TPSF yataka sera ya vijana kuanzisha biashara bila masharti ya benki

Mkurugenzi wa  TPSF, Godfrey Simbeye

Muktasari:

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imeitaka Serikali kuanzisha sera maalum itakayowawezesha vijana kujiajiri bila masharti magumu ya Benki.

Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imeitaka Serikali kuanzisha sera maalum itakayowawezesha vijana kujiajiri bila masharti magumu ya Benki.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Novemba 2, 2019 na mkurugenzi wa  TPSF, Godfrey Simbeye katika mdahalo wa ajira na Tanzania ya viwanda ulioandaliwa na taasisi ya Viva Legacy.

Simbeye amesema idadi ya vijana wanaoingia kwenye soko la ajira ni kubwa kuliko uwezo wa kuajiri.

“Viwanda kwa sasa vipo 57,000 nchi nzima lakini vijana wanaoingia kwenye ajira wako 1.2 milioni. Serikali imeajiri watu wasiozidi 600,000, hao waliobaki wanatakiwa kwenye sekta binafsi. Wengi wanaishia kwenye sekta isiyo rasmi,” amesema Simbeye.

Amesema hadi sasa  Tanzania kuna kampuni takribani 160,000 zilizosajiliwa alizodai hazitoshi kuchukua idadi kubwa ya vijana wanaotafuta ajira.

“Tuje na programu makini ya kuwafanya vijana wajiajiri, tuwe na mazingira ya kuwawezesha wajiajiri kirahisi. Kwanini kijana apewe masharti kama ya kijana wa China anayekuja kuwekeza na fedha nyingi? Kuwe na mchakato tofauti wa kuwawezesha vijana kujiajiri kirahisi,” amesema.

Amesema India mtu akianzisha kiwanda baada ya miaka saba ndio anaanza kulipa kodi, jambo ambalo kwa Tanzania halipo.

“Sisi ukishapewa TIN (Namba ya utambulisho wa kodi) unaambiwa ulipe kodi ya awali. Sasa huyu kijana atapata wapi hela? Kijana anakwenda kuomba mkopo anaambiwa lete hati ya nyumba ataitoa wapi? Kijana anaambiwa alipe kodi ya miaka mitatu. Tuwe na sera itakayowezesha vijana wanaoanzisha biashara,” amesema Simbeye.