Kesi ya Kitilya sasa yaiva Mahakama ya Ufisadi

Muktasari:

Ile kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili Kamishna Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanne, akiwemo mshindi wa taji la urembo nchini (Miss Tanzania 1996) Shose Sinare ambayo hapana shaka usikilizwaji wake umekuwa ukisubiriwa si tu na washtakiwa ambao hadi sasa wako mahabusu, bali na umma kwa jumla sasa itaanza kusikilizwa juma lijalo. 

Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili Kamishna Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanne, sasa imeiva baada ya kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa rasmi Jumatatu ijayo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Kitilya na wenzake wamekuwa mahabusu kwa miaka mitatu sasa tangu Aprili Mosi, 2016 walipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Dar es Salaam Kisutu Tanzania, kwa ajili ya kukamilisha upelelezi.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba 01 ya mwaka 2019, ni mshindi wa Mashindano ya Urembo (Miss Tanzania), mwaka 1996, Shose Mori Sinare na Sioi Graham Solomon, ambao walikuwa maafisa wa Benki ya Stanbic.

Vilevile, kuna maofisa wawili wa zamani wa Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda,  ambaye kwa sasa yuko  Ofisi ya Waziri Mkuu na  Alfred Misana, ambaye kwa sasa yuko  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.

Wamekaa mahabusu kwa muda wote huo wakisubiri kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha, ambayo hayana dhamana.

Hata hivyo, kesi hiyo itaanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka siku sita zijazo kutoka leo Jumatano, Julai 3, 2019.

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya mahakama hiyo, kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa na Jaji Emmaculata Banzi mfululizo kuanzia Julai 8 hadi Julai 18, 2019.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 58, yakiwamo ya kuisababishia  Serikali hasara ya Dola 6 milioni, kujipatia fedha kiasi hicho kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uwongo, kujipatia, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato wa kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya nchini Uingereza.