KESI YA KINA KITILYA: Watuhumiwa wawili kesi ya Kitilya wakataa tuhuma zote, wayakubali majina yao tu

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi, ya uhujumu uchumi inayomkabili mwenyekiti wa kampuni inayojihusisha na uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry Kitilya na wenzake wanne, umewasilisha vielelezo mahakamani vilivyothibitisha maelezo ya kesi hiyo dhidi ya washtakiwa wawili.

Uthibitisho huo uliwasilishwa jana na shahidi wa tatu katika kesi hiyo, kaimu mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Grace Sheshui wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo.

Washtakiwa hao ambao upande wa mashtaka ulithibitisha taarifa zao zilizoko kwenye maelezo ya mashtaka ni Bedason Shallanda (mshtakiwa wa nne) na Alfred Misana (mshtakiwa wa tatu) ambao hawakupinga maelezo ya ushahidi huo na mahakama ikaupokea na kuwa sehemu ya ushahidi.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Emmaculata Banzi katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Mbali na Kitilya, Shallanda na Missana, washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba 04 ya mwaka 2019 ni Shose Sinare na Sioi Solomon, ambao walikuwa maofisa wa Benki ya Stanbic.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 58, yakiwemo ya kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Dola 6 milioni, kujipatia fedha kiasi hicho kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato wa kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekeni 550milioni kutoka Benki ya Standard ya nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Shallanda na Misana wote walikuwa ni watumishi wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Shallanda akiwa Kamishna wa Sera na Misana akiwa Kaimu Kamishna wa Kitengo cha Madeni, ndani ya idara hiyo ya sera.

Wakati wa usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo, washtakiwa walisomewa mashtaka na kutakiwa kuyajibu kwa mara ya kwanza kwa kukubali au kukataa na kisha wakasomewa maelezo ya kesi, washtakiwa hao, wote walikana maelezo mengine isipokuwa majina yao tu.

Kwa upande wa Shallanda, upande wa mashtaka ulieleza kuwa alikuwa Kamishna wa Sera na mwenyekiti wa Kamati ya Kitaalamu ya Usimamizi wa Madeni (TDMC), na wakati huohuo akiwa ni Katibu wa Kamati ya Taifa ya Usimamizi wa Madeni (NDMC).

Kwa upande wa Misana, upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa alikuwa Kamishna Msaidizi wa Kitengo cha Madeni na pia katibu wa TDMC huku pia akiwa mjumbe wa NDMC.

TDMC ni kamati inayotoa ushauri wa kitaalamu kwa NDMC kuhusu ukopaji ndani na nje na NDMC ni kamati inayomshauri Waziri wa Fedha kuhusu suala la ukopaji ndani na nje ili kufidia upungufu katika bajeti ya Serikali kwa lengo la kutekeleza miradi mbalimbali.

Pia upande wa mashtaka uliieleza mahakama namna washtakiwa hao wawili kwa nafasi zao walivyoshirikiana na washtakiwa wengine katika kutenda makosa hayo.

Walipotakiwa kubainisha mambo wanayokubaliana nayo na wasiyokubaliana nayo katika maelezo hayo, washtakiwa hao walikubali majina yao tu na maelezo mengine yote wakayakana, zikiwemo nafasi zao za utumishi wa umma na majukumu yao, na kuupa jukumu upande wa mashtaka kuleta mashahidi kuthibitisha maelezo hayo waliyoyakana.

Lakini jana shahidi huyo wa tatu wa upande wa mashtaka aliwasilisha mahakamani vielelezo vya ushahidi kuthibitisha kuwa washtakiwa hao walikuwa ni watumishi wa wizara hiyo na nafasi zao pamoja na majukumu yao.

Kabla ya shahidi Sheshui, ushahidi wa utumishi wa washtakiwa hao, nyadhifa na majukumu yao yalielezwa mahakamani na shahidi wa kwanza, Mustafa Mkulo, waziri wa zamani wa Fedha na Uchumi na shahidi wa pili, Kaimu Kamishna wa Sera, Mgonya Benedict.

