondari ya Makoko Seminari kuanzia Januari 1988 mpaka Oktoba 1991.

Baada ya kuhitimu na kufaulu kujiunga na Shule ya Sekondari Mzumbe kati ya Julai 1992 hadi Juni 1994 alipohitimu kidato cha sita. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere Uganda mwaka 1995 hadi alipohitimu mwaka 2001 na kutunukiwa shahada ya udaktari.

Mwaka 2003 hadi 2005 alisomea Shahada ya Uzamili ya Anaesthesiology katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUHAS) na mwaka 2007-2010 alijiunga na Taasisi ya Teknolojia ya Blekinge ya Sweden ambako alisomea Shahada nyingine ya Uzamili, safari hii katika Utawala na Biashara (MBA).

Mwaka 2016 alikuwa mwanafunzi wa Shahada nyingine ya Uzamili katika Afya ya Jamii aliyosomea Chuo Kikuu cha Roehampton, Uingereza na pia Shahada ya Uzamivu ya Uongozi katika Chuo Kikuu Huria.