Magufuli: JK zididisha safari za nje baba

Muktasari:

“Wapo wanaosema wewe Rais unatembea sana nje ya nchi, lakini bila kutembea kwako tusingepata maendeleo tunayopata, hivyo tunakuomba uendelee kutembea ili tuendelee kupata maendeleo zaidi,” alisema Dk Magufuli.

Manyara
WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuongeza safari za nje, kwa sababu zinazochochea maendeleo kwa kasi nchini.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara kwenye ufunguzi wa Barabara ya Minjingu- Babati-Singida juzi, Dk Magufuli alisema Rais Kikwete ametekeleza ahadi zilizopo kwenye ilani ya CCM ya mwaka 2010.

“Wapo wanaosema wewe Rais unatembea sana nje ya nchi, lakini bila kutembea kwako tusingepata maendeleo tunayopata, hivyo tunakuomba uendelee kutembea ili tuendelee kupata maendeleo zaidi,” alisema Dk Magufuli.

Pia, aliwataka wananchi hasa wafugaji mkoani hapa kuhakikisha wanaitumia vizuri barabara hiyo, ili kuitunza na wasiiharibu.

Waziri Magufuli alisema vyema wakafuata sheria za barabarani, ikiwamo kupeleka mifugo maeneo yasiyo na vivuko na kwamba, hiyo itawaepushia hasara ya mifugo yao kugongwa na vyombo vya usafiri.

Akizindua barabara hiyo, Rais Kikwete alisema shabaha ya Serikali ni kuwatumikia wananchi wake kwa kutekeleza ahadi ilizotoa na kwamba, anapenda kila Mtanzania aishi maisha bora.

“Sipendi nipige hatua huku wenzangu wakibaki maskini, wapo waliokuwa wanadai wanatetea haki za Wamasai ili wapate huduma muhimu za jamii, lakini wakati huohuo wao ndiyo waliokuwa wakinufaika, huku wenzao wakiwa hawana wanachokipata kwa utetezi wao,” alisema Rais Kikwete.

Baada ya kufungua barabara hiyo, Dk Kikwete alisema Serikali yake imelenga kuunganisha mikoa yote kwa barabara za lami na kuahidi kuwa, kazi iliyobaki hivi sasa ni kuunganisha barabara ya Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Dodoma, ambayo ujenzi wake tayari umeanza.

“Nimeahidi kujenga barabara ifikapo mwaka 2015 CCM ikiingia madarakani iweze kumalizia patakapobaki, kwani nina uhakika hakuna chama kingine kitakachoweza kushika madaraka nchini zaidi ya CCM,” alisisitiza.

Pia, alisema iwapo kutakuwa na ahadi zitakazoshindwa kutekelezwa kipindi cha uongozi wake, hakuna sababu ya wananchi kuilaumu Serikali kwani yapo mengine ya miaka ya nyuma ambayo alianza nayo.

“Kama yale niliyoahidi sitaweza kuyatimiza yote, lakini baadhi nimeshayafanya kwani mengine ni ya miaka 20 iliyopita,” alisema Rais Kikwete.