Tofauti na Mkulo na Benedict, ambao walieleza kwa maneno matupu, Sheshui aliwasilisha mahakamani vielelezo vya nyaraka kuthibitisha maelezo yake.

Nyaraka hizo ni barua za uteuzi wao kushika nafasi hizo, ambazo zimeonyesha mamlaka iliyowateua, tarehe ya kuandikwa, tarehe ya kuanza uteuzi, majukumu yao, mishahara na stahiki nyinginezo.

Barua ya kwanza ni ya Shallanda iliyoandikwa na aliyekuwa katibu mkuu wa wizara hiyo, Ramadhani Khijja (sasa marehemu) Oktoba 15, 2010, ikieleza kuwa ameteuliwa kuwa kamishna wa Sera na kwamba uteuzi wake ulianza tangu Oktoba Mosi, 2013.

Barua hiyo pia inaeleza mshahara wake ni Sh2,062,000, mkopo wa gari aina ya saloon (gari ndogo), nyumba na samani, Sh205,000 kwa umeme na mawasiliano Sh180,000, huku majukumu yake yakiwa ni utafutaji wa vyanzo vya fedha kufidia upungufu wa bajeti na kuhakikisha deni la taifa linakuwa himilivu.

Kwa Misana barua ya uteuzi wake iliandikwa na kaimu katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Servacius Likwelile, Juni 19, 2013, ikieleza kuwa uteuzi wake utaanza Agosti Mosi, 2013. Pia ilieleza kuwa mshahara wake utakuwa Sh2,900,000, mkopo wa kununua gari aina ya saloon, nyumba na samani zake, Sh205,000, kwa ajili ya malipo ya umeme na mawasiliano Sh180,000.

Washtakiwa wenyewe pamoja na wakili wao hawakuzipinga barua hizo na hivyo mahakama ikazipokea na kuwa sehemu ya ushahidi wa upande wa mashtaka.

Katika hatua nyingine kuliibuka mabishano makali ya kisheria kati ya mawakili wa pande zote kuhusu upokeaji wa vielelezo vingine vya upande wa mashtaka.

Mvutano huo uliibuliwa na upande wa utetezi wakipinga mahakama kupokea nyaraka mbili ambazo shahidi huyo aliomba kuziwasilisha ili nazo ziwe sehemu ya ushahidi wa upande wa mashtaka.

Nyaraka hizo ni barua iliyoandikwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ya Januari 14, 2016 iliyokuwa ikimtaka awasilishe nyaraka mbalimbali kuhusiana na mchakato wa mkopo huo na barua yake (shahidi) akijibu barua ya Takukuru.

Awali akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Hashim Ngole, shahidi huyo alieleza kuwa mwaka 2016 aliandikiwa barua na Takukuru akitakiwa awasilishe nyaraka hizo na kwamba kwa kuwa nyaraka nyingine zilishawasilishwa, hivyo aliwasilisha nyaraka moja tu na akajibu kwa barua.

Alibainisha kuwa nyaraka hiyo aliyoiwasilisha yenye muhtasari wa kikao cha 61 cha TDMC, na akiongozwa na Wakili Ngole akaiomba mahakama hiyo izipokee barua hizo ziwe sehemu ya ushahidi.

Hata hivyo Wakili wa Kitilya, Majura Magafu alipinga barua hizo kupokewa, akiungwa mkono na mawakili wengine wa utetezi na hivyo kuibua mvutano mkali huku upande wa mashtaka ukiiomba mahakama hiyo itupilie mbali pingamizi hilo kwa madai kwamba halina mashiko.

Jaji Banzi baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha kesi hiyo hadi leo atakapotoa uamuzi.

Mbali na kuwa mwenyekiti wa Egma, Kitilya aliwahi kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mshitakiwa mwingine, Shose Sinare ni Miss Tanzania wa mwaka 1996.