Basi la Mwendokasi lateketea kwa moto Dar

Muktasari:

 Basi la Kampuni ya Mwendo Haraka (Udart) maarufu 'Mwendokasi' linalotoa huduma ya usafiri jijini Dar es Salaam nchini Tanzania limetekelea kwa moto eneo la Kimara Mwisho. Hakuna madhara ya kibinadamu yaliyoripotiwa.

Dar es Salaam. Basi la Kampuni ya Mwendo Haraka (Udart) maarufu 'Mwendokasi' lililokuwa likitoka Mjini kwenda Kimara Mwisho Dar es Salaam nchini Tanzania limeteketea lote kwa moto.

Tukio hilo limetokea leo usiku  wa Jumapili Septemba 1, 2019 eneo la Kimara Mwisho na kusababisha adha kwa watumiaji wa usafiri huo huku watu wengi wakijitokeza kushuhudia basi hilo ambalo limetekelea lote.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Teopista Malya amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokana na ajali hiyo.

Kamanda Malya amesema basi hilo lilitoka Mjini likiwa na abiria na lilipofika eneo la Kimara Mwisho walifanikiwa kushuka kabla halijateketea kwa moto.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na kukusanya taarifa zaidi za ajali hiyo, ikiwemo hasara iliyosababishwa na ajali hiyo.

Tukio hili si la kwanza kwa basi la Udart kuwaka moto kwani huko nyuma eneo la Ubungo Dar es Salaam liliwahi  kutokea ila uliwahi kufhibitiwa.

 
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi